TANZANIA YAONGOZA KWA UWEKEZAJI AFRIKA MASHARIKI, SERIKALI YAONGEZA NGUVU UZALISHAJI WA MAFUTA...! - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday, 5 April 2019

TANZANIA YAONGOZA KWA UWEKEZAJI AFRIKA MASHARIKI, SERIKALI YAONGEZA NGUVU UZALISHAJI WA MAFUTA...!

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Tanzania inaongoza kwa uwekezaji katika Afrika Mashariki na imeweza kuvutia uwekezaji wenye thamani ya dola za Marekani bilioni 1.18, ikifuatiwa na Uganda dola za Marekani bilioni 0.7 na Kenya dola za Marekani bilioni 0.67.

“Kutokana na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali kuvutia uwekezaji nchini, hali ya uwekezaji imeimarika ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika Mashariki. Ripoti mbalimbali za uwekezaji duniani zinaonesha kuwa Tanzania imeongoza kwa kuvutia uwekezaji miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki,” amesema.

Ametoa kauli hiyo Alhamisi, Aprili 4, 2019 Bungeni jijini Dodoma, wakati akiwasilisha taarifa ya mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2019/2020 kwenye mkutano wa 15 wa Bunge.

Amesema Taarifa ya Uwekezaji ya Dunia (World Investment Report) ya mwaka 2018 inayotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo (UNCTAD) imebainisha kiasi hicho kikubwa cha uwekezaji.

“Taarifa nyingine ya“The Africa Investment Index (AII) 2018” inaonesha kuwa Tanzania imeshika nafasi ya 13 kati ya nchi 54 za Afrika katika kutoa fursa za masoko na vivutio vya uwekezaji.”

Vilevile, Waziri Mkuu amesema kuwa taarifa ya “Where to Invest in Africa” ya mwaka 2018, nayo imeonesha kuwa Tanzania imeshika nafasi ya saba kati ya nchi 52 zinazovutia zaidi kwa uwekezaji barani Afrika.

Kutokana na uwekezaji huo mkubwa, Waziri Mkuu amewataka Watanzania wachangamkie fursa zinazojitokeza kutokana na ukuaji wa uchumi, maendeleo ya kijamii na pia uwekezaji wa sekta ya umma kwenye miundombinu kwa kuthubutu kuwekeza kwenye uzalishaji wa bidhaa na utoaji wa huduma.

Amesema katika mwaka wa fedha wa 2019/2020, Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara ikiwemo kutekeleza mapendekezo ya Mpango Kazi Jumuishi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji nchini. Pia itakamilisha mapitio ya Sera ya Taifa ya Uwekezaji na Sheria ya Uwekezaji.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema uhamasishaji wa miradi ya kisekta ndani na nje ya nchi, umefanikisha kuvutia uwekezaji kwenye sekta mbalimbali za kimkakati na unatarajia kuwekeza mitaji ya jumla ya dola za Marekani bilioni 1.84 na kuzalisha ajira mpya 15,491.

“Hadi kufikia Februari, 2019 jumla ya miradi mipya 145 ilisajiliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC). Kati ya miradi hiyo, miradi 104 sawa na asilimia 72 inamilikiwa na wawekezaji wa ndani; miradi 38 sawa na asilimia 26 inamilikiwa na wawekezaji kutoka nje na miradi mitatu sawa na asilimia 2.01 ni ya ubia,” amesema.

Akizungumzia kuhusu zoezi la utoaji wa vitambulisho kwa wajasiriamali wadogo nchini, Waziri Mkuu amesema Serikali imekusanya shilingi bilioni 9.9 tangu kuanzishwa kwa utaratibu huo Desemba, 2018.

