Baadhi ya wasanii wadau wa filamu wakiwa katika hafla fupi iliyoandaliwa na kampuni ya MultChoice Tanzania. |
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Innocent Bashungwa akizungumza katika hafla fupi iliyoandaliwa na kampuni ya MultChoice Tanzania. |
Na Projestus Binamungu, WUSM
WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Innocent Bashungwa amewataka wasanii wa Tanzania kutumia muda wao vizuri na kuachana na malumbano, ili kupata muda wa kutengeneza kazi zenye ubora na mvuto kwa watazamaji na wasikilizaji ambazo zitawanufaisha.
Mhe. Bashungwa ametoa kauli hiyo Disemba 2, 2021 jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza katika hafla fupi iliyoandaliwa na kampuni ya MultChoice Tanzania kuonesha mafanikio na mipango yake katika Sekta ya Sanaa. Amefafanua kuwa Serikali itaendelea kuwawekea mazingira wezeshi katika kutimiza ndoto zao kupitia tasinia ya sanaa.
"Watanzania wanahitaji burudani zenye mafundisho na zilizo andaliwa kwa kiwango kinacho ridhisha nashauri wasanii kutumia muda wenu vizuri kuzalisha filamu au kutengeneza muziki unaokidhi vigezo kwa ajili yenu na kwa ajili ya taifa". Amesema Mhe. Bashungwa.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Multchoice Tanzania, Bi. Jacquiline Woisso ameishukuru Serikali kwa ushirikiano mkubwa inaowapatia katika utendaji wa kazi zao za kila siku.
Aidha, Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dkt. Kiagho Kilonzo ameiomba Kampuni ya Multchoice Tanzania kupandisha bei ya ununuzi wa filamu akisema baadhi ya wasanii hawako tayari kupeleka filamu zao katika kampuni hiyo kwa madai kuwa gharama ya ununuzi wa filamu zao bado ni ndogo ikilinganishwa na ubora na gharama kubwa zinazotumika kuandaa filamu hizo.
Hafla hiyo fupi imeenda sambamba na uzinduzi wa filamu mbili ambazo ni tamthilia ya Danga na la Familia.
No comments:
Post a Comment