Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Ikungi, Mariam Mwandikile akichangia jambo kwenye kikao hicho.
Afisa Mawasiliano na Vijana wa shirika hilo Edna Mtui (kushoto) akiteta jambo na Ofisa wa shirika hilo, Aisha Msuya.
Na Dotto Mwaibale,Singida.
SHIRIKA la Empower Society Transform Lives (ESTL) linalojihusisha na
masuala ya kupinga ukatili wa kijinsia
limezindua rasmi huduma za elimu na uwezeshaji jamii kwenye wilaya ya
Ikungi mkoani hapa ambazo pamoja na mambo mengine zitajikita katika kuhakikisha
elimu ya kutosha inatolewa kwa wana Ikungi hususani kwenye kata mbili za Kikio
na Misughaa katika muktadha wa dhana hasi ya kuondokana na vitendo vya ukatili
kwa wanawake na watoto.
Kabla ya huduma hizo kutolewa wilayani Ikungi shirika hilo lisilo la kiserikali
kwa udhamini wa Ubalozi wa Finland,Uholanzi na Shirika la Foundation Civil Society (FCS) katika kipindi cha
miaka minne (2018/2022 limefanikiwa kuzifikia takribani kata 28 ndani ya Wilaya
za Singida Manispaa na Singida Vijijini kwa utekelezajiwa huduma kama hizo.
Kwa mujibu wa shirika hilo huduma nyingine walizofanikiwa kuzitoa kwenye
maeneo hayo ni pamoja na uanzishwaji wa utaratibu wa utoaji huduma mbalimbali
ndani ya eneo moja (One Stop Centre), uundaji wa kamati za MTAKUWWA zipatazo 39
sambamba na uanzishaji wa mfumo maalumu wa TEHAMA ambao umekuwa ukifanya kazi
ya kufuatilia kesi za matukio ya ukatili-ambapo kwasasa shirika lina mpango wa
kuuwezesha mfumo huo kufanya kitaifa.
Akizungumza wakati akifungua kikao cha tathmini na uzinduzi wa mradi huo, mbele ya kamati ya MTAKUWWA ngazi ya halmashauri ya wilaya ya Ikungi kupitia ufadhili wa Shirika la Foundation Civil Society (FCS) , Mkurugenzi wa ESTL Joshua Ntandu Lisu alisema wilaya hiyo ina vihatarishi vikubwa vya matukio ya ukatili kwa wanawake na watoto kutokana na jiografia yake ya mipaka na wilaya za jamii ya wafugaji za Hanang (Manyara) na Kondoa (Dodoma) zilizopo kwenye bonde la ufa ambazo kwa kiwango kikubwa zimegubikwa na matukio ya ukeketaji.
Hata hivyo, mjumbe wa kamati ya mtakuwwa ambaye ni Mkuu wa Polisi Wilaya ya
Ikungi (OCD) Suzana Kidiku alisema jeshi hilo limekuwa kwenye harakati
mbalimbali za kukabiliana na matukio ya ukatili wa kijinsia kwa nyakati
tofauti, ambapo kwa kipindi cha mwezi Julai hadi Septemba mwaka huu
limefanikiwa kunusuru kwa kuwarejesha shuleni wanafunzi watatu ambao walikuwa
hatarini kukatisha masomo yao kutokana na matukio ya ukatili.
Pia Kidiku alisema jeshi hilo wilayani hapa katika kipindi hicho
limefanikiwa kufikisha kesi tatu za matukio ya ukatili wa kijinsia kwenye
vyombo vya sheria, ambapo hata hivyo, mahakama iliwakuta watuhumiwa wakiwa na
hatia, na wawili walihukumiwa vifungo vya hadi miaka 30 huku mmoja akiadhibiwa
kifungo cha maisha.
Aidha, Mkaguzi wa Uhamiaji Wilaya ya Ikungi Abel Shindayi alisema kuna haja
ya mamlaka za elimu kufanya marekebisho ya mfumo wa mtaala wa elimu uliopo kwa
kuongeza kipengele cha somo la ukatili wa kijinsia, athari zake na namna bora
ya kukabiliana na matukio hayo kuanzia ngazi za shule za msingi hadi vyuo ili
kuwafanya wanafunzi kuwa na uelewa mpana wa masuala hayo.
Awali, akifungua kikao cha tathmini na uzinduzi wa mradi huo Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Richard Rwehumbiza aliwasihi viongozi wa shirika hilo kutofanya kazi kwenye kata mbili pekee bali wasambae kwenye kata zote ili kusaidia kuelimisha jamii hiyo kuachana na unyanyasaji wa aina zote hasa ukeketaji-ambao kwa sasa umeanza kuathiri hadi watoto wenye umri wa chini ya siku saba.
No comments:
Post a Comment