Mbunifu wa Mfumo wa kiteknolojia unaotumia akili bandia (AI) unaojulikana kama “MRI Kiganjani”, uliobuniwa na Dk. Jamal Banzi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), akizungumza na wanafunzi waliotembelea Banda la SUA wakati wa Maonesho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ubunifu na Ujuzi yaliyofanyika katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara jijini Tanga, Agosti 2026.
MFUMO wa kiteknolojia unaotumia akili bandia (AI) unaojulikana kama “MRI Kiganjani”, uliobuniwa na Dk. Jamal Banzi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), unatajwa kuwa na uwezo wa kusaidia kutambua viashiria vya magonjwa ya ubongo miaka 10 hadi 15 kabla dalili za ugonjwa hazijajitokeza.
Ubunifu huo unalenga kuwezesha madaktari kuchukua hatua za kinga na kuanza matibabu mapema, hivyo kupunguza madhara makubwa yanayoweza kusababishwa na magonjwa ya ubongo, ikiwemo kiharusi (stroke) na ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu (dementia).
Akizungumza katika mahojiano maalumu wakati wa Maonesho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ubunifu na Ujuzi yaliyofanyika katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara jijini Tanga, Agosti 2026,
Dk. Banzi alisema mfumo huo umetengenezwa kwa kutumia teknolojia ya akili bandia kuchakata vipimo vya kawaida vya afya na kuzalisha picha za ubongo zinazofanana kwa kiwango kikubwa na picha zinazopatikana kupitia mashine ya MRI.
“Mfumo huu wa MRI una uwezo wa kubaini mtu mwenye changamoto ya ubongo kuanzia miaka 10 hadi 15 kabla ya kuanza kuona dalili za ugonjwa. Hivyo, akianza mapema matibabu anaweza kuongeza umri wake,” alisema Dk. Banzi.
Alisema teknolojia hiyo huchambua kwa kina viashiria vidogo vya mabadiliko katika afya ya ubongo ambavyo vinaweza kuwa vigumu kubainika mapema kupitia uchunguzi wa kawaida.
Kwa mujibu wa Dk. Banzi, mfumo huo pia unaweza kutoa tahadhari ya awali kuhusu uwezekano wa mtu kupata kiharusi au dementia, hatua ambayo inaweza kuwapa wataalamu wa afya nafasi ya kuanza tiba kinga kabla uharibifu mkubwa wa ubongo haujatokea.
“Lengo kuu la mfumo huu ni kuwasaidia madaktari kufanya uamuzi wa haraka na kuchukua hatua za kinga kabla ubongo haujapata uharibifu mkubwa,” alisema.
Mbunifu wa mfumo huo Dk. Jamali Banzi akiwa katika kazi ya utafiti huo akijadiliana jambo na watafiti wenzake (hawapo pichani)
..................................
KIHARUSI CHANGAMOTO KUBWA
Dk. Banzi alisema Tanzania inakabiliwa na changamoto kubwa ya magonjwa yanayosababisha uharibifu wa ubongo na mfumo wa neva, huku tatizo hilo likiongezeka kutokana na kuongezeka kwa umri wa kuishi pamoja na mabadiliko ya mfumo wa maisha.
Alisema kiharusi ni miongoni mwa sababu kuu za uharibifu wa ghafla wa seli za ubongo nchini.
Kwa mujibu wa takwimu alizotaja, kiharusi kinachangia takribani asilimia 26.3 ya wagonjwa wanaolazwa katika wodi za magonjwa ya ndani katika baadhi ya hospitali nchini.
Alisema tafiti pia zimeonyesha kuwa maeneo ya mijini yanaweza kuwa na mzigo mkubwa zaidi wa kiharusi kutokana na kuongezeka kwa shinikizo la damu na mitindo ya maisha isiyofaa.
Dk. Banzi alitaja pia dementia kuwa miongoni mwa changamoto kubwa zinazohusisha uharibifu wa taratibu wa seli za ubongo na kuathiri uwezo wa mtu kukumbuka, kufikiri na kufanya maamuzi.
