Mtafiti Mkuu wa Udongo kutoka Chuo cha TARI, Uyole Mbeya Fedrick Mlowe akiwafundisha maafisa Ugani mkoani Ruvuma namna ya kupima udongo.
Na Albano Midelo, Ruvuma
MAAFISA Ugani 34 kutoka wilaya zote tano za Mkoa wa Ruvuma wamepewa mafunzo ya maandalizi ya upimaji wa afya ya udongo yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Songea Klabu mjini Songea.
Mafunzo hayo yameendeshwa kwa wiki moja kutoka kwa wataalam wa chuo cha TARI Uyole jijini Mbeya.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma Emanuel Kisongo, amesema mafunzo hayo ya wataalam wa kilimo ngazi ya Kata na vijiji yatawajengea uwezo wa kutekeleza zoezi la upimaji wa udongo linalotarajia kufanyika katika vijiji 100 mkoani Ruvuma.
Ametoa rai kwa maafisa kilimo hao mara baada ya kufuzu mafunzo hayo wakasimamie na kutekeleza kwa weledi zoezi la upimaji wa afya ya udongo katika vijiji ambavyo watapangiwa ambapo kila Afisa Ugani aliyepata mafunzo amepangiwa kufundisha vijiji vinne.
Katika hatua nyingine Katibu Tawala huyo wa Mkoa wa Ruvuma amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kutoa pikipiki 282 kwa ajili ya maafisa Ugani wa Kata na vijiji mkoani Ruvuma.
“Maafisa Ugani wa Kata na Vijiji wa Mkoa wa Ruvuma kila mmoja atapata pikipiki moja na seti ya vifaa vya kutolea huduma za ugani katika zoezi la kutambua afya ya udongo katika maeneo mbalimbali ndani ya Mkoa,’’ alisema Kisongo.
Kwa upande wake Mtafiti Mkuu wa Udongo Kutoka Chuo cha TARI –Uyole jijini Mbeya Fredrick Mlowe amesema zoezi hili lipo katika awamu ya tatu ya utekelezaji ambapo awamu ya kwanza ilikuwa mikoa ya Mbeya na Songwe awamu ya pili ilikuwa mikoa ya Rukwa,Mbeya ,Iringa na Morogoro.
Mlowe ameitaja dhima ya mafunzo hayo kuwa ni kwa lengo la kujenga uelewa wa afya ya udongo katika kanda sanjari na kuzishauri kampuni za uzalishaji wa Mbolea kutoa mapendekezo ya mazao mbalimbali ili yaweze kuzalishwa kwa tija.
Mtafiti huyo amesema matokeo hayo yatawasaidia wazalishaji wa mbolea kutengeneza mbolea inayoendana na hali ya maeneo kulingana na matokeo yaliyopatikana katika upimaji wa afya ya udongo.
Naye Afisa Biashara Mkoa wa Ruvuma Martin Joseph akimwakilisha Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji, amesema maafisa ugani waliopata mafunzo watasaidia wakulima wa Mkoa wa Ruvuma kujua matumizi sahihi ya mbolea ili waweze kulima kwa tija.
No comments:
Post a Comment