IDARA YA NYARAKA NA KUMBUKUMBU ZA TAIFA YAIPONGEZA OFISI YA MAKAMU WA RAIS UJENZI WA MAKAVAZI YA MUUNGANO - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Saturday, 6 July 2024

IDARA YA NYARAKA NA KUMBUKUMBU ZA TAIFA YAIPONGEZA OFISI YA MAKAMU WA RAIS UJENZI WA MAKAVAZI YA MUUNGANO

Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Bw. Firimin Msiangi (katikati) akizungumza jambo wakati wa kikao kazi cha wataalamu cha kujadili muundo wa Makavazi ya Muungano kilichofanyika katika Ofisi za Makamu wa Rais, Mtumba Jijini Dodoma Julai 5, 2024. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Muungano, Bi. Hanifa Selengu.

Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Bw. Firimin Msiangi (kulia) akizungumza jambo wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo cha nyaraka na kumbukumbu za Muungano (Makavazi) katika Ofisi za Makamu wa Rais, Mtumba Jijini Dodoma Julai 5, 2024. Kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi (Sera, Utafiti na Ubunifu) Ofisi ya Makamu wa Rais, Bw. Paulo Laizer.

Na Mwandishi Wetu, DODOMA

IDARA ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa imeipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kubuni ujenzi wa kituo cha kumbukumbu na Nyaraka za Muungano (Makavazi) unaoendelea katika Jengo la Utawala la Ofisi ya Makamu wa Rais Dodoma.

Pongezi hizo zimetolewa Julai 5, 2024 na Mkurugenzi Mkuu wa Idara hiyo, Bw. Firimin Msiangi wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho na kuongeza kuwa kituo kitasaidia kuhifadhi kumbukumbu muhimu za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Msiangi amesema ujenzi wa Kituo hicho umekuja katika wakati mwafaka kwani utarahisisha upatikanaji, uandaaji, uchambuzi na uunganishaji wa taarifa muhimu za utekelezaji wa masuala mbalimbali ya Muungano kwa kuzingatia mahitaji ya kijamii na kiuchumi.

Aidha Msiangi amesema utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka hizo hazina budi kuhifadhiwa katika mfumo wa kielektroniki na nyaraka ngumu ili kurahisisha upatikanaji wake pindi zinapohitajika kwa ajili ya rejea na mapitio kwa wasomaji mbalimbali.

“Muungano ni suala muhimu katika historia ya taifa…Naipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa hatua hii muhimu ya kutenga eneo maalum la kutunza na kuhifadhi nyaraka na kumbukumbu tutaendelea kushirikiana kwa karibu ili kufanikisha ujenzi huu” amesema Msiangi.

Aidha Msiangi amesema Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa itaendelea kutoa ushirikiano kwa Ofisi ya Makamu wa Rais katika kuhakikisha hatua zote zinafikiwa katika ujenzi wa kituo hicho ikiwemo ushauri wa kitaalamu na kiufundi unaohitajika katika usimikaji wa miundombinu ya kituo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi (Sera, Utafiti na Ubunifu) Ofisi ya Makamu wa Rais, Bw. Paulo Leizer ameishukuru Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa kwa ushauri inaoendelea kutoa ikiwemo usimikaji wa miundombinu muhimu itakayosimamia uendeshaji wa kituo hicho.

“Tutahakikisha ushauri uliotolewa tunauzingatia ili kuweza kukidhi mahitaji ya ujenzi wa kituo hiki ambacho ni mahsusi kwa ajili ya utunzaji wa nyaraka na kumbukumbu muhimu za historia ya Muungano wetu” amesema Laizer.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Muungano Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Hanifa Selengu amesema pindi kituo hicho kitakapokamilika kitawezesha kutoa elimu kwa umma na kutunza nyaraka na kumbukumbu mbalimbali za Muungano.

Ameongeza kuwa maeneo yaliyopendekezwa katika makavazi hiyo ni pamoja na sehemu ya kuhifadhi nyaraka, eneo la kupokelea nyaraka, eneo la uhifadhi nyaraka, eneo la kusomea, ukumbi wa mikutano, eneo la makumbusho na eneo la utawala.

Ziara hiyo pia iliongozwa na baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya Ofisi ya Makamu wa Rais na Mkurugenzi wa Idara ya Waasisi kutoka Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Bw.  Salum Kyando.

No comments:

Post a Comment