RAIS HLI DUNIANI KUSHIRIKI MIAKA 30 YA PROLIFE TANZANIA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday, 5 July 2024

RAIS HLI DUNIANI KUSHIRIKI MIAKA 30 YA PROLIFE TANZANIA

Mwenyekiti wa Shirika la Kutetea Uhai (PROLIFE) Tanzania, Emil Hagamu akizungumza na wanachama wa Chama cha Wanahabari Watetezi wa Uhai, Familia, Ndoa na Maisha (JOLIFA)- Tanzania kuhusu maadhimisho ya Miaka 30 ya PROLIFE- Tanzania  yanayofanyika Dar es Salaam Julai 8 hadi 14, mwaka huu.

Mwenyekiti wa Shirika la Kutetea Uhai (PROLIFE) Tanzania, Emil Hagamu akizungumza na wanachama wa Chama cha Wanahabari Watetezi wa Uhai, Familia, Ndoa na Maisha (JOLIFA)- Tanzania kuhusu maadhimisho ya Miaka 30 ya PROLIFE- Tanzania  yanayofanyika Dar es Salaam Julai 8 hadi 14, mwaka huu. Kulia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wanahabari Watetezi wa Uhai, Familia, Ndoa na Maisha (JOLIFA)-Tanzania, Bw. Gaundence Hyera.

Mwenyekiti wa Chama cha Wanahabari Watetezi wa Uhai, Familia, Ndoa na Maisha (JOLIFA)-Tanzania, Bw. Gaundence Hyera (kulia) akifafanua jambo kwa wanahabari katika mkutano huo.

RAIS wa Shirika la Kimataifa la Kutetea Uhai la Human Life International (HLI), Padri Shenan Boquet na Mkurugenzi wa Elimu na Utafiti wa HLI, Dk Brian Clowes ni miongoni mwa wageni kutoka mataifa mbalimbali watakaoshiriki maadhimisho ya Miaka 30 ya Utetezi wa Uhai (PROLIFE) Tanzania yanayoanza Jumatatu.

Mwenyekiti wa Shirika la Kutetea Uhai (PROLIFE) Tanzania, Emil Hagamu amebainisha hayo Dar es Salaam wakati akizungumza na wanachama wa Chama cha Wanahabari Watetezi wa Uhai, Familia, Ndoa na Maisha (JOLIFA)- Tanzania kuhusu maadhimisho ya Miaka 30 ya PROLIFE- Tanzania  yanayofanyika Dar es Salaam Julai 8 hadi 14, mwaka huu.

Hagamu ambaye pia ni Mkurugenzi wa HLI Kanda ya Afrika kwa Nchi zinazozungumza Kiingereza, amesema washiriki wageni katika maadhimisho hayo ni pamoja na viongozi wa dini mbalimbali waliosadia sana Utume wa Utetezi wa Uhai Tanzania, wawakilishi kutoka serikalini na katika Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) na watendaji wa PROLIFE Tanzania katika maeneo yao mbalimbali.

Wengine kwa mujibu wa Hagamu ni kutoka nchi za Lesotho, Zimbabwe, Rwanda, Burundi, Kenya, Marekani, Ireland, na Malawi na sehemu mbalimbali duniani.

“Kutoka Marekani ni pamoja na Rais wa Human Life International (HLI) duniani, Padri Shenan Boquet na Mkurugenzi wa Elimu na Utafiti wa HLI, Dk Brian Clowes,”anasema.

Anaongeza: “Kutoka Burundi, anakuja Mratibu wa Utume wa Uzazi Wajibifu na wakufunzi wawili kutoka Malawi.” 

Amesema PROLIFE Tanzania inaadhimisha miaka 30 ya huduma zake huku ikijivunia mafanikio katika mambo mengi ikiwa ni pamoja na na ushirikiano wa dhati inaoupata kutoka serikalini pamoja na kuokoa mamia ya vijana, wanawake na wanaume wanaopitia changamoto za kifamilia, ndoa na maisha.

“Tunaishukuru serikali kwa namna inavyotuunga mkono maana tulipoona yanayotukera kwa kuhatarisha uhai wa watu, ndoa na familia tuliikimbilia (serikali) na ikatusaidia ndio maana ilikataa hoja na miswada kadhaa iliyokuwa inakwenda kinyume na utamaduni wa uhai na ulinzi wa ndoa na familia,” amesema Hagamu.

