MCHEZA KAYAMBA CHAMWINO IKULU - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 10 January 2022

MCHEZA KAYAMBA CHAMWINO IKULU

 

Kwaya iliyoimba mwaka 1964.

Kanisa la Parokia ya Bikira Maria Imakulata Chamwino Ikulu.

Na Adeladius Makwega, Chamwino

JUMAPILI ya Januari 9, 2022 niliamka nyumbani kwangu saa 11. 48 ya asubuhi na kujiandaa haraka haraka kuelekea ibadani Kanisani Parokia ya Bikira Maria Imakulata Chamwino Ikulu. Nilianza safari hiyo haraka haraka nikiwa njiani nilikutana na ndugu mmoja akiwa na boda boda yake.

Ndugu huyu alinipita, alafu akaniuliza mkubwa unaenda kanisani? Nikamjibu ndiyo, akasema twenda mkubwa. Nilijiuliza maswali kadhaa, kwanza bure ni ghali, lakini pia ilikuja hoja juu ya watu wasiojulikana. Kwa sekunde 20 nilipata jibu juu ya watu wasiojulikana, kwa kuwa mimi amenibeba nyuma yake ni vigumu mno ndugu huyo kunifanyia ubaya, labda awe na mwezake.

Kwa hakika nilikuwa na silaha tatu; kwanza mwili wangu mwenyewe, pili silaha ya kiroho na tatu silaha nyingine. Kwa hiyo niliipanda bodaboda kwa kujiamini lakini nikibakia na hoja ya bure aghali.

Ndugu huyu kweli alikuwa akienda kanisani na tukiwa njiani tulibaini kuwa tulikuwa tumechelewa kama dakika 17 tangu ibada ianze, maana muda huo ilikuwa ni 12.17 asubuhi. Tulipofika kanisani nilishuka na kumshukuru sana ndugu huyu, kwani alikuwa mtu mwema tu, kwa mtazamo wa nje. Kwa hiyo zile silaha zangu tatu ziliendelea kuwa kibindoni.

”Unaweza kuulizwa na Bwana Yesu, eh mbona mimi nilikuja kwa njia jamaa wa bodaboda, mbona ulinikataa?”

Nilijisemea moyoni juu swali hilo la Bwana Yesu, kuwa suala la watu wasiojulikana linaweza kutufanya wengi kuchuma dhambi. Watu wasiojulikana nawao watambue kuwa kesho kuna moto. Kwa maana siku hizi tunaogopana wenyewe kwa wenyewe.

Nilifika kanisani wakati wa Utukufu kwa Mungu inaimbwa. Niliingia haraka haraka nikasema kama jamaa huyu asingalinibeba, nisingafika wahi Injili. Hatua zote za ibada hii zilifanyika vizuri sana huku idadi ya waumini kidogo ikiwa kubwa siku hii. Mara baada ya walei kupokea ilikuwa wasaa wa sadaka ya pili ambapo vikapu vya sadaka viliwekwa vizuri na watu kwenda kutoa sadaka hiyo.

Binafsi sadaka ya pili sikuitoa kwa kuwa sadaka yangu yote nilitoa katika sadaka ya awali, wakati wenzangu wanaamka kutoa sadaka mimi niliendelea kuketi katika benchi hili ambalo lilikuwa la mwisho kabisa, lililokuwa na watu kama watano hivi.

Wanakwaya walisimama, waliimba wimbo wa Mbali Kule. Hapa mwanakwetu! mimi nilikuwa nimekaa nyuma nawaona vizuri tangu sauti ya kwanza, ya pili, ya tatu, ya nne na wapiga ala za muziki.

“Je hamjui  jambo kuu la kuzaliwa Mwokozi…” Wanakwaya hao waliendelea kuimba.

Wanakwaya walichangamka mno, wakijitahidi kuimba vizuri na kuipamba ibada hii ya dominika. Sauti zao tamu zilisindikizwa na kinada, ngoma, kayamba na vifaa vingine vya asili ya ngoma na muziki wa kiafrika.

Walei waliendelea kutoa sadaka, huku mimi nikiwangalia wanakwaya wa kanisa hili, mwanakwetu! Mimi nilivutiwa mno na jamaa mmoja ambaye alikuwa akicheza kayamba na akiuchezesha mwili wake uliokuwa ukiendana fika na midundo, mapigo ya ngoma, sauti za waimbaji na ala zingine za muziki. 

Mpiga kayamba huyu alisababisha na mimi kuvuta kukumbuka ya historia ya kutumika ala la muziki wa mwafrika kanisani. Kwanza kabisa nilikumbuka kuwa, ngoma, kayamba, filimbi na ala zingine za muziki zinatumika katika ngoma za asili za mwafrika. Kutumika kwa ala hizo za muziki katika Kanisa Katoliki kunahusishwa na Watakatifu 22 ambao wanafahamika kama mashahidi wa Uganda ambalo ni kundi la watakatifu 45 huku 22 Wakatoliki na 23 Waangilikana waliouwawa na Mfalme wa Buganda, Daniel Kabaka Mwanga II kati ya Januari 31, 1885 na Januari 27, 1887.

