Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali inaendelea kutoa misaada ya kibinadamu na urejeshaji wa hali kutokana na athari zilizosababishwa na Kimbuga HIDAYA kwenye maeneo ya Kilwa, Mafia, Rufiji na Ifakara.
Amesema kuwa hatua hizo za Serikali zimeshirikisha Wizara za Kisekta, Ofisi za Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Kamati za Usimamizi wa Maafa katika ngazi mbalimbali pamoja na wadau wengine muhimu.
Amesema hayo wakatiakitoa taarifa rasmi kuhusu kimbunga Hidaya kilichotokea Mei 03 mwaka huu katika Pwani ya Bahari ya Hindi.
Amesema kuwa hatua zilizochukuliwa katika Wilaya ya Kilwa ni pamoja kuendesha zoezi la utafutaji na uokokoaji ambapo jumla watu 4,080 wameokolewa katika maeneo mbalimbali.
“Hatua nyingine ni kurejesha hali ya miundombinu ya barabara kuu ya Lindi – Dar es Salaam. TANROADS wapo eneo la tukio wanaendelea na kazi; Juhudi zinafanyika za urejeshaji wa daraja la Somanga - Mtama ili magari yaliyokwama yaendelee na safari”
Waziri Mkuu amesema hatua zilizochukuliwa katika Wilaya za Rufiji na Kibiti ni pamoja na Kutoa huduma ya Afya ya Akili, Msaada wa Kisaikolojia na Kijamii kwa waathirika 1,941(1,501 Kibiti na 440 Rufiji);Kuwaunganisha waathirika 24 (12 Rufiji na 12 Kibiti) walio kambini na huduma za matibabu na hivyo kufanya idadi ya waathirika waliofikiwa na huduma hiyo hadi sasa kufikia 912 (472 Kibiti na 440 Rufiji) na Kutoa elimu ya usafi, ulinzi na usalama kwa mtoto kwa waathirika 1,023 (583 Kibiti na 440 Rufiji).
Katika Wilaya ya Mafia, Waziri Mkuu amesema hatua zilizochukuliwa ni kuwaunganisha waathirika na ndugu na majirani ili wapate hifadhi ya muda baada ya nyumba zao kubomoka na kuzingirwa na maji. Kwa upande wa Kilwa Waziri Mkuu amesema Serikali imeanzisha makazi ya muda kwenye shule za Msingi ambapo kwa sasa wananchi wapo kwenye vituo vitatu vya Shule za Msingi za Mchakama, Ruhatwe na Ndende.
“Mahitaji ya chakula ikiwemo unga, maharage, mafuta ya kula vimepelekwa kwa waathirika; na Kamati ya Usimamizi wa Maafa ya Wilaya ya Kilwa imeendelea kuimarishwa na kuunda Kamati ndogo ndogo kwa ajili ya kuongeza ufanisi katika uratibu na usimamizi wa kukabiliana na madhara yaliyotokea”, Amesema.
Katika Hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema juhudi za kuokoa watu zilifanyika kwa kupeleka Fiber Boat kupitia kikosi cha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ambapo watu wanaendelea na kupelekwa Somanga mjini. “Afya zao ni nzuri na wanaendelea kuhudumiwa. Vilevile, kwa upande wa shule iliyozingirwa na maji, wanafunzi 92 wa kidato cha sita wamehamishwa katika kituo cha mtihani kwenye Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kilwa (FDC)”.
“Katika Mkoa wa Mtwara, Wananchi waliokosa makazi baada ya nyumba zao kubomoka na kuzingirwa na maji katika Manispaa ya Mtwara na Wilaya ya Mtwara Vijijini wameendelea kuunganishwa na ndugu na jamaa kwa ajili ya hifadhi ya muda”.
Katika kata nne za Mbasa, Viwanja Sitini, Kibaoni na Katindiuka zilizoko kwenye Halmashauri ya Mji wa Ifakara ambazo ziliathirika na mafuriko ya mto Lumemo, Serikali imechukua hatua ya kuwahamisha waathirika katika maeneo ambayo ni salama ili kupunguza athari kwa wananchi hao.
“Ili kupunguza athari kwa wananchi ambao nyumba zao zilibomoka na kuzingirwa na maji Serikali imewahamishia waathirika kwenye majengo ya shule na kuwapatia misaada ya kibinadamu kama chakula, vifaa vya malazi na dawa za kibinadamu”
Amesema kuwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limefanya marekebisho ya nguzo zilizoanguka na huduma ya umeme imerejea kwa baadhi ya sehemu.
Hata hivyo, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kulitaarifu Bunge kwamba hadi sasa, mvua zilizonyesha zikiambatana na upepo mkali katika maeneo yote zimesababisha vifo vya watu watano, majeruhi saba, kaya 7,027 zenye watu 18,862 zimeathirika.
No comments:
Post a Comment