WAZIRI Mkuu Kassim
Majaliwa amefanya mazungumzo rasmi ya kiserikali na mgeni wake, Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Korea, Lee Nak-yon ambaye yuko hapa nchini kwa ziara ya kikazi
ya siku tatu.
Viongozi hao wawili,
kwa pamoja, Julai 22, 2018 wameshuhudia uwekaji saini mkataba wa kuondoa hitaji
la viza kwa watu wenye hati za kusafiria za kidiplomasia na za kikazi
(diplomatic and service passports).
Uwekaji saini huo
ulifanywa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dk. Augustine
Mahiga na Makamu wa Kwanza Wizara ya Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Korea, Bw. Lim
Sung-nam kwenye ukumbi wa Kikwete, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na
waandishi wa habari waliohudhuria hafla ya uwekaji saini, Waziri Mkuu amesema
kwenye mazungumzo yao wamejadiliana mambo mengi ambayo yamelenga kukuza
uhusiano wa kidiplomasia baina ya nchi hizo mbili.
“Tumejadili namna ya
kuimarisha mahusiano yetu kidiplomasia; kuimarisha ushirikiano katika
sekta ya uchumi na maendeleo; ushirikiano katika elimu, sayansi na TEHAMA
ushirikiano katika sekta ya utamaduni na utalii,” amesema.
“Pia tumeongelea fursa
ya mradi mkubwa wa reli, ujenzi wa daraja la Salender, mradi wa hospitali ya
Mloganzila; mradi wa NIDA ambao tumepata mkopo wa masharti nafuu kwa ajili ya
kuendelea kutoa vitambulisho vya uraia; ujenzi wa daraja la Kigongo - Busisi
lenye urefu wa mita 3,200; ujenzi wa barabara ya Kazirambwa – Chaya yenye urefu
wa km. 42 na uimarishaji wa sekta ya afya kwa kujenga hospitali tano za rufaa
kwenye kanda zetu,” amesema.
Waziri Mkuu amesema
amewaalika makampuni ya kutoka Jamhuri ya Korea yaje kuwekeza nchini ili
kuiwezesha Tanzania kufikia azma yake ya kuwa nchi ya uchumi wa viwanda ifikapo
mwaka 2025. “Pia wafanyabiashara aliokuja nao, kesho watashiriki kongamano la
kibiashara baina ya Korea na Tanzania ili waweze kubadilishana uzoefu na wenzao
wa Tanzania.”
“Tumewaomba pia
watangaze vivutio vya utalii vya hapa nchini huko kwao na Balozi wetu wa
Tanzania huko Korea atasimamia utangazaji wa vivutio vya hapa nchini kwetu.
Sisi pia tumewapongeza kwa uamuzi wa Korea Kusini kukaa pamoja na Korea
Kaskazini na kuimarisha amani kwa nchi zao,” amesema.
Mkutano huo pia
ulihudhuriwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Isack Kamwele;
Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani; Waziri wa Viwanda na Biashara wa
Zanzibar, Balozi Amina Salum Ally; Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais wa Zanzibar,
Bw. Issa Gavu na Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Eng. Stella
Manyanya. Wengine ni Makatibu Wakuu wa wizara mbalimbali na wakuu wa
taasisi.
Waziri Mkuu Lee
Nak-yon anatembelea Tanzania ikiwa ni hatua ya kuimarisha uhusiano wa
kidiplomasia baina ya nchi hizi mbili. Hii ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa
ngazi ya juu wa nchi hiyo kufanya ziara ya kiserikali tangu nchi hizo zianzishe
mahusiano ya kidiplomasia mwaka 1992.
Jamhuri ya Korea ni
mshirika mkubwa wa maendeleo wa Tanzania ambapo kupitia Shirika la
Kimataifa la Maendeleo (KOICA) na Mfuko wa Ushirikiano wa Uchumi na Maendeleo
(EDCF) yamekuwa yakitoa misaada na mikopo ya masharti nafuu ikiwemo misaada ya
fedha katika bajeti, ujenzi wa miundombinu ya jamii, mafunzo ya muda mfupi na
mrefu, wataalamu wa kujitolea, vifaa na mashine kwa ajili ya sekta mbalimbali
ikiwemo ya afya.
Baadhi ya miradi
ambayo imegharamiwa na Serikali ya Korea ni pamoja na Mradi wa kuboresha Huduma
ya Mama na Mtoto katika Hospitali ya Chanika, Mradi wa Mfumo wa Usajili wa Meli
na Mabaharia kwa Njia ya Mtandao Zanzibar, Mradi wa Ujenzi wa Hospitali ya Taifa
ya Taaluma na Tiba (MUHAS) kampasi ya Mloganzila na ujenzi wa daraja katika mto
Malagarasi.
Vile vile, Korea ni
mshirika mkubwa katika kusaidia maendeleo ya Bara la Afrika ambapo hivi
karibuni katika mkutano wa Sita wa Jukwaa la Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya
Korea na Afrika (KOAFEC VI) uliofanyika Mei 2018, Busan, Korea ambapo Serikali
ya Korea ilitangaza msaada wa dola za Marekani bilioni 5 kwa ajili ya Bara la
Afrika kwa kipindi cha 2018-2020. Tanzania ni miongoni mwa nchi zitakazonufaika
na msaada huo.
No comments:
Post a Comment