NAIBU WAZIRI SANGU AWAFUNDA WANAJOPO WA KADA YA AFYA, ASISITIZA UADILIFU - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday 11 September 2024

NAIBU WAZIRI SANGU AWAFUNDA WANAJOPO WA KADA YA AFYA, ASISITIZA UADILIFU

Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus  Sangu  akizungumza na Kaimu Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Dkt. Cairo Mwaitete mara baada ya kuwasili  kwa ajili ya kuzungumza na kushuhudia wataalamu kutoka kwenye Taasisi mbalimbali za Serikali ambao wamechaguliwa kuwa  wanajopo wa kuendesha zoezi la usaili wa mahojiano ya ana kwa ana kwa  wasailiwa kada ya afya Jijini Arusha.

Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Mhandisi Samuel Tanguye akizunguma na Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus  Sangu  mara baada ya kuwasili  kwa ajili y kushuhudia uendeshaji wa  zoezi la usaili wa mahojiano ya ana kwa ana kwa  wasailiwa kada ya afya Jijini Arusha.

Na Lusungu Helela- Arusha

NAIBU Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu amewataka wanajopo la usaili kuhakikisha wanakuwa waadilifu na wanatenda haki huku akisititiza ajira ni suala la usalama wa nchi.

 

Ametoa kauli hiyo Jijini Arusha wakati akizungumza na wataalamu kutoka kwenye Taasisi mbalimbali za Serikali ambao wamechaguliwa kuwa wanajopo wa kuendesha zoezi la usaili wa mahojiano ya ana kwa ana kwa  wasailiwa kada ya afya unaendelea katika mikoa mbalimbali nchini.

 

Amesema Serikali imejipanga kuhakikisha  haki inatendeka kwa kila msailiwa ili atakayeshinda ashinde kwa haki na atakayeshindwa ashindwe kwa haki.

 

Mhe. Sangu ametumia fursa hiyo kutoa rai kwa wanajopo hao kutanguliza mbele maslahi ya taifa huku akionya yeyote atakayethubutu kuvuruga zoezi hilo atakuwa ameingia kwenye matatizo makubwa

 

‘’ Tunatafuta vijana watakaoingia Serikalini katika Utumishi wa Umma si chini ya miaka 25 na wengine wenye umri mdogo mpaka miaka 30 kwa hiyo tukifanya makosa tukapeleka vijana wasio na sifa, uadilifu na mengineyo tutalighalimu taifa kwa zaidi ya miaka 25.

 

Kufuatia hatua hiyo Mhe. Sangu amewataka wasaili hao kujiepusha na tabia ya kupendelea na pale inapotea jambo la kujadiliana lijikite katika  kutenda haki.

 

"Tunataka haki itendeke na ionekana imetendeka kwa wasailiwa wote " amesisitiza Mhe. Sangu.

 

Amesema kwa mujibu wa sera ya ajira toleo la pili la mwaka 2008 inaelekeza kuwa ajira zote zipatikane kwa ushindani.

 

‘’Maombi yamekuwa mengi sana kati ya nafasi 12,000 zilizotangazwa za kada ya afya zaidi ya vijana 47,000 wameomba huku kwenye walimu jumla ya vijana waliomba ni 200,000 kati nafasi za ajira za ualimu 11,015 zilizotangazwa hivyo hakuna njia nyingine ya kupata watumishi pasipo kushindanisha,’’

 

Amesema kwa sasa vijana wengi wamemaliza vyuo na wapo mtaani ila kutokana na bajeti ya serikali na hali ya uchumi haiwezi kuwa na bajeti ya kuajiri vijana wote waliomaliza vyuo.

 

Hata hivyo amesema Serikali imekuwa ikifanya jitihada kubwa chini ya Uongozi wa Samia Suluhu Hassan ambapo katika kipindi chake cha miaka mitatu ametoa vibali vya ajira zaidi ya 100,000 ambayo ni idadi kubwa sana katika kipindi cha miaka mitatu ukifananisha na miaka mitano iliyopita.

 

Naye Kaimu Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Mhandisi Samuel Tanguye amesema zoezi hili limeshirikisha watalaamu mbalimbali lengo ni kuhakikisha vijana watakaopatika katika machakato huo ni wenye weledi wataokwenda kulisaidia taifa.

No comments:

Post a Comment