RAIS MSTAAFU DKT JAKAYA MRISHO KIKWETE AONGOZA HARAMBEE KUCHANGIA GHARAMA ZA MATIBABU KWA WATOTO KUTOKA FAMILIA ZISIZO NA UWEZO WENYE UGONJWA WA MOYO - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Sunday, 3 November 2024

RAIS MSTAAFU DKT JAKAYA MRISHO KIKWETE AONGOZA HARAMBEE KUCHANGIA GHARAMA ZA MATIBABU KWA WATOTO KUTOKA FAMILIA ZISIZO NA UWEZO WENYE UGONJWA WA MOYO

 





Na Issa Michuzi


RAIS Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, ametoa wito kwa taasisi na watu binafsi wenye nia njema kujitokeza na kuchangia matibabu ya watoto wenye matatizo ya moyo kutoka familia zisizo na uwezo ili kuwaondolea au kupunguza mateso yanayosababishwa na maradhi hayo.


Dkt. Kikwete alitoa wito huo Jumamosi usiku wakati wa harambee aliyoongoza kuchangia gharama za matibabu ya watoto hao, iliyoandaliwa na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Heart Team Africa Foundation (HTAF) katika hoteli ya Joihari Rotana, jijini Dar es Salaam.


Rais Mstaafu, ambaye ni mlezi wa watoto wanaohitaji matibabu ya moyo, alieleza kuwa lengo kuu la harambee hiyo ni kuchangisha asilimia 30 ya gharama zilizobaki za matibabu, kwani asilimia 70 ya gharama hizo huchangiwa kila mwaka na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.


"Naishukuru serikali kwa kuchangia asilimia 70 ya gharama zote za matibabu ya wagonjwa hao. Hata hivyo, asilimia 30 iliyobaki, ambayo familia ya mgonjwa inapaswa kuchangia, bado ni mzigo mzito kwa familia nyingi. Wanahitaji kusaidiwa," alisema.


Alieleza kuwa kuna watoto 1,500 kutoka familia zisizo na uwezo ambao wamesajiliwa JKCI wakisubiri matibabu ya haraka ili kuokoa maisha yao. Bila matibabu hayo, watoto hawa wanakabiliwa na hatari kubwa ya kupoteza maisha.


"Nawashukuru sana wadau wote waliochangia katika harambee hii ambapo hadi sasa kiasi cha shilingi 2,718,525,000/= kimepatikana. Kiasi hiki kitawezesha kugharamia matibabu ya watoto 500 ambao wanahitaji huduma ya haraka," aliongeza Rais Mstaafu.


Akitoa shukurani za pekee kwa Benki ya NMB kwa mchango wake wa shilingi bilioni moja, aliomba taasisi zingine ziige mfano huu si tu kwa kuwasaidia wagonjwa, bali pia kwa kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika kupunguza au kutatua tatizo hilo.


Pia aliipongeza na kuishukuru taasisi ya kimataifa ya BAPS Charities tawi la Tanzania kwa mchango wake wa dola za Kimarekani laki nne (takriban shilingi 1,078,674,800), pamoja  na Benki ya CRDB kwa kuchangia zaidi ya shilingi milioni 700 katika vipindi tofauti huku ikiahidi kuendelea na zoezi hilo kila mwaka. 


Rais Mstaafu aliwashukuru pia wadau wote waliojitokeza kwenye hafla hiyo kwa kuchangia pesa na wengine kutoa ahadi, akiwaomba kila mmoja wao kuheshimu ahadi aliyotoa ili kufanikisha zoezi zima la kuwaokoa watoto hao wenye matatizo ya moyo.


Dkt. Kikwete pia aliishukuru Serikali ya Awamu ya Tano na ya Sita kwa kuendelea kuwekeza kwenye vifaa vya kisasa katika JKCI na kuleta madaktari bingwa, jambo ambalo limeiongezea uwezo JKCI wa kuhudumia Watanzania wenye maradhi ya moyo.


Alitumia hafla hiyo pia kumtambulisha Prof. David Mwakyusa, ambaye alisema akiwa Waziri wa Afya, yeye na timu yake ya wataalamu aliyoiongoza walitoa mchango mkubwa katika kuanzishwa kwa Taasisi ya JKCI mwaka 2015. 


Mwenyekiti wa HTAF, Mhe. Mussa Hassan Zungu, ambaye pia ni Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amemshukuru Rais Mstaafu kwa kubuni na hatimaye kuanzisha Taasisi ya JKCI, ambayo kwa sasa ni ya tatu kwa ubora barani Afrika, ikifuatia kwa karibu taasisi kama hizo za Misri na Afrika Kusini.


Mhe. Zungu alieleza kuwa uwepo wa JKCI umepunguza kwa kiwango kikubwa gharama za matibabu ya wagonjwa wa moyo, kwani uwepo wa taasisi hiyo umewezesha matibabu yaliyokuwa yakipatikana India na nchi zingine kwa gharama kubwa, sasa kupatikana hapa nchini na kwa ubora uleule wa huduma za nje.


Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI katika risala yake alisema hivi sasa taasisi hiyo imefikisha uwezo wake wa kutoa huduma kwa kiwango cha asilimia 90, na kwamba ina madaktari bingwa wazawa 50 na wa kawaida zaidi ya 40 wanaotoa huduma za kisasa.


Hivi karibuni, JKCI imepokea tuzo ya taasisi ambayo imetoa mchango mkubwa na wa kipekee kiuchumi na kijamii katika kuleta matokeo makubwa kwa kipindi cha mwaka 2023/2024.


Tuzo hiyo ilitolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati akifungua kikao kazi cha wenyeviti wa bodi na watendaji wakuu wa taasisi za umma kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina na kufanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC).


Tuzo hiyo inatoa heshima kwa JKCI kwa hatua zake za kufanikisha malengo ya taasisi na kusaidia taasisi zingine kuweza kufikia mafanikio sawa katika utoaji wa matibabu ya moyo.


Mafanikio haya yanaonesha kazi nzuri ya Taasisi hiyo katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita ambapo JKCI ilitoa huduma za upasuaji mkubwa wa moyo wa kufungua kifua kwa wagonjwa 654, ambao hapo awali walihitajika kwenda nje ya nchi kwa matibabu.


Kupitia upasuaji huo, JKCI imeokoa zaidi ya shilingi bilioni 9.8 za Kitanzania kutokana na huduma hizi kupatikana ndani ya nchi.


JKCI pia imezijengea uwezo nchi za jirani katika kutoa huduma na matibabu ya magonjwa ya moyo, ikiwemo Hospitali ya Moyo ya Zambia, Hospitali ya King Faisal ya Rwanda, Hospitali ya Queen Elizabeth ya Malawi, pamoja na hospitali mbalimbali za hapa nchini.

No comments:

Post a Comment