Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Mpwampwa, kwenye ukumbi wa chuo cha uwalimu Mpwapwa mkoani Dodoma, Oktoba 10, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu). |
*Amuagiza mkuu wa wilaya afanye uchunguzi ....
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Bw. Jabir Shekimweri afanye uchunguzi kuhusu matumizi ya sh. milioni 70 zinazotelewa kila mwezi na Serikali kwa ajili ya kununulia dawa kwenye wilaya hiyo.
"Kilichokuwa kinasemwa na wabunge bungeni nilidhani sicho, nikasema nakuja niyasikie mwenyewe. Kweli wananchi hawaridhiki nimeona. Sasa mkuu wa wilaya shughulikia hili jambo ili kubaini fedha za dawa zinakwenda wapi.”
Alitoa agizo hilo Oktoba 10, 2018 wakati akihutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa shule msingi Mpwapwa, ambapo alipokea malalamiko ya wananchi juu ya ukosefu wa dawa. Dawa pekee wanazopewa ni za kutuliza maumivu tu.
Waziri Mkuu alisema lengo la Serikali kutoa fedha hizo kila mwezi ni kuhakikisha kwamba wananchi wote wanapata huduma za afya popote walipo badala ya kusafiri umbali mrefu kwenda makao makuu ya wilaya.
"Kila mwezi Serikali inatoa zaidi ya sh milioni 70 kwa ajili ya kununulia dawa kwenye wilaya hii ya Mpwapwa. Pia kuna fedha za mfuko wa afya sh. milioni 60 pamoja na fedha za matokeo mazuri ya afya sh. milioni 300 kwa mwaka, shida ya dawa haitakiwi kuwepo hapa.”
Waziri Mkuu alibainisha kuwa Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imedhamiria kuwatumikia wananchi ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuwapatia mahitaji muhimu kama huduma bora za afya na ndiyo sababu ya kutoa fedha hizo za dawa.
Awali, kabla ya mkutano huo, Waziri Mkuu alimuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mpwawa, Bw. Paul Swea kuwahamishia vijijini baadhi ya watumishi waliopo kwenye idara ya kilimo. Hatua imekuja baada ya kubaini idara hiyo ina watumishi saba ambao wote wapo ofisini badala ya kuwepo vijijini na kuwasaidia wananchi kwenye shughuli za kilimo.
Alimtaka mkurugenzi huyo kuandika barua za uhamisho kwa watumishi hao kwenda vijijini kisha nakala za barua hizo akabidhiwe kabla hajaondoka wilayani Mpwapwa, ambapo alisisitiza kuwa watumishi hao wanapaswa kwenda kufanyakazi na wakulima kwa karibu na kuhakikisha wanawapa elimu ya kutosha itakayowawezesha kulima kwa kisasa.
No comments:
Post a Comment