TANZANIA YAWA MWENYEJI WA MKUTANO WA MAFUNZO YA MIFUMO YA UANGAZI WA HALI YA HEWA DUNIANI KWA NCHI ZA KANDA YA AFRIKA MASHARIKI NA KASKAZINI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 7 October 2024

TANZANIA YAWA MWENYEJI WA MKUTANO WA MAFUNZO YA MIFUMO YA UANGAZI WA HALI YA HEWA DUNIANI KWA NCHI ZA KANDA YA AFRIKA MASHARIKI NA KASKAZINI





TANZANIA kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa kushirikiana na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) imekuwa Mwenyeji wa mkutano wa Mafunzo ya WMO kwa wataalamu wa hali ya hewa kutoka nchi Wanachama wa WMO Kanda ya Afrika Mashariki na Kaskazini. Lengo likiwa ni kuwajengea uwezo wataalamu wa Hali ya Hewa wanaofanya kazi katika vituo hivyo vya “WMO Regional WIGOS Centres (RWCs)”  vya kanda ya Afrika Mashariki na Kaskazini Afrika.

Akifungua rasmi mafunzo hayo yanayofanyika katika Hoteli ya Four Points by Sheratons, kuanzia tarehe 7-11 Oktoba, 2024,  Mgeni rasmi na Mwenyekiti wa Bodi ya TMA, Mhe. Jaji Mshibe Ally Bakari alisema suala muhimu kwa Taasisi za Hali ya Hewa za Afrika ni kuimarisha upatikanaji wa taarifa za hali ya hewa zenye ubora kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi, hivyo mafunzo hayo yatasaidia kuboresha zaidi shughuli zinazofanywa, ikiwa ni pamoja na kuboresha mtandao wa kubadilishana data ili kuboresha zaidi utabiri wa matukio ya hali mbaya ya hewa katika nchi wanachama wa WMO.

Aidha, Jaji Mshibe aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuwekeza katika uboreshaji wa miundo mbinu ya huduma za hali ya hewa. Jaji Mshibe aliwashukuru pia WMO na washirika wengine kwa jitihada zao za kuimarisha huduma za hali ya hewa barani Afrika, ikiwemo kuanzisha mfuko wa uwezeshaji wa huduma za uangazi wa hali ya hewa ambapo kupitia jitihada hizo, kiasi cha dola za kimarekani milioni 9 zimeidhinishwa kuboresha huduma za hali ya hewa nchini Tanzania.

Awali, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Mwakilishi wa kudumu wa WMO, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi, Dkt. Ladislaus Chang’a, alieleza umuhimu wa kuimairsha uangazi na kuongeza upataikanaji wa data kwa ajili ya kuimairsha utoaji wa tahadhari za matukio ya hali mbaya ya hewa na kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa. 

Aidha Dkt. Chang’a alieleza kuwa Tanzania kupitia TMA imejipanga kuendelea kushiriki katika kuongoza na kuwa kinara katika baadhi ya jitihada za kuimarisha huduma za hali ya hewa Barani Afrika. “ Tumejiandaa vyema kuwa mwenyeji wa Mkutano huu mkubwa wa Kikanda, na pia kama mwenyeji wa Kituo cha mfumo wa Kidunia wa  kufuatilia vituo vya uangazi wa hali ya hewa kwa nchi za Afrika Mashariki” alisema Dkt. Chang’a. TMA itawasilisha mada zenye kueleza uzoefu wake katika utekelezaji wa jukumu hilo.

Kwa upande wake, Mwakilikishi kutoka WMO alisema kumekuwa na changamoto ya matukio mbalimbali ya Hali mbaya ya Hewa hivyo ushirikiano wetu utasaidia katka kutoa tahadhari za mapema juu ya matukio ya Hali mbaya ya Hewa na tahadhali za mapema”.Alisema, Abubakari Salih Babiker

Washiriki wa mkutano huo wametoka Taasisi za Hali ya Hewa za nchi za Tanzania, Tunisia, Algeria, Egypt, Sudan, South Sudan, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Somalia, Ethiopia, Djibouti, Madagascar, Comoros, Sychelles, Mauritius, Morocco, Afrika Kusini na waalikwa kutoka Oman na Sekretarieti ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani.

No comments:

Post a Comment