NAIBU WAZIRI SANGU : WAZAZI TIMIZENI WAJIBU WENU KATIKA MALEZI YA WATOTO - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday 27 September 2024

NAIBU WAZIRI SANGU : WAZAZI TIMIZENI WAJIBU WENU KATIKA MALEZI YA WATOTO

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.Deus Sangu akizungumza na Wazazi pamoja na wanafunzi  katika mahafali ya 37 ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Kibakwe wilayani Mpwapwa Mkoani Dodoma.

Sehemu ya wanafunzi wakiimba wimbo wa Shule ya Sekondari Kibakwe katika mahafali ya 37 ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Kibakwe wilayani Mpwapwa Mkoani Dodoma.

Na Lusungu S. Helela

NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deus Sangu amewataka Wazazi kutimiza jukumu la malezi ya Watoto   badala ya kuwaachia walimu pekee yao  kutokana na wimbi kubwa la mmonyoko wa maadili linaloikumba jamii, Amesema malezi ya wazazi kwa watoto ni muhimu sana katika nyakati hizi.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.Deus Sangu katika mahafali ya 37 ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Kibakwe wilayani Mpwapwa Mkoani Dodoma.

Amesema kitendo cha jumla ya wanafunzi 80 kuacha shule kati ya wanafunzi 247 walioanza kidato cha kwanza mwaka 2021 kutokana na sababu za utoro  na mimba, hii  inaonesha kuwa kuna baadhi ya wazazi hawawajibiki ipasavyo

" Leo  jumla ya  watoto 157  wanahitimu kidato cha nne huku tukiwa  tumepoteza watoto 80 kutokana na tatizo la utoro na mimba za utotoni, hii sio sawa Wazazi liangalieni hili" amesisitiza Mhe.Sangu

Ameongeza kuwa  " Elimu ndo msingi wa kila kitu ukiamua kuwa mfanyabiashara ni lazima uwe na elimu ukitaka kuwa mjasiliamali ni lazima uwe na elimu  ndo maana Mhe.Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan anahakikisha watoto wote wanapata elimu bila ubaguzi wowote"  amesisitiza Mhe.Sangu.

Kufuatia hatua hiyo, Mhe.Sangu amewataka wazazi kujiepusha na tabia ya kuwaozesha mabinti katika umri mdogo badala yake wahakikishe wanakumbatia elimu itakayowaandaa kwa ajili ya kupambana na maisha'

Katika hatua nyingine, Mhe.Sangu amesema Serikali inatarajia kuwapangia vituo vya kazi   jumla ya  Walimu 247  katika Mkoa wa Dodoma hususan katika Wilaya ya Mpwapwa   kutokana na tatizo kubwa la uhaba wa walimu unaoikumba wilaya hiyo.

Amesema walimu hao watapelekwa katika Wilaya mbalimbali ikiwemo Mpwapwa  hivi karibu ikiwa  ni kati ya ajira 11015 za walimu zilizokuwa zimetangazwa na Ofisi ya Rais, Sekretariet ya Ajira mwezi Julai mwaka huu.

Amesema Serikali ya Rais Mhe.Dkt. Samia Suluhu imejipambanua kwa kuhakikisha watoto wanapata elimu iliyo bora  ndio maana anafanya kila liwekanalo kuhakikisha suala la uhaba wa walimu katika shule mbalimbali nchini linakuwa historia.

Aidha, Mhe.Sangu ameipongeza shule hiyo kwa mikakati ya kufuta daraja la nne na sifuri ambapo  wamefanikiwa kwa kiasi  cha hali ya juu jambo ambalo kwa miaka miwili iliyopita hakuna waliopata daraja la nne na sifuri

No comments:

Post a Comment