Mfanyabiashara na mdau wa Utalii Duniani Nicholas Reynolds ‘ Bongozozo’. |
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amemshukuru Mfanyabiashara na mdau wa Utalii Duniani Nicholas Reynolds ‘ Bongozozo’ kwa juhudi zake za kuendeleza michezo pamoja na kutangaza Utalii wa Zanzibar.
Dk. Mwinyi ametoa shukrani hizo wakati alipozungumza na mwanamichezo na Mdau huyo wa Utalii Ikulu Jijini Zanzibar, ambapo pamoja na mambo mengine amefika kwa ajili ya kujitambulisha.
Alisema juhudi zinazofanywa na mdau huyo katika kuimarisha shughuli za michezo hapa nchini pamoja na kutangaza Utalii, ni jambo jema kwa kuzingatia kuwa Serikali haiwezi kufanya kila kitu.
Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kumuomba Mdau huyo kuwa Balozi wa Utalii Zanzibar, ili kuitangaza zaidi kiutalii ndani na nje ya Tanzania.
Aidha, aliwashukuru wadau mbali mbali wanaoshirikiana na mdau kwa kumshawishi na kuzuru Zanzibar, hatua iliomuwezesha kuandaa mashindano maalum ya soka kisiwani Pemba.
Naye, Mfanyabiashara na Mdau huyo wa Utalii Duniani Nicholas Reynolds alimshukuru Rais Dk. Mwinyi na kusema ziara yake inalenga kuunga mkono juhudi za Rais Dk. Mwinyi katika kuileta maendeleo Zanzibar kupitia sekta mbali mbali, ikiwemo ya michezo pamoja na Utalii.
No comments:
Post a Comment