Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Mhandisi Kundo Mathew akisaini kitabu ofisini kwa Waziri wake Mhe. Nape Nnauye mara baada ya kuwasili Wizarani hapo. |
WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye amewasili katika Ofisi za Wizara hiyo zilizopo katika Mji wa Serikali Mtumba na kupokelewa na Menejimenti na watumishi wa Wizara hiyo wakiongozwa Naibu Waziri wake Mhandisi Kundo Mathew na Katibu Mkuu Dkt. Jim Yonazi mara baada ya kuapishwa Ikulu ya Chamwino Januari 10, 2022 baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mhe. Samia Suluhu Hassan kufanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri na watendaji wakuu Wizara katika ngazi ya Makatibu Wakuu na Manaibu Katibu Wakuu.
Mhe. Nape amezungumza na watumishi wa Wizara hiyo na kuwataka kufanya kazi kwa bidii, weledi na utulivu ili kuwezesha Sekta mbalimbali kupitia huduma za mawasiliano na TEHAMA pasipo urasimu na hatimaye nchi izidi kusonga mbele na Wizara yake iwe ni Wizara ya mfano katika kusukuma gurudumu la maendeleo ya nchi.
Ameongeza kuwa Mhe. Rais Samia amewapeleka katika Wizara hiyo kwa ajili ya kufanya kazi kwa kushirikiana na wataalamu wa Wizara hiyo kwa matokeo chanya na yeye yupo tayari kulinda haki za watumishi wa Wizara hiyo huku akiwasisitiza kufanya kazi kwa bidii na kutimiza wajibu
“Safari niliyopita imenifundisha kutambua haki za watu na kuwa mnyenyekevu, nitasifiwa nimefanya vizuri kama nyie mtafanya vizuri, na itakuwa hivyo kama mazingira yenu ya kazi yakiwa mazuri na kutimiza wajibu wenu kwa kiwango kinachohitajika”, Amezungumza Mhe. Nape
Naye Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Mhandisi Kundo Mathew amesema kuwa viongozi waliopita walifanya kazi kubwa na kuifikisha Wizara mahali ilipo sasa na ana imani kubwa Wizara hiyo itaendelea kusonga mbele katika kuboresha, kuwezesha na kusimamia Sekta ya Habari, Mawasiliano na TEHAMA chini ya uongozi wa Waziri wake Mhe. Nape Nnauye, Katibu Mkuu Dkt. Jim Yonazi na Naibu Katibu Mkuu Mohammed Khamis.
Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Jim Yonazi amesema kuwa siku ya leo mara baada ya uapisho Viongozi wa Wizara hiyo wamekutana na Menejimenti na baadhi ya watumishi kwa lengo la kusalimiana na kufahamiana huku kikao rasmi cha Waziri huyo na watumishi wa Wizara kitaandaliwa na kufanyika kwa kadri itavyoonekana inafaa
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mohammed Khamis amesema kuwa anamshukuru sana Mhe. Rais kwa kumteua na kumpatia fursa ya kuitumikia nchi yake kwa taaluma aliyosomea na kuahidi kuitendea haki.
Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imefanyiwa mabadiliko ya uongozi katika ngazi ya Waziri ambapo Mhe. Nape Nnauye ameteuliwa na kuapishwa kuongoza Wizara hiyo, Katibu Mkuu Dkt. Jim Yonazi ambaye awali alihudumu katika cheo cha Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo na Naibu Katibu Mkuu Mohammed Khamis aliyeteuliwa na kuapishwa kuongoza Wizara hiyo huku Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhandisi Kundo Mathew ameteuliwa tena kuendelea katika nafasi hiyo.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
No comments:
Post a Comment