Alisema inakadiriwa kuwa Tanzania ina takribani watu 250,000 wanaoishi na changamoto ya kupoteza kumbukumbu.
Hata hivyo, alisema changamoto kubwa ni uelewa mdogo kuhusu dementia katika jamii, hali inayosababisha baadhi ya wazee wenye ugonjwa huo kutengwa, kunyanyapaliwa au hata kuhusishwa kimakosa na imani za kishirikina kutokana na mabadiliko ya tabia yanayosababishwa na ugonjwa huo.
KIFAFA AJALI NA MAGONJWA MENGINE
Dk. Banzi alisema kifafa pia kinahusishwa na kuvurugika kwa shughuli za umeme katika ubongo, huku maeneo ya vijijini yakiwa miongoni mwa maeneo yenye mzigo mkubwa wa ugonjwa huo.
Alisema changamoto nyingine ni wagonjwa kuchelewa kupata matibabu ya kitaalamu kutokana na baadhi yao kuanza kutafuta huduma kwa waganga wa jadi au viongozi wa kiroho wakiamini kuwa ugonjwa huo unasababishwa na nguvu za giza.
“Visababishi vingine vya uharibifu wa ubongo ni ajali za pikipiki (bodaboda) na magari ambazo zinasababisha majeraha makubwa ya kichwa na ubongo na kuwaacha maelfu ya vijana na ulemavu wa kudumu wa akili au viungo kila mwaka,” alisema.
Aliongeza kuwa malaria kali ya ubongo kwa watoto, uti wa mgongo (meningitis) pamoja na athari zinazohusishwa na VVU ni miongoni mwa visababishi vingine vya uharibifu wa tishu za ubongo.
Dk. Banzi akizungumza na wananchi waliotembelea Banda la SUA.
...............................................
UPUNGUFU WA WATAALAMU NA VIFAA
Akizungumzia changamoto za huduma za kitabibu, Dk. Banzi alisema Tanzania bado inakabiliwa na uhaba wa madaktari bingwa wa upasuaji wa ubongo (neurosurgeons) na wataalamu wa mfumo wa neva (neurologists).
Alisema pia kuna upungufu wa vifaa vya kisasa, ikiwemo mashine za MRI na CT-Scan katika baadhi ya hospitali za mikoa na wilaya.
Kwa sababu hiyo, alisema ubunifu wa teknolojia kama “MRI Kiganjani” unaweza kuwa na umuhimu mkubwa endapo utathibitishwa kisayansi na kuidhinishwa na mamlaka husika.
MATUMAINI MAKUBWA KWA WATAALAMU
Utafiti huo umepokelewa kwa matumaini na baadhi ya wataalamu wa afya kutokana na uwezekano wa kupunguza gharama na muda wa kupata huduma za uchunguzi.
Kwa sasa, hospitali nyingi za wilaya, hasa maeneo ya vijijini, hazina mashine za MRI kutokana na gharama kubwa za ununuzi, uendeshaji na matengenezo.
Kwa mujibu wa maelezo ya utafiti huo, teknolojia ya “MRI Kiganjani” inalenga kutumia vipimo vya kawaida vya afya na akili bandia kuzalisha picha za ubongo zinazofanana kwa kiwango kikubwa na picha za MRI halisi.
Uwezo huo, endapo utathibitishwa kikamilifu, unaweza kusaidia kusogeza huduma za uchunguzi wa magonjwa ya ubongo karibu na wananchi ambao kwa sasa hulazimika kusafiri hadi miji mikubwa kupata huduma hizo.
Aidha, teknolojia hiyo inaweza kusaidia kupunguza mzigo kwa madaktari bingwa wa mionzi (radiologists) wanaohudumia idadi kubwa ya wagonjwa katika hospitali za rufaa.
TAHADHARI KABLA YA KUTUMIKA HOSPITALINI
Pamoja na matumaini hayo, wataalamu wa afya wanasisitiza kuwa teknolojia hiyo haiwezi kuchukua nafasi ya mashine halisi za MRI au uamuzi wa daktari kabla ya kufanyiwa majaribio na uthibitisho wa kina wa kitabibu.
