UWEZO TANZANIA, ALiVE KUSHIRIKIANA NA WANAHABARI KUENEZA ELIMU YA STADI ZA MAISHA NA MAADILI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 4 August 2025

UWEZO TANZANIA, ALiVE KUSHIRIKIANA NA WANAHABARI KUENEZA ELIMU YA STADI ZA MAISHA NA MAADILI

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Uwezo Tanzania, Bw. Baraka Mgohamwende (kushoto) akizungumza alipokuwa akifunga warsha ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari ili kuhakikisha wanakuwa sehemu ya nyenzo za kutoa elimu kufanikisha mradi wa stadi za maisha na maadili kwa vijana kati ya miaka 6 hadi 17.

Mkurugenzi wa Shirika la SAZAN, Zanzibar, Bi. Safia Mkubwa akizungumza katika warsha ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari ili kuhakikisha wanakuwa sehemu ya nyenzo za kutoa elimu kufanikisha mradi wa stadi za maisha na maadili kwa vijana kati ya miaka 6 hadi 17.

Warsha ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari ili kuhakikisha wanakuwa sehemu ya nyenzo za kutoa elimu kufanikisha mradi wa stadi za maisha na maadili kwa vijana kati ya miaka 6 hadi 17 ikiendelea, wa kwanza kulia ni Afisa Programu Mwandamizi toka Shirika la Milele Zanzibar Foundation, Bw. Samson Sitta.

Meneja Mawasiliano wa Shirika la Uwezo Tanzania, Bw. Greyson Mgoi (kulia) akiwasilisha mada kwenye warsha ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari ili kuhakikisha wanakuwa sehemu ya nyenzo za kutoa elimu kufanikisha mradi wa stadi za maisha na maadili kwa vijana kati ya miaka 6 hadi 17. Wa pili kulia ni Afisa Programu Mwandamizi toka Shirika la Milele Zanzibar Foundation, Bw. Samson Sitta akifuatilia.

Washiri katika picha ya pamoja mara baada ya wafunzo hayo.

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

MKURUGENZI Mtendaji wa Shirika la Uwezo Tanzania, Bw. Baraka Mgohamwende amesema taasisi hiyo kwa kushirikiana na wadau wengine wameanza kuwajengea uwezo waandishi wa habari ili kuhakikisha wanakuwa sehemu ya nyenzo za kutoa elimu kufanikisha mradi wa stadi za maisha na maadili kwa vijana au watoto kati ya miaka 6 hadi 17.

Bw. Mgohamwende amesema hayo juzi jijini Dar es Salaam alipokuwa akifunga warsha ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari ili kuhakikisha wanakuwa sehemu ya nyenzo za kutoa elimu kufanikisha mradi wa stadi za maisha na maadili kwa vijana kati ya miaka 6 hadi 17.

Alisema kwa sasa wanafanya kampeni kwa waandishi wa habari kwa kipindi cha wiki 10, huku lengo likiwa ni kuhakikisha ushirikiano huo na vyombo vya habari unaendelea kwa kipindi cha hadi miaka mitano ili kuhakikisha kila mdau ambaye anafanya kazi na vijana wakiwomo wazazi wanaingiza elimu ya stadi za maisha na maadili kwa kundi la vijana.

"...Katika karne ya 21 tunaitaji vijana wengi wawe na uwezo wa ujuzi laini ambao unaweza kuwafanya wawe tayari kutatua changamoto zao na pia kuwa na ushirikiano wa kutosha kati yao, kama tunavyoona katika jamii zetu changamoto kubwa wanaopata watoto na vijana ni kushindwa kumudu utatuzi wa changamoto zao za kawaida jambo linalochangia wao kushindwa kufanya maamuzi sahihi," alisema.

Aliongeza kuwa taasisi ya Uwezo imefanya utafiti katika Wilaya 45 za Tanzania na kubaini kuwa stadi za maisha na maadili, yaani ujuzi au umahiri kwa vijana bado upo chinmi sana na kwa maana hiyo panaitajika juhudi za makusudi kwa kila muhusika kuweza kusaidia kundi hilo la vijana kukuza stadi za maisha na maadili kwao.

Kwa upande wake, Afisa Programu Mwandamizi toka Shirika la Milele Zanzibar Foundation, Bw. Samson Sitta miongoni mwa wadau wanaotekeleza mradi huo, alisema mradi unatekelezwa na mashirika takribani manne kwa Tanzania, na kwa sasa umejikita kuangalia ni namna gani stadi za maisha na maadili vinaweza kuingizwa katika mfumo wa elimu nchini ili kuwajenga vijana.

Alisema hatua hiyo itawezesha kuona vijana wanapomaliza elimu yao wanapata pia elimu ya stadi za maisha na maadili, zinazoweza kuchangia kitu kwenye taaluma zao walizozipata wakiwa shuleni. 

"...Ni namna gani tunaingiza stadi hizi za maisha na maadili kwenye mitaala ya elimu, tunafanya kazi na taasisi ya elimu Zanzibar na taasisi ya elimu Tanzania Bara na mabaraza ya mitihani pande zote mbili kushirikiana kwa pamoja namna ya kuingiza mada za stadi za maisha na maadili kwenye mtaala mpya ulioboreshwa wa elimu nchini.

Alisema kwa sasa wanawaandalia walimu moduli ambazo zitatumia kuwaandaa walimu kwanza kabla ya wao kuanza kuingiza elimu ya stadi za maisha na maadili katika mada zao mbalimbali wanazozitumia kuwafundisha wanafunzi shuleni.

"...Kwa sasa tunafanya kazi kuangalia namna ambavyo tutawaandalia walimu moduli au vitu ambavyo watajifunza katika kozi zao za mafunzo ya ualimu ili waweze kujua kiurahisi kabisa katika masomo wanayofundisha namna gani mulemule ndani wanaweza kupanga maandalio ya somo na kutengeneza mbinu mahususi ambazo zitakuwa zikikuza stadi za maisha na maadili kwenye hayo hayo masomo wanayofundisha kwa watoto," alisema Bw. Sitta akizungumza katika wasilisho lake kwa washiriki wa warsha hiyo.

Aidha aliongeza moduli wanazoziandaa mbali na kusambazwa katika vyuo vya walimu ili kuwaandaa, pia zitatumika kuwajengea uwezo walimu ambao tayari wanaendelea na kazi shuleni kwa sasa nao kuweza kuwa na elimu ya stadi za maisha na maadili kabla ya kuanza kuitumia kuchopeka kwenye mada zao kwa ajili ya wanafunzi.

No comments:

Post a Comment