Mtaalam wa masuala ya barabara toka Bodi ya Mfuko wa Barabara nchini (RFB), Eng. Rashid Kalimbaga akisaini mkataba wa ushirikiano katika kuhakikisha usalama wa barabarani unazingatiwa. |
SERIKALI imewataka wadau wote wa miundombinu ya barabara kushirikiana ili kuhakikisha barabara zote nchini zinakuwa salama kwa kwa watumiaji wote na wakati wote.
Hayo yamesemwa na Mkuu
wa Wilaya ya Kinondoni, Bw. Saad Mtambule alipokuwa akimwakilisha Waziri wa
Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa katika hafla ya kufunga mradi wa
majaribio wa mpango wa hatua kumi (Ten
step plan), wa miundombinu ya barabara salama nchini Tanzania.
Mpango huo
uliotekelezwa kwa miezi 30 kwa kudhaminiwa na Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa
Usalama Barabarani na Benki ya Dunia unalenga kuzipa hadhi barabara nchini
kutoka nyota moja hadi tano kutokana na uwezo wake wa kutosababisha ajali na
hivyo kulinda maisha na mali kwa watumiaji wa barabara.
“…Serikali inathamini
jitihada za wadau wote wa barabara ikiwemo Benki ya Dunia, Shirikisho la
Barabara la Kimataifa (IRF), Mpango wa Kimataifa wa Tathmini ya Barabara (iRAP)
na Chama cha Wadau wa Barabara nchini Tanzania (TARA) kwa kuiwezesha Tanzania
kuwa nchini ya kwanza duniani kutekeleza mradi huo wa majaribio ya barabara
salama ,” amesema DC Mtambule.
Naye Mkurugenzi wa
Barabara wa wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Eng. Alois Matei amesema Wizara kwa
kushirikiana na wadau wake imejipanga kuhakikisha barabara zinazojengwa
zinakuwa na alama zote za usalama barabarani na zinatenganisha maeneo ya
watembea kwa miguu, waendesha baiskeli na magari ili kupunguza ajali.
Amebainisha kuwa Serikali inaendelea kuboresha bajeti zake kila mwaka ili katika ujenzi wa barabara mpya usanifu wake uzingatie viwango vyote vya usalama barabarani na kuondoa vikwazo kwenye maeneo yanayosababisha ajali mara kwa mara.
Zaidi ya watu milioni
moja na laki nne wanahofiwa kuwa hupoteza maisha kila mwaka duniani kutokana na
ajali za barabarani zinazosababishwa pamoja na mambo mengine uwepo wa barabara
zisizo salama.
No comments:
Post a Comment