Mpaka Januari 31, 2022 itakuwa inakaribia miaka 137. Ikiaminika kuwa mmoja wa Watakatifu hao alikuwa ni mzaliwa wa Mtanzania.

Mchakato wa Kanisa katoliki kuwatangaza kuwa watakatifu ndugu zetu hao ulikamilika Oktoba 18,1964 Ikiwa ni siku kubwa ya kukumbukwa barani Afrika na Duniani ambapo Kanisa Katoliki chini Baba Mtakatifu Paulo VI alipowatangaza Waafrika 22 kuwa Watakatifu katika Kanisa la Mtakatifu Peter Basilika Vatikani. Ibada ya kuwatangaza watakatifu hao ilitanguliwa na Mtaguso wa Pili wa Vatikani. Baadhi ya mambo yaliyoamuliwa ilikuwa ni kanisa hilo kuanza kuendesha ibada zake kwa kutumia lugha za asili pale kanisa lilipo, huku awali kilitumika Kilatini.

Niliendelea kukumbuka kuwa Iliamuliwa hata ibada ya kuwatangaza watakatifu hao 22, kwaya yake kuimba kwa lugha walizokuwa wakitumia Watakatifu hao. Kazi ya kutunga nyimbo alikabidhiwa mtunzi wa nyimbo wa Uganda Joseph Kyagambiddwa.

Kyagambiddwa alitunga nyimbo 22 ambapo zilikuwa zikielezea tukio hilo hadi la kuwatangaza ndugu hao kuwa Watakatifu. Kutokana na gharama kubwa ya kuwasafirisha wanakwaya wanaotambua lugha hizo kutoka Uganda, iliamuliwa kuwakusanya vijana wa kiafrika wakike kwa wakiume na kuwaweka pamoja, kuwafundisha nyimbo hizo mpya zilizotungwa na ndugu huyu. Walikusanywa wanafunzi waliokuwa huko Ughaibuni kama vile Ujerumani, Uswizi an Italia.

Nakukumbusha kuwa bado nilikuwa kanisani na sadaka inatolewa na wanakwaya hawa wanaimba.

“..Glooooolia Glooolia Glooooliaa…”

Maamuzi hayo ya kuwafundisha wanafunzi waliopo Ughaibuni yalifanywa na Askofu Mkuu Joseph Kiwanuka wa Jimbo la Rubaga Uganda ndipo vijana hao walikusanywa katika makundi matatu katika mataifa hayo niliyokutajia.

“Tulikusanywa kutika mataifa matatu ya ulaya na wengine walitoka Nijeria na mataifa mengine ya Afrika ambapo walikuwa vyuo vikuu vya Ulaya, ilikuwa ngumu kuwapata wanafunzi wa Uganda pekee.” Haya yalikuwa maneno yaliyosemwa na Bi Justine Nakiganda alikuwa miongoni mwa wanakwaya hao.

Ilipofika Oktoba 18, 1964 Ndugu Kyagambiddwa akiwa mwalimu na mwongozaji wa kwaya hii katika mimbari ya Kanisa la Mtakatifu Peter Basilika aliwaongoza wanakwaya wenye asili ya Afrika kuipamba ibada ya kutangazwa watakatifu hao 22.

“Ndipo ilikuwa siku ya kwanza katika ulimwengu wa Kanisa Katoliki, kwanza kwaya kutoka Afrika ilipoimba kwa lugha za Kiafrika, Pili ilikuwa siku ya kwanza kutumia vifaa vya asili kuimbia kwaya katika kanisani hilo na tatu ilikuwa ni siku ya kwanza wanawake walipoimba kwaya katika kanisa hilo.” Niliyakumbuka maneno Bi Justine Nakiganda.

Teddy Nampeera ambaye pia alikuwepo miongoni mwa wanakwaya hao alisema kuwa siku hiyo ilikuwa ni ya fahari na nzuri sana kwao, huku watu wakiwauliza je mnatokea Afrika ya Mashariki? Mnatoke Uganda eh?, walijibu ndiyo huku wakifaya ishara ya msalaba.

Kulingana na hesabu zangu nifikrilia kuwa kuwa ikifika Oktoba 18, 2024 itakuwa ni miaka 60 tangu kanisa katoliki lianze kutumia ala za asili kuimba kwaya kanisani, miaka 60 tangu kuanza kutumia lugha za asili kusalia kanisani, Pia miaka 60 tangu hata wanawake kuanza kuimba kwanya kanisani. 

Gafla niliona kimya, nikashituka natafakari yangu, nikasema ohh kumbe nipo kanisani na ibada haijaisha. Yakasomwa matangazo, Padri wetu akasema nendeni na Amani na mie nikarudi kwangu madongo poromoka.

makwadeladius@gmail.com

0717649257


No comments:

Post a Comment