NMB YAZINDUA WORLDWIDE PESA, HAKUNA MIPAKA KUTUMA FEDHA EAC, SADC - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday, 29 November 2024

NMB YAZINDUA WORLDWIDE PESA, HAKUNA MIPAKA KUTUMA FEDHA EAC, SADC







NA MWANDISHI WETU

BENKI ya NMB imezindua Huduma ya Kimkakati kwa Ustawi wa Sekta ya Fedha na Uchumi wa Taifa ‘NMB Worldwide Pesa, inayowapa fursa Watanzania ya kutuma na kupokea pesa kutoka nchi 22 za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kupitia simu za mkononi.

Uzinduzi wa NMB Worldwide Pesa ‘Dhumuni Halina Mipaka,’ umefanyika jijini Dar es Salaam leo Alhamisi Novemba 28, ikizinduliwa na Mkurugenzi wa Biashara ya Kimataifa na Diplomasia ya Uchumi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi John Ulanga.

NMB Worldwide Pesa inayoletwa kwa ushirikiano wa NMB, Mastercard, Thunes, TerraPay na Nala, ni zao la maboresho maalum ya huduma ya Worldwide Pesa iliyozinduliwa mwaka jana, ikilenga kuwawezesha Watanzania waishio nje ya nchi ‘Diaspora,’ kutuma fedha nchini kutokea kote duniani.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Afisa Mkuu wa Wateja Wakubwa na Serikali wa NMB, Alfred Shao, dhamira ya huduma hiyo ni kusapoti lengo la Serikali la kuongeza kiwango cha fedha kinachopokelewa kutoka kwa Diaspora wa Tanzania hadi kufikia kiasi cha Sh. Trilioni 3.75 kwa mwaka ifikapo mwaka 2028.

“Kwa kulitambua lengo hilo, nasi kuunga mkono, NMB tuko hapa kuleta masuluhisho muhimu ya kuendana na adhma hiyo ya Serikali na taifa letu kwa ujumla, na Worldwide Pesa itakuwa na mchango mkubwa sio tu wa kufanikisha lengo hilo, bali pia kutanua wigo wa huduma zetu na kuzifanya kuwa za kisasa zaidi.

“Kwetu sisi NMB, ni heshima kubwa kwetu kupata imani kutoka kwa washirika wetu ambao ni taasisi za fedha kama Mastercard, Thunes, TerraPay na Nala, ambazo zina mtandao mpana na mahusiano na mabenki makubwa ya nchi nyingi za ndani na nje ya Afrika,” alibainisha Shao.

Aliongeza ya kuwa, ushirikiano wa taasisi hizo utaiwezesha NMB kuongeza tija ya huduma za kifedha (kutuma na kupokea), huku akitambia uwekezaji mkubwa ambao wameufanya kwenye Teknolojia ya Kidijitali hasa kwenye Kulinda Usalama wa Mifumo na Taarifa za Benki na Wateja ‘Cybersecurity Technologies.’

Aidha, Shao aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia kwa kujenga misingi imara inayoharakisha ukuaji wa sekta ya fedha, huku akiahidi benki yake kuendeleza mashirikiano mema na Benki Kuu ya Tanzania katika kuhakikisha taifa linapiga hatua za haraka za kimaendeleo

Kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mohamed Thabit Kombo, Balozi Ulanga aliipongeza NMB kwa mapinduzi chanya na uwekezaji mkubwa wa kiteknolojia katika kufanikisha huduma rahisi, rafiki, nafuu na salama kwa ukuaji wa haraka wa uchumi wa wateja na Watanzania.

“Siri namba moja ya mafanikio yenu ni pamoja na kujali wateja na namna ya kutatua changamoto zao, pili matumizi ya teknolojia kwa sababu kampuni zote zilizofanikiwa duniani, zimefaanya uwekezaji katika eneo hilo na siri ya tatu ni wafanyakazi weledi, wabunifu na mkiendelea ‘ku-focus’ katika hayo, mtafanikiwa zaidi.

“Sisi kama Serikali tuna furaha kuona huduma yenu hii mpya imeanza na nchi 22 wanachama wa Jumuiya mbili kubwa Afrika yaani Afrika Mashariki (EAC) na Kusini mwa Afrika (SADC), kwani itakuwa chachu ya mzunguko wa fedha katika ukanda huu, ambao sisi ni wanachama wa jumuiya zote mbili,” alisisitiza.

Balozi Ulanga aliitaka NMB kuunda mfumo utakaowezesha matumizi ya huduma hiyo kutoka benki zote na kwamba hilo litaharakisha na kuongeza kasi ya ukuaji wa taasisi hiyo, ambayo kwa ilipofikia inapaswa kuvuka mipaka ya nchi na bara la Afrika kutokana na ukubwa na ubora wake kihuduma

“Kwa sasa wacha tuendelee na mataifa 22, lakini dhamira iwe kuvuka mipaka ya kujitanua kama ndio kweli benki bora ya kimapinduzi, napowapongeza kwa ‘innovation’ hii, nitumie nafasi hii kuwaahidi kuwa Wizara tuko tayari kuwasaidia kufikia malengo yenu, ambayo yanasaapoti uchumi wa taifa.

“Kwa ‘innovation’ hizi, haitoshi kusema NMB tupo tu Tanzania, tunapaswa kuvuka mipaka ya nchi na bara zima la Afrika.. Tuna wafanyabiashara hapa kutoka mataifa ya Comoro, DRC, ambao kitovu cha ukuaji wao kibiashara ni Tanzania, kwahiyo tunapaswa kuiona NMB Bank nchini Comoro, ambako itakuwa kubwa kule,” alisema.

Kwa upande wake, Meneja wa Akaunti – Afrika Mashariki wa Thunes, Jack Ngari, aliishukuru NMB kwa kujenga msingi imara wa ushirikiano kihuduma na kwamba imani waliyopata kutoka kwa NMB inawapa nguvu ya kushiriki ukuzaji uchumi wa Tanzania, jambo ambalo ni fahari kwao.

Naye Doreen Ngalo, ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa TerraPay, alisema wanajivunia miaka mitano ya ushirikiano wa kibiashara na NMB, wenye wastani wa miamala ya kimataifa yenye thamani ya zaidi ya Dola Mil. 1.2 na kwamba uzinduzi wa NMB Worldwide Pesa unawapa uhakika wa kuongezeka kwa miamala hiyo.

No comments:

Post a Comment