SERIKALI KUTOA RUZUKU YA TANI 52,000 ZA MBEGU BORA MSIMU WA KILIMO WA 2024/25 - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday, 20 December 2024

SERIKALI KUTOA RUZUKU YA TANI 52,000 ZA MBEGU BORA MSIMU WA KILIMO WA 2024/25

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji wa Serikali, Geryson Msigwa akizungumza na waandishi wa habari wakati akitoa taarifa kuhusu masuala mbalimbali yaliyotekelezwa na Serikali katika mkutano uliofanyika Desemba 19, 2024 jijini Dar es Salaam.

Na Dotto Mwaibale, Dar

SERIKALI imepanga kutoa ruzuku ya tani 52,000 za mbegu bora za mahindi kwa wakulima katika msimu wa 2024/2025.

Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji wa Serikali, Geryson Msigwa wakati akitoa taarifa kuhusu masuala mbalimbali yaliyotekelezwa na Serikali katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Desemba 19, 2024 jijini Dar es Salaam.

“Hadi kufikia Novemba 30, 2024 jumla ya tani 4,000 za mbegu bora za mahindi zenye thamani ya Sh. 3,496,721,000 ya ruzuku zimenunuliwa na wakulima 79,335,” alisema Msigwa.

Akizungumzia upatikanaji wa mbegu bora alisema makadirio ya mahitaji ya mbegu hizo nchini kwa msimu wa 2024/2025 ni tani 80,000 ambapo upatikanaji umefikia tani 42,471.09 sawa na asilimia 53 ya makadirio ya mahitaji. Alisema kati ya tani hizo, tani 29,819.57 zimezalishwa ndani ya nchi na tani 12,651.52 zimeingizwa kutoka nje ya nchi.

Msigwa alisema uzalishaji wa ndani wa mbegu zilizothibitishwa ubora za mazao mbalimbali umeongezeka kutoka tani 42,096.68 msimu wa 2022/2023 hadi kufikia tani 56,114 msimu wa 2023/2024.

Alisema hali hiyo inaonesha kuimarika kwa uzalishaji wa ndani wa mbegu ikiwa ni hatua mahsusi ya kuchangia utoshelevu wa pembejeo za kilimo ndani ya nchi kwa kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji na kushirikisha sekta binafsi katika uzalishaji wa mbegu kwa kutumia mashamba ya Serikali yanayomilikiwa na Wakala wa Mbegu za Kilimo (Agricultural Seed Agency – ASA).

Akizungumzia makadirio ya mahitaji ya mbolea na visaidizi vyake kwa msimu wa 2024/25 ni tani 1,000,000 ambapo hali ya upatikanaji wa mbolea  nchini kufikia tarehe 30 Novemba, 2024 ulikuwa ni tani 769,060 sawa na asilimia 77 ya mahitaji.

Alisema kiasi hicho cha upatikanaji kilitokana na bakaa ya msimu uliopita tani 260,403, uzalishaji wa ndani tani 58,669 na zilizoingizwa kutoka nje ya nchi tani 449,988.

“Uzalishaji wa ndani wa mbolea umeendelea kuimarika kutokana na jitihada zinazofanywa na Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi kwa kutumia malighafi za ndani ikiwemo rock phosphate ambapo uzalishaji wa ndani wa mbolea umeongezeka kutoka tani 84,696 mwaka 2022/2023 hadi tani 158,628 msimu wa 2023/2024,” alisema Msigwa.

Akielezea utekelezaji wa utoaji wa ruzuku ya mbolea na mbegu bora katika msimu wa 2024/2025 alisema Serikali inatekeleza mpango wa utoaji wa Ruzuku ya Mbolea na mbegu bora za mahindi kwa wakulima.

Alisema lengo la utoaji wa ruzuku hiyo ni kupunguza gharama ya mbolea kwa mkulima ili kuongeza uzalishaji na tija katika kilimo, kuimarisha usalama wa chakula na kuongeza upatikanaji wa malighafi za viwanda.

Msigwa akizungumzia mfumo wa utoaji wa ruzuku ya mbegu za mahindi na mbolea alisema utaratibu wa utoaji wa ruzuku unatumia mfumo wa kidigitali wa Digital Subsidy System ambao unaratibiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (Tanzania Fertilizer Regulatory Authority –TFRA) na Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (Tanzania Official Seed Certification Institute – TOSCI).

Alisema utoaji wa ruzuku unazingatia mahitaji halisi ya mkulima kulingana na taarifa za usajili na bajeti ya Serikali iliyotengwa.

Aidha, Msigwa akizungumzia usajili wa wakulima na wafanyabiashara wa pembejeo alisema ili kutekeleza mpango wa mbolea na mbegu za ruzuku kupitia mfumo huo wa kidigitali, wakulima wanapaswa kujisajili katika daftari la usajili wa wakulima kwenye ngazi ya Kijiji/ Kata.

Alisema baada ya kujisajili kwenye daftari, maafisa kilimo wanaingiza taarifa za wakulima hao kwenye mfumo wa kidigitali wa utoaji wa ruzuku ya pembejeo.