Akaongeza: “Serikali wakati wote imeshirikiana nasi kwa kuwa mstari wa mbele kujenga na kulinda utamaduni wa uhai miongoni mwa jamii na kusisitiza watu kujiheshimu, kulinda tunu na maadili....”

Hagamu ametoa mfano akisema: “Kwa mfano, Rais Samia Suluhu Hassan anafanya kazi kubwa kusisitiza tunu na maadili ya taifa… Kwa kweli PROLIFE tunamshukuru na kumpongeza sana Rais kwa kulinda tunu na maadili ya Mtanzania… Hili limetusaidia sana kubeba na kufikisha zaidi dhima hii ya utetezi wa uhai kwa Watanzania. Kwa kweli hii ni serikali sikivu kwelikweli.”

Miongoni mwa mambo ambayo Prolife Tanzania inajivunia kufanikiwa kuyafanya katika kipindi cha uhai wake tangu mwaka 1994 ilipoanzishwa, ni pamoja na kufikisha elimu kwa wanandoa, wanafalia na vijana dhidi ya madhara ya matumizi ya vidhibiti mimba kuweka mpishano wa watoto.

Mengine ni kuelimisha jamii kuhusu madhara ya mauaji yote yakiwamo ya watoto ambao hawajazaliwa kupitia utoaji mimba, madhara ya kuanza vitendo vya ngono mapema na kabla ya ndoa pamoja na kuhimiza uzazi wajibifu.

“Tumeanzisha na kuendeleza program ya majiundo kwa watoto na vijana katika shule na vyuo ili vijana wakue wakizingatia upendo, heshima, imani, uzalendo na usafi wa moyo” 

Anasema PROLIFE imesaidia wanandoa kubaini changamoto zao likiwamo suala la kupanga mpishano wa watoto bila kutumia njia hatarishi za kiafya, kisaikolojia na zinazokwenda kinyume na mafundisho ya imani juu ya uumbaji.

“Tumefikia na kuwasaidia watu wengi wakiwamo walioathirika na vidhibiti mimba, utoaji mimba na tumesaidia watu wengi walioathiriwa kiakili na kiafya katika jamii kutokana na utoaji mimba na dawa za kulevya au changamoto za uzazi katika ndoa…” anasema Hagamu.

Anafafanua: "Tumekuwa tukifundisha wanandoa namna ya kutambua mwenendo wa uzazi ndani ya mwanamke, kuelewa wakati gani anaweza kupata mimba, wakati gani hawezi kupata mimba, namna gani mwanamke awe tayari kiakili na kimwili kupata mtoto…"

Kwa mujibu wa Hagamu, PROLIFE Tanzania katika shughuli zake imegundua wanawake wengi wanaotumia vidhibiti mimba, baadaye hupoteza uzazi na kujuta.

Amesema: “Katika familia nyingi kuna kesi za wanawake kuwanyima waume zao tendo la ndoa na wengi wanasema hawajisikii… Ndio maana tunasisitiza wanandoa kutumia kanuni za asili za kutambua mwenendo wa uzazi na wakati wa kupata mimba, au wakati ambao hata tendo litafanyika mara 100 mimba haiwezi kutungwa.”

Prolife Tanzania pia imeanzisha na kuendesha program kuwaelimisha vijana shuleni na katika vyuo kutambua na kuishi tunu za upendo, heshima, adabu, utii, kazi, usafi wa moyo, imani na uzalendo.

“Tumeanza na vijana shuleni ili wajitambue kuwa wao ni binadamu wenye thamani na heshima kubwa na tumekuwa tukifanya unasihi na uponyaji kwa watu wanaoathirika na matumizi ya dawa za kulevya, vidhibiti mimba na utoaji mimba.

Anatoa mwito kwa Watanzania kuuenzi, kuuthamini na kudumisha uhai wa binadamu ili taifa lipate maendeleo huku wakiwa makini dhidi ya itikadi chafu za mataifa ya Magharibi zinazokengeusha maadili.

No comments:

Post a Comment