Muonekaano wa baadhi ya vifaa vya kielektoniki vinavyo tumika katika utafiti huo.
........................................................
Hii ni kwa sababu hata tofauti ndogo katika usahihi wa mfumo wa AI inaweza kuwa na madhara makubwa iwapo itasababisha mgonjwa kupewa utambuzi usio sahihi.
Kwa hiyo, mfumo huo unahitaji kufanyiwa majaribio ya kliniki, tathmini ya usalama na ufanisi, pamoja na kupata vibali kutoka mamlaka husika kabla ya kuanza kutumika rasmi katika hospitali.
Miongoni mwa hatua zinazohitajika ni kuwafanyia majaribio wagonjwa halisi, kuchambua matokeo, kuthibitisha usahihi wa mfumo na kuwapa wataalamu wa afya mafunzo ya namna ya kutumia na kutafsiri majibu yanayotolewa na AI.
JINSI “MRI KIGANJANI” INAVYOLENGA KUFANYA KAZI
Kwa mujibu wa maelezo ya mtafiti, akili bandia hufundishwa kwa kutumia maelfu ya picha za ubongo ili kutambua tofauti kati ya ubongo wenye afya na ule unaoonyesha viashiria vya ugonjwa.
Baada ya kupokea vipimo vya mgonjwa, mfumo huchakata taarifa hizo na kuzalisha picha za pande tatu (3D) zinazolenga kufanana na picha zinazopatikana kupitia MRI.
AI kisha huchambua mabadiliko madogo katika ubongo na kutoa tahadhari iwapo kuna viashiria vinavyoweza kuhusishwa na magonjwa fulani.
Mfumo huo unatajwa kuwa na uwezo wa kutoa majibu ndani ya muda mfupi, jambo ambalo linaweza kupunguza muda wa kusubiri majibu ya vipimo.
HOSPITALI ZINAZOWEZA KUNUFAIKA
Iwapo teknolojia hiyo itathibitishwa na kuidhinishwa, hospitali kubwa za rufaa na taasisi zenye miundombinu imara ya kidijitali zinaweza kuwa miongoni mwa maeneo ya awali ya matumizi.
Miongoni mwa taasisi hizo ni Hospitali ya Taifa Muhimbili, Hospitali ya Benjamin Mkapa, Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, KCMC, Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya pamoja na baadhi ya hospitali binafsi zenye mifumo ya kisasa ya kuhifadhi na kuchakata taarifa na picha za kitabibu.
Hata hivyo, lengo kubwa la teknolojia hiyo ni kufikisha huduma za uchunguzi kwa maeneo ambayo hayana mashine kubwa na ghali za MRI.
Kwa mfano, hospitali ya wilaya inaweza kuhitaji kompyuta au kishikwambi chenye programu husika, badala ya kuwekeza moja kwa moja katika ununuzi wa mashine kubwa ya MRI, iwapo mfumo huo utathibitishwa kuwa salama na sahihi kwa matumizi hayo.
GHARAMA ZA HUDUMA
Miongoni mwa matarajio yanayohusishwa na ubunifu huo ni kupunguza gharama za uchunguzi wa magonjwa ya ubongo.
Kwa sasa, gharama za vipimo vya MRI zinaweza kuwa kubwa kwa wananchi wengi, huku upatikanaji wa huduma hiyo ukiwa mkubwa zaidi katika hospitali chache zenye miundombinu husika.
Iwapo “MRI Kiganjani” itathibitishwa na kuidhinishwa, gharama za uchunguzi zinaweza kuwa chini ikilinganishwa na MRI halisi, jambo ambalo linaweza kuongeza uwezo wa wananchi kupata huduma za utambuzi wa mapema.
Hata hivyo, gharama halisi za huduma hiyo, pamoja na iwapo italipiwa na mifuko ya bima ya afya, zitategemea uthibitisho wa teknolojia, usajili wake, sera za afya na taratibu za mamlaka husika.
HATUA ZA KISHERIA
Kabla ya teknolojia hiyo kutumika kwa wagonjwa kwa kiwango kikubwa, inapaswa kupitia taratibu za udhibiti na uthibitishaji wa vifaa tiba na teknolojia za afya.