“Hadi tarehe 10 Machi 2019, jumla ya vitambulisho 496,221 sawa na asilimia 74 vilikuwa vimegawiwa kwa wajasiriamali wadogo katika mikoa yote nchini.” Amesema hatua hiyo ilichukuliwa ikiwa ni kutambua umuhimu wa wajasiriamali wadogo nchini katika kuchangia pato la Taifa na kukuza uchumi

“Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitoa vitambulisho 670,000 kwa ajili ya wajasiriamali wadogo ambao mitaji yao haizidi shilingi milioni nne. Lengo la kutoa vitambulisho hivyo vyenye kugharimu shilingi 20,000 kwa kila kimoja ni kuwatambua, kuwaandalia maeneo ya kufanya biashara bila usumbufu wowote na kuziwezesha Mamlaka za Serikali za Mitaa kuongeza mapato ya ndani,” amesema.

WAKATI HUO HUO; UZALISHAJI mdogo wa zao la Michikichi ni miongoni mwa sababu za kushindwa kujitosheleza kwa mahitaji ya mafuta ya kula nchini na Serikali imekuwa ikilazimika kutumia fedha nyingi za kigeni kwa ajili ya kununua mafuta  hayo kutoka nje ya nchi.

Kutokana na changamoto hiyo, Serikali imeamua kuweka nguvu kubwa kwenye uzalishaji wa mazao ya mbegu za mafuta ili kuondokana na utegemezi na kuokoa matumizi ya fedha za kigeni.

Hayo yamesemwa Aprili 4, 2019 na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akiwasilisha hotuba ya Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2019/2020.

Waziri Mkuu amesema katika kutekeleza azma hiyo, Serikali imeanza kuimarisha kilimo cha zao la michikichi hususan katika mkoa wa Kigoma ili kusaidia upatikanaji wa mbegu bora za chikichi.

Amesema lengo ni kuzalisha na kusambaza kwa wakulima miche ipatayo milioni 20 katika kipindi cha miaka minne (2018/2019 hadi 2021/2022), pia Serikali imeamua kukifanya Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kihinga, mkoani Kigoma kuwa Kituo cha Utafiti wa Mbegu Bora za michikichi.

“Maamuzi haya ya Serikali yameanza kuzaa matunda, hadi kufikia Februari 2019, Kituo cha Kihinga kimezalisha mbegu 4,747 ambazo zimefanyiwa uoteshwaji wa awali. Katika mwaka 2019/2020, Serikali imepanga kuzalisha miche ya michikichi milioni tano.”

Waziri Mkuu amesema matarajio ya Serikali ni kuhakikisha kwamba usimamizi mzuri wa mkakati huo wa miaka minne utalisaidia Taifa kuondokana na uagizaji wa mafuta ya kula kutoka nje, kutengeneza fursa mbalimbali za ajira na kuwaongezea kipato wakulima wa michikichi.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema hali ya uzalishaji wa mazao ya chakula kwa msimu wa 2017/2018 na upatikanaji wa chakula kwa mwaka 2018/2019, imeendelea kuimarika.

Waziri Mkuu amesema hatua hiyo imetokana na hali nzuri ya mvua katika maeneo mengi ya nchi, kuongezeka kwa tija na uzalishaji. “Uzalishaji wa mazao ya chakula umefikia tani milioni 16.89 ikilinganishwa na mahitaji ya chakula ya tani milioni 13.57 na kufanya nchi kuwa na ziada ya chakula ya tani milioni 3.32.”

Amesema uzalishaji wa mazao makuu ya kimkakati yakiwemo chai, kahawa, korosho, pamba na tumbaku umeimarika kutokana na juhudi zinazofanywa na Serikali ikiwemo kuimarisha ushirika.

“Kwa mfano, uzalishaji wa zao la pamba uliongezeka kutoka tani 132,934 mwaka 2017/2018 hadi kufikia tani 222,039 mwaka 2018/2019 wakati uzalishaji wa zao la Kahawa uliongezeka kutoka tani 45,245 hadi kufikia tani 65,000.”

Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kutoa kipaumbele kwa mazao hayo na mengine kwa kuwa ndiyo mhimili wa kutoa malighafi za kuendesha viwanda na yana mnyororo mpana wenye fursa ya kutoa ajira nyingi na kuliingizia Taifa fedha za kigeni.

No comments:

Post a Comment