NHC TBA ACHENI KUDEMADEMA UJENZI JENGO LA WUSM - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday, 24 February 2022

NHC TBA ACHENI KUDEMADEMA UJENZI JENGO LA WUSM

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ndugu Saidi Othuman Yakubu.

Na Adeladius Makwega - WUSM

NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ndugu Saidi Othuman Yakubu  Februari 24, 2022 amesema kuwa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Mkandarasi Mjenzi na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Mkandarasi Mshauri waache kudemadema kukamilisha ujenzi wa jengo la wizara hiyo.

“Nasema mnawajibu kwa kutimiza majukumu yenu ipasavyo Ili kukamilisha ujenzi wa jengo hili kwa wakati kwani Rais Samia Suluhu Hassan ametoa pesa za ujenzi kwa Wizara zote kwa wakati mmoja iweje jengo la wizara yetu mtucheleweshe?” Aliuliza.

Akizungumza kwa msisitizo Naibu Katibu Mkuu Yakubu, alisema kuwa anafuatilia kwa ukaribu mno ujenzi wa jengo hilo kuliko hata NHC na TBA wanavyodhani.

“Hapa hakuna utani, lazima mtawajibika kwa kufanya kazi hii kwa uzembe, kwani nimekuwa nikifika hapa kila asubuhi nawakuta wafanyakazi wawili au watatu, huku hata wakati wa kazi watumishi ni wachache mno, ongezeni wafanyakazi na nyie wenyewe mnatambua kuwa mpo nje ya muda.” Alisisitiza.

Naibu katibu Mkuu Yakubu alisema kuwa lazima kwa hali hii NHC na TBA mtawajibika msipojirekebisha.

Aliongeza kuwa kwa hali ya ujenzi inavyoendelea Mkandarasa Mshauri (TBA) kama angekuwa anatimiza majukumu yake ipasavyo, hali hii isingaliweza kutokea, kwa hiyo  hiyo Mkandarasi Mshauri anapaswa kutimiza wajibu wake ipasavyo na pia kwa Mkandarasi Mjenzi.

Naibu Katibu Mkuu Yakubu aliongeza kuwa utendaji wa kazi wa NHC na TBA ni kipimo tosha kwa kazi za mbeleni za Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo zikiwamo ujenzi wa viwanja.

Kwa pamoja TBA na NHC kwa wale watendaji walikuwepo katika eneo la ujenzi walisema kuwa watajitahidi kutekeza majukumu yao kwa wakati na wameyapokea maelezo ya Naibu Katibu Mkuu Yakubu.


No comments:

Post a Comment