HAKUNA KASORO TULIYOIBAINI KATIKA UJENZI HUU - MHE. NDEJEMBI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 7 October 2024

HAKUNA KASORO TULIYOIBAINI KATIKA UJENZI HUU - MHE. NDEJEMBI

 



Na Mwandishi Wetu, Msalala

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Deogratius Ndejembi amesema baada ya kutembelea shule ya sekondari Ntobo hakuna kasoro waliyoibaini katika ujenzi huu wa Shule hiyo iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Msalala, huku akipongeza zaidi kwa kubakia na salio la zaidi ya Milioni 10.

Mhe. Ndejembi amesema haya leo Oktoba 6, 2024 alipofika shuleni hapo kutembelea na kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Msalala ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku mbili mkoani Shinyanga.

"Nawapongeza sana Halmashauri ya Wilaya ya Msalala kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa shule hii ya Ntobo, tumetembelea, tumekagua lakini mpaka sasa hakuna kasoro tuliyoiona katika utekelezaji wa mradi huu zaidi ya yote shule inao ubora unaoendana na thamani ya pesa na kwamba mmebakiwa na pesa zaidi ya Mil. 10 huu ni mfano wa kuigwa," amesema Mhe. Ndejembi.

Akisoma taarifa mbele ya mgeni rasmi, Mkuu wa Shule ya Ntobo Sekondari Mwl. Hussein Mbwambo amesema kuwa wanayo furaha kumtaarifu Waziri kuwa ujenzi wa vyumba vya madarasa 7, matundu 8 ya vyoo, ofisi 1 ya walimu umekamilika vizuri na kubakiwa na salio la zaidi ya Sh. Milioni 10 ambapo wamemuomba Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala awaruhusu zitumike kukarabati jengo la utawala.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Macha amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuipatia fedha za miradi ya maendeleo katika Wilaya hiyo ambapo katika Sekta ya Elimu zimeboresha miundombinu yote muhimu ya watu wenye ulemavu, ya kufundishia walimu na kusomea wanafunzi jambo ambalo limekuja kuondoa tofauti ya Shule za binafsi na hizi za Serikali kwani kwa sasa shule zinavutia zaidi kuliko za binafsi.

Ujenzi wa Shule ya Sekondari Ntobo ulianza rasmi mwaka 2006, ni shule ya kutwa ambayo ni mchanganyiko ambayo kwa sasa ina Kidato cha kwanza hadi cha nne na jumla ya wanafunzi 577 sanjari na bweni la watoto wa kike lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 48.


Katika ziara hiyo, Mhe Dejembi ameongozana na mwenyeji wake Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha, Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mhe. Mboni Mhita, Mbunge wa Jimbo la Msalala Mhe. Iddy Kassim Iddy.

No comments:

Post a Comment