Na Dotto Mwaibale, Singida
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Mandewa mkoani Singida kupitia kamati ya siasa ya kata hiyo wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa Sh. 600 Milioni kwa ajili ya kujenga Kituo cha Afya eneo la Mtaa wa Mwaja katika kata hiyo.
Kukamilika kwa ujenzi wa kituo hicho cha afya wananchi wa eneo hilo hasa wajawazito wataondokana na adha ya kutembea umbali mrefu wa kwenda kupata huduma za afya Hospitali ya Sokoine iliyopo mjini hapa.
Akizungumza wakati wa ziara iliyofanywa na kamati hiyo ya kukagua ujenzi wa kituo hicho cha afya juzi Mwenyekiti wa CCM wa kata hiyo Hamisi Ireme alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwakumbuka wananchi wa eneo hilo na kuwapa kiasi hicho cha fedha za ujenzi.
Akizungumzia soko hilo jipya la Samaki Samaki lililopo Unyankhaye ambalo linatumiwa na wafanya biasha ndogo ndogo walioondolewa kwenye maeneo yasio rasmi kwa agizo la Serikali Ireme alitumia nafasi hiyo kuwahasa maafisa wa Serikali kushirikiana na viongozi wa Serikali za mitaa na madiwani kwenye kata zao ili kuondoa migongano isiyo ya lazima wakati wa kutekeleza shughuli mbalimbali za kimaendeleo.
"Kwa nafasi ya kipekee nimshukuru Mbunge wa Jimbo la Singida Mjini Mussa Sima kwa kutoa fedha za mfuko wa jimbo ambazo zinasaidia kuchonga barabara katika viwanja vilivyopimwa jambo litakalosaidia kuleta maendeleo kwenye kata yetu" alisema Ireme.
Diwani wa Kata ya Mandewa Baraka Hamisi akizungumzia ziara hiyo alisema imeleta hamasa na kama Serikali wamekuwa na mambo wanayoyafanya hasa pale zinapoibuka changamoto mbalimbali huwa wanatafuta sehemu ya kuzipeleka ambapo ni kwenye chama.
Alisema katika Soko la Samaki Samaki wamebaini changamoto za watu kutoka nje ya kata hiyo kupewa maeneo ya kujenga vibanda na kuondoka na hali hiyo ilitokana na viongozi wa eneo hilo kutoshirikishwa jambo ambalo limechangia kwa wafanyabiashara waliowengi kutotumia eneo hilo na kurudi kwenye maeneo yao ya awali.
"Suala la wafanyabiashara hao kutengewa maeneo rasmi ni agizo la Rais lakini tumeshindwa kuwarudisha kwa kuwa mchakato mzima wa kuwahamishia katika soko hilo hatukushirikishwa lakini kwa kuwa lipo ndani ya uwezo wetu tutalifanyia kazi" alisema Hamisi.
Katibu wa CCM wa kata hiyo Yusuph Kijanga Makera aliushukuru uongozi wa CCM kuanzia ngazi ya wilaya, mkoa na ngazi ya Taifa chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa walioifanya ya kuwapatia mradi mkubwa ambapo wanapokea pongezi nyingi kutoka kwa wananchi hasa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan anavyoitekeleza ilani ya CCM.
Alisema katika Soko la Samaki Samaki wameona changamoto nyingi za kutokuwepo kwa vyoo, maji,umeme, guba la takataka na baadhi ya watu kutoka nje ya eneo hilo kupewa vibanda ambapo wajasiriamali wa eneo hilo wameomba kufanyike uhakiki mpya ili waweze kutambuliwa.
Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Mwaja Subira Mukhenyi aliishukuru Serikali kwa kuwajengea kituo hicho kwani kukamilika kwake kitatoa msaada mkubwa wa matibabu hasa kwa wajawazito.
No comments:
Post a Comment