Alisema wakulima kupitia simu zao hupokea ujumbe mfupi unaowafahamisha namba ya siri ambayo wataitumia kununua mbegu za mahindi na mbolea ya ruzuku kwa kipindi cha msimu wa kilimo kulingana na ukubwa wa shamba na aina ya zao aliloainisha wakati wa usajili.

Msigwa alisema mkulima haruhusiwi kutumia namba ya simu ya mtu mwingine wakati wa usajili au kununulia mbegu na mbolea.

Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo alisema wazalishaji, waagizaji, wasambazaji binafsi (mawakala) na Vyama vya Ushirika vinavyohusika kununua na kusambaza mbegu na mbolea husajiliwa na TOSCI na TFRA na kupewa namba maalumu ya usajili.

“Hadi kufikia Novemba 30, 2024, jumla ya wakulima 4,141,730 , kampuni 31 na wafanyabiashara/mawakala 2877 wa mbolea na mawakala 666 wa mbegu bora wenye jumla ya vituo vya mauzo (Active outlets) 7,000 wamesajiliwa kwenye mfumo, “ alisema Msigwa.

Alisema utoaji wa ruzuku ya mbolea na mbegu bora kwa wakulima msimu wa kilimo wa 2024/2025 umeanza katika baadhi ya mikoa inayopata mvua kuanzia mwezi Oktoba ikiwemo mikoa ya Mbeya, Kagera, Kigoma, Njombe, Dodoma, Singida, Morogoro, Tabora, Geita, Shinyanga, Mwanza, Mara, Simiyu, Manyara, Iringa, Rukwa, Katavi na Songwe ambapo ununuzi wa mbolea na mbegu bora unaendelea.

Alisema katika kipindi cha kuanzia tarehe 1 Julai, 2024 hadi kufikia tarehe 30  Novemba, 2024 jumla ya tani 253,669.342 za mbolea zenye thamani ya Shilingi 435,724,224,815 zimenunuliwa kwa utaratibu wa ruzuku na wakulima 406,966 ambapo ruzuku ya Serikali ni Sh. 90,485,490,128.

Msigwa aliongeza kuwa katika kuimarisha huduma za ugani, Serikali imenunua na kusambaza vishikwambi 5,285 kwa Maafisa Ugani, magari 15 kwa maafisa Kilimo ngazi ya mkoa, magari madogo 10 kwa maafisa Kilimo ngazi za wilaya na pikipiki 6,444 kwa maafisa wa Kata na Vijiji.

Alisema , Serikali imenunua na kusambaza vipima afya ya udongo 143 (soil scanner); visanduku vya ugani 1,000 (extension kit) na sare za maafisa ugani 6,456.

Aidha, Serikali inaendelea na ujenzi wa nyumba 50 za maafisa ugani pamoja na kununua pikipiki 300 ili kutosheleza mahitaji ya pikipiki kwa maafisa ugani waliopo.

Msigwa alitumia mkutano huo kutoa wito kuwa msimu wa kilimo umeanza katika maeneo mengi nchini, hivyo wakulima wote wahakikishe wana namba ya mkulima ambayo pamoja na kuwawezesha kununulia mbolea pia inatumika kunununulia mbegu bora za mahindi kwa mfumo wa ruzuku.

Kwa wakulima ambao hawajapata namba hiyo, wajitokeze kwenye ofisi za vijiji/mitaa kwa ajili ya kujiandikisha kwenye daftari la mkulima.

Aliwaomba Wataalam wa kilimo katika ngazi za Wilaya na Vijiji/mitaa kwa kutumia vishikwambi walivyopewa, waongeze kasi ya usajili wa wakulima kwenye mfumo ili kuwezesha wakulima kupata namba zitakazotumika kununualia mbolea na mbegu bora za ruzuku.

 Halmashauri zote Tanzania Bara zitoe kipaumbele katika uimarishaji na ugharamiaji wa huduma za ugani kwa kuhakikisha kwamba kila Afisa Ugani anatumia vitendea kazi alivyopewa na anatekeleza wajibu wake kwa kuwahudumia wakulima ipasavyo.

Msigwa alihitimisha mkutano huo kwa kueleza kwamba Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji wa mkutano mkubwa wa Wakuu wa Nchi za Afrika wa masuala ya Nishati utakaofanyika Januari 28, 2025.

Alisema hatua hiyo inatokana na mkakati wa Serikali ya Awamu ya sita ya kuimarisha upatikanaji wa nishati ya umeme nchini kwa kupeleka umeme vijijini na vitongojini kwa kasi hali ambayo imewavutia viongozi hao kuamua kufanyia mkutano huu mkubwa nchini kwetu.

Alisema sisi kama wanahabari tunalo jukumu la kushiriki na kuendelea kuwahabarisha Watanzania kuhusu mafanikio haya muhimu.

Alisema Serikali imeendelea kutekeleza miradi ya kusambaza umeme vijijini ambapo hadi sasa vijiji 12,278 kati ya vijiji 12,318 tayari vimeunganishwa kwa umeme. Vijiji 40 vilivyosalia vitakuwa vimeunganishwa na umeme ndani ya mwezi huu. 

No comments:

Post a Comment