WAZIRI KITILA AIPONGEZA BENKI YA CRDB KWA KUPELEKA WAFANYABIASHARA UTURUKI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday, 19 October 2021

WAZIRI KITILA AIPONGEZA BENKI YA CRDB KWA KUPELEKA WAFANYABIASHARA UTURUKI

Waziri wa Viwanda na Biashara, Prof. Kitila Mkumbo (katikati) akimkabidhi Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Strecth Fabric Tanzania, Samia Mangalili, pasi ya kusafiria pamoja na tiketi ikiwa ni ishara ya kuwatakia safari njema kundi la wafanyabiashara zaidi ya 100 wanaotarajiwa kwenda nchini Uturuki kushiriki Kongamano la Afrika la Uchumi na Biashara 2021 (Turkey - Africa Economic and Business Forum), hafla hiyo imefanyika jana kwenye hoteli ya Serena jijini Dar es salaam. Wengine pichani ni Mkurugenzi wa Wateja Wadogo na wa kati wa Benki ya CRDB, Boma Raballa (wa pili kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya uwakala wa safari ya Go Extra Mile Safaris, Diana Gasper (kushoto) pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Biashara wa Benki ya CRDB, Toyi Ruvumbagu (wa pili kulia).

Waziri wa Viwanda na Biashara, Prof. Kitila Mkumbo (katikati) akimkabidhi Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Shayakye TRD, Shakiru Yahya pasi ya kusafiria pamoja na tiketi ikiwa ni ishara ya kuwatakia safari njema kundi la wafanyabiashara zaidi ya 100 wanaotarajiwa kwenda nchini Uturuki kushiriki Kongamano la Afrika la Uchumi na Biashara 2021 (Turkey - Africa Economic and Business Forum), hafla hiyo imefanyika jana kwenye hoteli ya Serena jijini Dar es salaam. Wengine pichani ni Mkurugenzi wa Wateja Wadogo na wa kati wa Benki ya CRDB, Boma Raballa (kushoto), pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Biashara wa Benki ya CRDB, Toyi Ruvumbagu.
 

 
WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo ameipongeza Benki ya CRDB kwa kushirikiana na kampuni ya Go Extra Miles Safaris kwa kuwezesha wafanyabiashara wa Tanzania kuhudhuria kongamano la biashara na uchumi baina ya nchi ya Uturuki na Bara la Afrika likalofanyika jijini Instanbul nchini Uturuki. Waziri Kitila ametoa pongezi hizo katika hafla ya kuwaaga wafanyabiashara hao iliyofanyika katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.

 
Akizungumza na wafanyabiashara hao Waziri Kitila amewasihi kutumia fursa hiyo vizuri kujifunza kwa wafanyabiashara wenzao ambao wamepiga hatua kubwa katika biashara zao huku akisisitiza kuwa ni vyema wafanyabiashara hao wakaenda wakiwa na malengo makhususi ambayo wangependa kuyafanikisha wakiwa huko.

"Ni matumaini yangu kuwa mtatumia fursa hii vizuri kujifunza na kutengeneza mtandao ili mtakaporudi nchini muweze kuongeza tija katika biashara zenu jambo ambalo pia litaongeza tija kwa nchi yetu kwani mnapofanya vizuri pia Serikali inanufaika kupitia makusanyo ya kodi" alisema Waziri Kitila.

 
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Wateja Wadogo na Kati wa Benki ya CRDB, Boma Raballa alisema kuwa Benki ya CRDB imeendelea kuonyesha utayari wake katika kusaidia sekta ya viwanda na biashara na safari hii ina manufaa makubwa kwa wafanyabiashara na nchi kwa ujumla.

"Pamoja na kuendelea kuimarisha uhusiano wa kibiashara kati ya nchi zetu mbili, safari hii ina manufaa makubwa kwa wafanyabiashara wetu ambao pamoja na kuhudhuria kongamano la biashara pia watapata fursa ya kutembelea viwanda mbalimbali nchini Uturuki na kujifunza uzalishaji wa bidhaa mbalimbali" alisisitiza Boma.

Mkurugenzi huyo wa Benki ya CRDB alisema kuwa wao kama benki wametoa mkopo wenye masharti nafuu na rafiki kwa wafanyabiashara hao ili kuwawezesha kushiriki katika safari hiyo bila kuathiri mzunguko wa fedha zao za biashara.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya uwakala wa safari ya Go Extra Mile Safaris, Diana Gasper ameishukuru Benki ya CRDB kwa kushirikiana nao katika kuandaa safari hiyo ambayo ni muhimu kwa wafanyabiashara wa Tanzania. 
 
"Tunawashukuru sana Benki ya CRDB kwa kushirikiana nasi katika kuandaa safari kwa wafanyabiashara wetu wa Kitanzania ambao wanahitaji sana fursa kama hizi ili kujifunza na kutanua fursa za kimasoko nje ya mipaka ya nchi yetu" alisema Diana. 
 
Safari hiyo itahusisha wafanyabiashara zaidi ya 100 na inatarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 19 hadi 27 Oktoba ambapo wafanyabiashara hao wataambatana na Waziri mwenye dhamana ya viwanda na biashara, Profesa Kitila Mkumbo na maafisa waandamizi kutoka Benki ya CRDB na Go Extra Mile Safaris.







No comments:

Post a Comment