WADAU wa masuala ya Jinsia wameiomba Serikali kuweka mifumo na mikakati ambayo itasaidia kupambana na vitendo vya ukatili dhidi ya Wanawake hasa katika njanya ya siasa nchini.
Ombi hilo limetolewa jijini Dodoma Agosti 09, 2023 wakati wa kikao kilichoandaliwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum na wadau kwa lengo la kujadili na kuweka mikakati muhimu ya kupambana na vitendo vya ukatili dhidi ya Wanawake katika siasa.
Akizungumza katika kikao hicho Mbunge wa Viti Maalum (NGOs) Mhe. Neema Lugangira amesema kumekuwa na changamoto za ushiriki wa Wanawake kwenye nyanya ya siasa hasa ngazi za mitaa na Kata.
Akitoa takwimu za uwiano kati ya Wanaume na Wanawake katika uongozi kwa ngazi ya Mitaa na Kata amesema kwa ngazi ya Vitongoji kuna Viongozi Wanawake 4117 kati ya Viongozi 58441 sawa na asilimia 6.7 huku kwa ngazi ya Mitaa Wanawake viongozi ni 528 kati ya 4117 sawa na asilimia 12.6.
Aidha kwa ngazi ya Kijiji wanawake Viongozi ni 246 kati ya 11915 sawa na asilimia 2.1 huku kwa ngazi ya udiwani na ubunge ikiwa na asilimia za kuwa na Viti Maalum kwa ajili ya Wanawake.
"Ingawa kuna jitihada nyingi za Serikali na wadau zimefanyika kuhakikisha Wanawake wanashiriki kugombea nafasi za uongozi hasa kwenye nyanja za kisiasa, bado nguvu inahitajika kukabiliana na vitendo vya unyanyasaji na madhila mengine yanayowakumba Wanawake katika kugombea nafasi za uongozi " amesema Mhe. Neema
Pia amewaasa Wanawake kutokata tamaa katika kugombea nafasi mbalimbali za kisiasa na wanapofanyiwa vitendo vya ukatili kwenye hatua mbalimbali za kugombea nafasi hizo.
Akijibu baadhi ya hoja za wadau Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Evelyn Makala amesema kuwa Serikali inakaribisha wadau mbalimbali kutoa maoni yao hasa Viongozi Wanawake katika siasa ili kuwa na takwimu sahihi kutoka kwa wahusika wenyewe na kuweka mipango madhubuti ya kuwawezesha na kuwajengea uwezo Wanawake kushiriki katika kugombea nafasi za uongozi.
Ameongeza kuwa Serikali imeona changamoto ya uwiano mdogo wa Viongozi Wanawake na wanaume hivyo Wizara kwa kushirikiana na Wizara za kisekta zinaweka mikakati mbalimbali kwa kushirikiana na wadau ili kuhamasisha Wanawake kushiriki katika kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ngazi zote nchini.
"Changamoto zilizotolewa na wadau na maoni yenu tumeyachukua na tutayafanyia kazi kwa kushirikiana na wenzetu Wizara nyingine na wadau wengine wa masuala ya usawa wa kijinsia ili tuwe na uwiano mzuri wa wanawake na wanaume katika ngazi za uongozi" amesema Evelyn.
Naye Mkurugenzi wa Shirika la NDI Sandy Quimbaya amesema Shirika lake lipo tayari kufanya tafiti mbalimbali kuhusu vitendo vya ukatili dhidi ya Wanawake hasa katika njanya ya siasa ili kuwa na mipango madhubuti ya kuhakikisha Serikali kwa kushirikiana na wadau inapambana kutokomeza vitendo hivyo.
No comments:
Post a Comment