Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na
Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi amesema Serikali itaendelea kuweka
mazingira wezeshi kwa Watu wenye Ulemavu ili kukuza ustawi wa kundi hilo katika
kuchochea shughuli za maendeleo.
Ameeleza hayo katika tamasha la kimataifa la familia yenye furaha la Watu wenye
Uziwi na usikivu hafifu, lililofanyika jijini Dar es Salaam ambapo tamasha hilo
lilihusisha pia mshindano la kumsaka mrembo, mtanashati pamoja na mwanamitindo
bora duniani mwenye Uziwi.
Aidha, Mhe. Katambi amesema kuwa Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan anawapenda
na kuwajali Watu wenye Ulemavu na ndio maana serika anayoiongoza imeunda wizara
mahususi ili kusimamia watu wenye ulemavu.
Amebainisha kuwa Serikali inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan imefufua
vyuo vya Watu wenye Ulemavu kwa kutumia Tsh. Bilioni 3.4 kukarabati miundmbinu
ambayo imechakaa katika vyuo 6.
Pia ameeleza kwa mwaka huu wa fedha 2023-2024 serikali imetenga Bil. 3 kwa
ajili ya ujenzi wa vyuo vipya vitatu vya ufundi stadi ili kuongeza udahili wa
vijana wenye Ulemavu kupata ujuzi utakaowawezesha kujiajiri au kuajiriwa.
Vile vile, katika kuimarisha utambuzi wa mapema wa watoto wenye Ulemavu,
serikali imeandaa mwongozo wa utambuzi wa mapema na afua staki kwa watoto wenye
Ulemavu.
Sambamba na hayo, amesema kuwa Serikali imeendelea kuwawezesha Watu wenye
Ulemavu kiuchumi kama ilivyoainishwa katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya
mwaka 2020 kwa lengo la kuwawezesha kujikwamua kiuchumi.
Tamasha hilo limehusisha washiri zaidi ya 200 kutoka mataifa ya Afrika Kusini,
Australia, Belarus, Brazil, Ethiopia, Falme za Kiarabu, Guyana, Haiti,
Hispania, India, Iran, Italia, Kenya, Kongo DRC, Malasia, Macedonia, Marekani,
Mexico, Misri, Morocco, Msumbiji, Nigeria, Pakistan, Poland, Romania, Rwanda,
Senegal, Siera Leone, Sudan Kusini, Thailand, Tunisia, Jamhuri ya
Czechoslovakia, Ufaransa, Uganda, Ujerumani, Ukraine, Urusi, Zambia, Zimbabwe
na wenyeji Tanzania.


No comments:
Post a Comment