MASHINE ZA KUCHANGANYA CHUMVI NA MADINI JOTO - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday, 24 February 2022

MASHINE ZA KUCHANGANYA CHUMVI NA MADINI JOTO

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof.Abel Makubi akikabidhi nyaraka za mashine za kuchanganyia chumvi na madini joto kwa katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI Prof. Riziki Shemdoe kwa ajili ya kuwakabidhi Makatibu Tawala  wa mikoa ya Pwani, Mtwara na Tanga ili kusaidia kuongeza uzalishaji wa chumvi yenye kiwango cha kutosha cha madini joto.

Mashine za kuchanganya chumvi na madini joto zitakazosimikwa katika mikoa ya Pwani, Tanga na Mtwara ambazo Wizara ya Afya imezikabidhi  kwa Ofisi ya Rais-TAMISEMI mara baada ya kutolewa na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania kupitia ufadhili wa shirika la Nutrition International kwa ajili ya kusaidia kuongeza uzalishaji wa chumvi yenye madini joto ya kutosha.

WIZARA  ya Afya imekabidhi mashine tano za kisasa za kuchanganya chumvi na madini joto kwa Ofisi ya Rais - TAMISEMI zilizotolewa na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania kupitia shirika la Kimataifa la Nutrition Intenational kwa ajili ya kusimikwa katika Mikoa ya Tanga, Pwani na Mtwara ili kusaidia kuongeza uzalishaji wa chumvi yenye kiwango cha  kutosha cha madini joto nchini.

Akizungumza wakati wa kukabidhi mashine hizo kwa katibu mkuu Ofisi ya Rais -TAMISEMI, katibu mkuu wizara ya Afya Prof. Abel Makubi amesema Utafiti uliofanyika nchini mwaka 2019 ulibaini Tanzania inazalisha chumvi Tani 330,712 kwa mwaka na kati ya Chumvi hiyo Tani 141, 22 ambapo ni sawa na asilimia 43 haiwekwi madini joto hivyo ujio wa mashine hizo utasaidia kuongeza uzalishaji wa chumvi yenye madini hayo.

Prof Makubi amesema mashine hizo ambazo zimetengenezwa nchini na wataalamu kutoka VETA zimeweza kugharimu kiasi cha shilingi milioni 55 huku gharama ya mashine moja ikigharamu kiasi cha shilingi milioni 11 na kusaidia kuokoa milioni 14 kwa kila mashine endapo zingeagizwa kutoka nje ya nchi.

“Mwaka 2018 shirika la Nutrition International ilifadhili ununuzi wa mashine tatu zilizoagizwa kutoka Afrika Kusini kwa jumla ya Shilingi milioni 75 ambapo mashine moja iligharimu shilingi Milioni 25 na kusimikwa Halmashauri za Kilwa, Hanang na Meatu na zinaendelea kufanya kazi na safari hii mashine hizo zimeweza kutengenezwa na Watalaam wetu kutoka VETA kusaidia kuokoa shilingi milioni 14 kwa kila mashine” alisema Prof Makubi.

Awali akitoa maelezo juu ya programu ya kuzuia upungufu wa madini joto nchini Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania, Dkt. Germana Leyna amesema Madini joto ni moja ya kirutubisho muhimu kwa ukuaji mzuri wa akili na mwili wa binadamu na endapo mtu atakuwa na upungufu wa madini joto basi anaweza kupata madhara mbalimbali ikiwa ni pamoja na udumavu wa akili na mwili.

Dkt. Germana amesema katika kukabiliana tatizo la upungufu wa madini joto Taasisi ya Chakula na Lishe inatekeleza programu ya kuzuia upungufu wa madini joto nchini kwa kutumia mkakati endelevu wa kuongeza madini joto kwenye chumvi (Universal Salt Iodation) kuanzia miaka ya tisini na mkakati huo unalenga kuhakikisha kuwa angalau asilimia tisini (90%) ya kaya zote nchini zinatumia chumvi yenye madini joto ya kutosha kama inavyopendekezwa na shirika la afya duniani (WHO).

“Serikali kwa kupitia Taasisi ya Chakula na Lishe kwa kushirikiana na wadau wengine tumefanya jitihada mbalimbali ikiwemo kutoa elimu na mafunzo kwa wazalishaji chumvi kuhusu uzalishaji bora na uchanganyaji wa chumvi na madini joto, kuhakikisha upatikanaji wa madini joto,  kutoa vifaa vya kupimia uwepo wa madini joto kwenye chumvi (Test Kits) na vile vya kuangalia kiwango cha madini joto yaliyomo kwenye chumvi (WYD mashines).” alisema Dkt. Germana.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Nutrition International Dkt. Daniel Nyagawa amesema katika Mpango mkakati wake wa miaka 6 ulioanza mwaka 2018 hadi 2024 shirika hilo limejielekeza kufanya kazi zake kwa karibu na Serikali na Taasisi zake ili kwa pamoja  kuweza kupambana na utapiamlo na madhara yatokanayo na utapiamlo.

Dkt. Nyagawa amesema kwa sasa wanafarijika kuona sasa Mashine hizi zitaweza kupatikana nchini tena chini ya Taasisi ya Serikali hivyo zoezi la ugawaji wa mashine hizi utakuwa endelevu wakati wowote zikihitajika  na kuna uwezekano Tanzania ikavuka asilimia 61 ya kaya zinazotumia chumvi yenye madini joto toshelevu endapo zitatumika kikamilifu.

Akizungumza kwa niaba ya Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Katibu Mkuu Prof. Riziki Shemdoe ameipongeza VETA kwa kuanza kutengeza mashine hizo kwa gharama nafuu tofauti na zingeagizwa toka nje ya nchi na amewaagiza makatibu tawala wa mikoa itakayopewa mashine hizo kuhakikisha  wanazitumia ipasavyo na siyo kwenda na kuzifungia stoo.

Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Caroly Nombo amesema kutengenezwa kwa mashine hizo na Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) imejidhihisha kuwa sasa wahitimu na wanafunzi wa vyuo hivyo vilivyopo nchi nzima sasa wameanza  kutatua changamoto zinazoikabili jamii na wanaweza kutengeneza vitu amavyo vitapatikana kwa gharama nafuu na kuokoa gharama za fedha za serikali endapo bidhaa hizo zitaagizwa nje ya nchi.

Tanzania ina zaidi ya wazalisha wadogo wa Chumvi 7000 wanaotumia teknolojia duni za kuzalisha chumvi na wametawanyika katika maeneo mbalimbali  ambayo hayafikiki kwa urahisi hivyo ujio wa mashine hizi utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza kiwango cha nguvu kinachozalishwa nchini bila kuweka madini chumvi ya kutosha.

No comments:

Post a Comment