Na Mwandishi Wetu, Ukonga
MBUNGE wa Ukonga ambaye pia ni Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Jerry Silaa amegawa majiko ya gesi ya kupikia kwa mama lishe jimboni kwake, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhamasisha jamii kutumia nishati safi ya kupikia.
Mhe. Silaa alikuwa katika ziara jimboni humo ambapo amesema matumizi ya gesi ni salama na yanaokoa fedha nyingi pamoja na kutunza mazingira, ziara hii ikiwa ni muendelezo wa ziara yake jimboni humo aliyoianza Septemba 09, 2024.
Akiwa katika soko dogo la Pugu Mhe. Silaa alizungumza na Wafanyabiashara ya chakula ambapo aliwataka kutathmini matumizi ya mkaa na gesi.
"Ndugu zangu tumieni majiko haya ya gesi na mfanye tathmini ninyi wenyewe ni nishati ipi inayotumia gharama kubwa," amesema Mhe. Silaa.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi waliopokea majiko hayo wamesema mbali na gharama kubwa za nishati za kuni na mkaa kuna madhara makubwa ya kiafya wanayoyapata.
"Mimi natumia mkaa wa shilingi elf 7 hadi 8 kwa siku, ni gharama kubwa ambayo nikiuza chakula napata faida kidogo na wakati mwingine sipati kabisa, pia naumia na moshi wa kuni na mkaa ninaopikia" amesema Bi. Riziki Ramadhan Mkazi wa Pugu Kona.
Naye Bi. Khadija Kawegela Mkazi wa Pugu Kajiungeni amesema matumizi ya nishati ya gesi, yatamsaidia kupika chakula kwa wakati na kuepukana kutumia muda mwingi kutafuta nishati mbadala ambazo hazina mazingira rafiki kwa afya.
"Mheshimiwa
Mbunge, Mimi nimezaliwa mwaka 1949, na uzee huu hili jiko litanisaidia sana,
nilikuwa natumia muda mwingi kutafuta kuni na mkaa, maisha yangu ni magumu
sana, hajika mmenirahisishia maisha, nakushukuru wewe binafsi na Rais Samia kwa
kutuletea maendeleo haya," amesema Khadija Kawegela.
No comments:
Post a Comment