Kamamti ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeipongeza Wizara ya Ujenzi kwa kuandaa andiko la mkakati wa kuwawezesha makandarasi wazawa na washauri elekezi kwenye utekelezaji wa miradi ya Ujenzi na kusisitiza andiko hilo kushirikisha wataalamu kutoka Sekta mbalimbali nchini ili kuweza kuleta tija kwa Taifa.
Akizungumza katika Semina
iliyofanyika jijini Dodoma Mwenyekiti wa Kamati ya PAC, Mheshimiwa,
Naghenjwa Kaboyoka, pamoja na mambo mengine amesisitiza ni muhimu kwa Wizara
kupata maoni kutoka kwa wahandisi, wakandarasi, wachumi na wataalam kutoka
Wizara ya Fedha ili kuona namna ya kuboresha wazo hilo.
“Tunawapongeza Wizara ya
Ujenzi kwa kuja na wazo hili, wazo ni zuri na tumelipokea, maoni mliopewa na
waheshimiwa wabunge hakikisheni mnayafanyia kazi na mpange tena semina nyingine
ya kushirikisha wadau wote ili kupata maoni zaidi”, amesema Kaboyoka.
Aidha, amefafanua kuwa moja
ya mapendekezo yanayotakiwa kufanyika ni pamoja na maboresho katika Sera ya
Ujenzi na mabadiliko ya Sheria ambazo zinamnyonya mkandarasi wa ndani na
kuhakikisha wataalam hao wanajengewa uwezo kwa kupatiwa fursa ya kutekeleza
miradi midogo na mikubwa.
Kwa upande wake, Naibu
Waziri wa Ujenzi, Mha. Godfrey Kasekenya ameishukuru Kamati ya PAC kwa
kuendelea kutoa ushirikiano ili kuhakikisha kuwa ushiriki wa Makandarasi na
Wahandisi Washauri Wazawa unasimamiwa kikamilifu kwa ukuaji wa uchumi na
maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
Kadhalika, Kasekenya ameeleza
kuwa Tathmini iliyofanyika ilibaini kuwa wazawa walitekeleza miradi 35,351
yenye thamani ya shilingi Trilioni 23.749 sawa na asilimia 38.5 ya jumla ya
thamani ya miradi yote 36, 839 yenye thamani ya Shilingi Triloni 61.638
iliyosajiliwa katika kipindi cha kuanzia 2013 hadi 2023.
“Ni Dhahiri kwamba ingawa wazawa wametekeleza miradi mingi kwa idadi, lakini miradi hiyo ina thamani ndogo kuliko miradi michache iliyotekelezwa na wageni, hali hii haikubaliki, ni lazima tufanye mikakati ya haraka kuwainua wazawa”, amesema Kasekenya.
Naye, Muwasilishaji wa
andiko hilo, abaye pia ni Mtendaji Mkuu wa Baraza la Taifa la Ujenzi, Dkt.
Matiko Nturi, amesema kuwa utafiti uliofanyika
umeonesha masuala mbalimbali
ikiwemo wazawa kukosa uzoefu wa utekelezaji wa miradi mikubwa, uwezo wa kifedha
au mitaji ya kutosheleza kutekeleza miradi, kutokuwa na mitambo ya uhakika
pamoja na wataalam wa kutosha wenye uzoefu na hivyo wengi kushindwa kukidhi
vigezo vya zabuni.
No comments:
Post a Comment