BENKI ya NMB imedhamini Mashindano maalum ya Mchezo wa Golf ya Mkuu wa Majeshi nchini yanayotarajia kufanyika Oktoba 13 na kushirikisha wachezaji wa gofu kutoka klabu mbalimbali nchini.
Udhamini uliotolewa ni wa shilingi milioni 26 pamoja na vifaa mbalimbali zikiwemo jezi zitakazo tumika katika mashindano hayo vimekabidhiwa jana jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Kitengo cha Wateja wadogo na wa kati wa benki ya NMB, Omari Mtiga katika viwanja vya Lugalo.
Kukabidhiwa kwa udhamini huo ni mwendelezo wa Benki ya NMB kudhamini na kusaidia shughuli anuai za michezo hususani ya Jeshi la wananchi.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mara baada ya kukabidhiwa kwa udhamini huo, Makamu Rais wa Umoja wa Klabu za Golf Tanzania, Luteni Canali David Luoga alisema mashindano hayo yanatarajia kushirikisha wachezaji kutoka vilabu mbalimbali vya golf Tanzania na makundi ya wachezaji wakiwemo watoto.
Alisema mashindano hayo ambayo yatafanyika kwa siku moja pekee na kufunguliwa na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama (JWTZ), Jenerali Venance Mabeyo washindi watajipatia fedha taslimu pamoja na vikombe.
Aliongeza kuwa mashindano hayo yatakuwa na mvuto wa pekee kwa kile kushirikisha viongozi waandamizi mbalimbali kutoka Serikalini waliostaafu na awaliopo madarakani.
"Kama unavyofahamu klabu yetu ya mchezo wa golf inashirikisha pia viongozi mbalimbali waandamizi kutoka Serikalini waliostaafu na wengine bado wapo madarakani nao tunatarajia watashiriki katika mashindano haya...hivyo yatakuwa na mvuto wa kipekee," alisema Luteni Canali Luoga.
No comments:
Post a Comment