Mkuu wa Kitengo cha Malipo Kidijitali wa Halotel, Emmanuel Golden (kushoto) akifanya malipo ya bidhaa aliyonunua dukani kupitia mtandao wa Halopesa na Visa. |
KAMPUNI za Halotel Tanzania na Visa zimesaini mkataba wa kimkakati ambao utawawezesha watumiaji wa Halopesa kufanya malipo kwa njia ya Visa kupitia simu zao. Ushirikiano kati ya kampuni hizo utawezesha watumiaji wa Halopesa kutumia huduma ya Visa kwenye simu zao kwa kufanya malipo ya bidhaa na kuweka pesa na kutoa kwa mawakala wa huduma ya Visa.
Takwimu kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) iliyotoa mwaka 2018 inasema kuwa Halopesa ni huduma ya malipo kwa njia ya simu inayokua kwa kasi sana hapa Tanzania.
Idadi ya wateja waliojisajili kwa huduma ya Halopesa imeongezeka kwa kiasi cha asilimia 71.76 katika kipindi cha mwaka 2018. Kampuni ilifunga mwaka 2017 ikiwa na jumla watumiaji wa Halopesa wapatao 780,000. Idadi hiyo imeongezeka kwa kiasi kikubwa hadi kufikia jumla ya watumiaji milioni 1.3 mwishoni mwa mwaka 2018.
“Kwa ukuaji mkubwa wa idadi ya wateja wa Halotel na kuwa ni mtandao wa simu unaokua kwa haraka hapa Tanzania tangu tuanze kutoa huduma hapa nchini, tuna imani kwamba idadi ya watumiaji wa Halopesa pia itaendelea kuongezeka,” amesema Naibu Mkurugenzi wa Halotel, Nguyen Tien Dung.
Bw. Dung amesema kuwa kwa sasa Halopesa ina zaidi ya mawakala 40,000 na kwamba nguvu ya huduma ya Visa inaipa Halopesa thamani na uwezo zaidi wa kuwezesha wateja kufanya manunuzi kwa njia ya Visa kupitia simu zao.
“Kupitia ushirikiano huu, Halopesa itawapa wateja kulipa kwa muuzaji kwa kutumia msimbo (code) iliyoko kwenye huduma ya Visa kwenye simu zao. Huduma hii ya Visa katika simu huwezesha wateja kupata fedha zao moja kwa moja kutoka katika akaunti zao za benki kupitia simu zao na kulipia bidhaa kwa wauzaji, kutuma pesa bila gharama yoyote, kuweka pesa au kutoa pesa kupitia wakala yeyote wa huduma ya Visa,” amesema na kuhitimisha Bw. Son.
Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Visa nchini Tanzania Olive Njoroge, ameelezea kuwa ushirikiano huo unalenga zaidi katika kuunganisha Watanzania kwenye huduma ya Visa na kuleta usalama wa fedha zao kufanya malipo fanisi kwa huduma na bidhaa.
‘Tunafarijika kwa ushirikiano huu kati yetu na kampuni muhimu ya huduma za mawasiliano ya simu kama Halotel. Ushirikiano wetu na Halotel utawafanya Watanzania kulipa kwa kutumia Visa katika simu zao kupitia zaidi ya wachuuzi wapya 40,000. Pia itawasaidia kupanuka kwa wigo wa Watanzania wanaotumia huduma za kifedha hapa nchini,” amesema Bi. Njoroge.
Kupitia huduma ya Visa, muuzaji atapewa msimbo (QR code) pamoja na namba maalum ya wakala ambayo mteja ambaye simu yake ina huduma ya Visa ataitumia kwa ajili ya malipo kupitia simu yake.
Ushirikiano huu unadhihirisha nia ya dhati ya VISA kutanua wigo wa malipo kupitia Huduma za kifedha kwa njia ya simu Ulimwenguni kote.
No comments:
Post a Comment