Miongoni mwa mamlaka muhimu ni Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA) pamoja na Wizara ya Afya.
Aidha, majaribio ya kliniki na tathmini ya kisayansi ni muhimu ili kubaini ufanisi, usalama na mipaka ya matumizi ya mfumo huo.
Ni hatua hii itakayosaidia kuhakikisha kuwa AI inatumika kama nyenzo ya kumsaidia daktari, badala ya kuchukua nafasi ya mtaalamu katika kufanya uamuzi wa mwisho wa matibabu.
Wadau wakipata maelezo walipotembelea Banda laa SUA.
..................................................................
WADAU WAPONGEZA UBUNIFU
Dk. Micky Ulaya wa Pride Polyclinic mjini Singida amepongeza utafiti huo akisema unaweza kusaidia kupunguza foleni za wagonjwa wanaosubiri vipimo.
“Kama Taifa tunaona tunapiga hatua za maendeleo kupitia tafiti zenye tija. Serikali imekwisha kufanya jitihada za kuwawezesha watafiti. Tunachosubiri ni kuona utafiti huo unathibitishwa kisheria na mamlaka husika kwa matumizi,” alisema.
Kwa upande wake, Upendo Haule Nyisega, mkazi wa Kibaha Picha ya Ndege mkoani Pwani, alisema magonjwa ya ubongo yamekuwa yakiongezeka kutokana na changamoto mbalimbali za maisha.
“Jambo lolote ukilibaini mapema unaweza kupata suluhisho lake kabla ya kufikia hatua mbaya. Hivyo tuna kila sababu ya kupongeza ubunifu huu ambao unaweza kutambua mtu mwenye changamoto ya ubongo hata miaka 10 kabla ya dalili za wazi kuonekana,” alisema Haule.
Gabriel Mponjoli, mkazi wa Ushirika Tukuyu mkoani Mbeya, alisema familia yao iliwahi kukutana na changamoto ya ugonjwa wa ubongo baada ya baba yao kuanza kuonyesha dalili za kupoteza kumbukumbu na kubadilika kwa tabia.
“Baba yetu alikuwa akisahau-sahau. Alifikia mahali hata simu yake akiiweka sehemu alikuwa hakumbuki na alikuwa mkali bila sababu yoyote.
Baada ya kupita miaka mitatu ndipo ilipogundulika kuwa ana changamoto ya ubongo,” alisema.
Mponjoli alisema iwapo utafiti wa Dk. Banzi utathibitishwa na kuanza kutumika kwa mujibu wa taratibu za kitabibu, unaweza kuwa msaada mkubwa kwa familia zinazokabiliwa na changamoto za magonjwa ya ubongo.
Kwa ujumla, ubunifu wa “MRI Kiganjani” unaweka mbele dhana ya kutambua na kuzuia ugonjwa kabla haujaleta madhara makubwa.
Hata hivyo, pamoja na matumaini makubwa yanayoambatana na teknolojia hiyo, wataalamu wanasisitiza umuhimu wa uthibitisho wa kina wa kisayansi, majaribio ya kliniki na uidhinishaji wa mamlaka husika.
Endapo hatua hizo zitakamilika kwa mafanikio, teknolojia hiyo inaweza kuwa miongoni mwa bunifu zinazosaidia Tanzania kusogeza huduma za uchunguzi wa magonjwa ya ubongo karibu na wananchi, hasa wale wanaoishi maeneo ambayo hayana vifaa vya kisasa vya uchunguzi
Muonekano wa vifaa vya utafiti huo.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Dk. Amos Nungu, akizungumzia Tafiti hizo alisema COSTECH kupitia Serikaali imekuwa ikifadhili masuala mbalimbali ya Sayansi na Teknolojia kwa kutoa fedha kufanikisha miradi ya bunifu kwa ajili ya maendeleo ya kijamii na uchumi.
...........................
Makala hii imeandaliwa na Dotto Mwaibale simu namba o754362990,









No comments:
Post a Comment