HAKI ZA DEREVA KWA MUJIBU WA SHERIA...! - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday, 30 March 2021

HAKI ZA DEREVA KWA MUJIBU WA SHERIA...!

Dereva barabarani.

 HAKI ZA DEREVA KWA MUJIBU WA SHERIA.

DEREVA ni mfanyakazi, hivyo ana haki zake kwa mujibu wa Sheria ya Kazi (Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini) au kwa Kiingereza “The Employment and Labour Relations Act(ELRA), Cap 366). Ni Wajibu wa Mfanyakazi Mwenyewe kuzijua haki hizi na Kuzidai. Na pia Kwa mujibu wa Kifungu cha 16 cha Sheria ya Kazi, ni wajibu wa Mwajiri Kumjulisha au kumwonesha mfanyakazi haki hizi ili azijue. Haki hizo ni zifuatazo:

1. HAKI YA KUTOBAGULIWA.

Ubaguzi wa aina yoyote umekatazwa na kifungu cha 7 na 8 cha Sheria. 


2. HAKI YA KUJUMUIKA (Right to exercise freedom of association)

Haki hii ni kwa mujibu wa Katiba na imetajwa pia katika kifungu cha 9 cha sharia ya kazi. Dereva ana haki ya kujiunga au kutoka kwenye chama chochote cha wafanyakazi au cha madereva. 


3. HAKI YA KUPEWA MKATABA au MAELEZO YA KAZI (Right to be supplied with the Contract of Service/Statement of Particulars). Kama hana mkataba basi apewe maelezo ya kazi anayofanya.

Haki hii imetambuliwa kwenye kifungu cha 14 na 15 cha Sheria ya Kazi. 


4. HAKI YA KUJULISHWA HAKI ZAKE.

Ni haki ya dereva au mfanyakazi yeyote kujulishwa haki zake na mwajiri. Hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 16 cha Sheria. Mwajiri anaweza kumjulisha kwa kumpa maandishi yanayoonesha haki zake, kubandika ukutani au kuweka kwenye mkataba wa kazi. 


5. HAKI YA LIKIZO YA MWAKA (Right to annual leave)

Haki hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 31 cha Sheria. Likizo ni siku 28 kwa mwaka na inaweza kuchukuliwa kwa awamu. 


6. HAKI YA LIKIZO YA UZAZI/ULEZI/UGONJWA (Right to maternity/paternity/sick leave)

Haki hii imetambuliwa na kifungu cha 32,33, na 34 cha Sheria ya Kazi. Uzazi ni siku 84 kwa wanawake na kwa wanaume ni siku 3. Likizo ya ugonjwa ni siku 126. 


7. HAKI YA KUPATA CHETI CHA UTUMISHI BAADA YA KUACHA/KUACHISHWA KAZI(Right to certificate of service on termination)

Haki hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 44 cha Sheria ya Kazi. 


8. HAKI YA UJIRA (Right to remuneration and written statement of particulars supporting each payment of remuneration)

Haki hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 27 cha Sheria, Na kwa sekta ya usafirishaji mshahara kima cha chini kwa mweiz ni shilingi 200,000. 


9. HAKI YA KUTOKATWA MSHAHARA BILA RIDHAA

Isipokuwa kwa makatao ya kisheria, Mfanyakazi anayo haki ya kutokatwa mshahara bila ridhaa yake. Hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 28(2)(e) cha Sheria. Na hata pale atakapokubali kukatwa, makato hayatakiwi kuzidi ¼ ya mshahara wa mfanyakazi. 


10. HAKI YA KULIPWA MUDA WA ZIADA WA KAZI (Right to payment for the overtime worked and night work allowance)

Hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 19 cha sheria. 


11. HAKI YA KUFANYA KAZI MASAA YASIYOZIDI 9 KWA SIKU NA 45 KWA WIKI.

Hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 19 cha Sheria ya Kazi 


12. HAKI YA MAPUMZIKO WAKATI WA KAZI

Mfanyakazi anatakiwa kupumzika dakika 60 kila siku wakati wa kazi. Na hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 23cha Sheria. 


13. HAKI YA MAPUMZIKO (Right to daily and weekly rest periods as provided for in the Act)

Hii ni haki kwa mujibu wa kifungu cha 24 cha sheria. Mfanyakazi anatakiwa kupumzika kwa muda wa masaa 12 tangu kwisha kwa kazi na kuanza kwa kazi siku nyingine. Na pia anastahili mapumziko ya mwisho wa wiki. 


14. HAKI YA KUPUMZIKA SIKU ZA SIKUKUU AU KULIPWA MARA MBILI.

Sheria inampa mfanyakazi haki ya kupumzika wakati wa sikukuu za umma au ikilazimika afanye kazi basi alipwe ujira mara mbili ya siku hiyo. Yaani kama ni 5000 kwa siku basi alipwe 10,000. Hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 25 cha Sheria. 


15. HAKI YA KUREJESHWA ALIKOTOKEA BAADA YA KUACHISHWA KAZI (Right to be repatriated to place of recruitment on termination)

Hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 43 cha sharia. 


16. HAKI YA MALIPO KATIKA KIPINDI ALICHOACHISHWA KAZI NA KUSUBUIRI KUSAFIRISHWA NYUMBANI (Right to daily subsistence allowance between termination date and the date of transporting an employee and family to the place of recruitment) 


17. HAKI YA KUPEWA TAARIFA YA KUACHISHWA KAZI

Mfanyakazi anastahili notisi ya kuachishwa kazi kwa mujibu wa sharia au malipo badala ya notisi. 


18. HAKI YA KUSIKILIZWA KABLA YA KUCHUKULIWA HATUA KWA MAKOSA YA NIDHAMU

Mfanyakazi anayo haki ya kujulishwa kosa lake, kujitetea/kusikilizwa kwa kosa lake kabla ya kuchukuliwa hatua  za kinidhamu. 


19. HAKI YA KULIPWA KIINUA MGONGO

Mfanyakazi ana haki ya kulipswa kiinua mgongo iwapo hakuachishwa kazi kwa makosa ya utovu wa nidhamu na iwapo atakuwa amefanya kazi kwa mwajiri huyo huyo miezi 12 mfululizo. 


20. HAKI NYINGINE ZOZOTE ZINAZOTOLEWA KWA MUJIBU WA SHERIA (Any other rights as provided for under the Act) au makubaliano ya kimktaba kati ya Mwajiri na mwajiriwa. 


Ni Imani yangu Makala hii imekuongezea maarifa kuhusu haki zako kazini. Ni wajibu wako sasa kuzifuatilia haki hizi. Siku zote HAKI INADAIWA. 

No comments:

Post a Comment