KATIKATI MKUU WA MKOA WA RUVUMA AKIZUNGUMZA MARA BAADA YA KUKAGUA UKARABATI WA UWANJA WA NDEGE WA SONGEA AMBAPO SERIKALI IMETOA SHILINGI BILIONI 37.09 KUTEKELEZA MRADI HUO. |
MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akiwa ameongozana na Kamati ya Ulinzi na Usalama, amekagua mradi wa ukarabati wa kiwanja cha ndege cha Songea ambacho serikali imetoa shilingi bilioni 37.09 kutekeleza mradi huo.
Akizungumza mara baada ya kukagua mradi huo,Mkuu wa Mkoa ameishukuru serikali ya Awamu ya sita kwa kuhakikisha kuwa Tanzania na Mkoa wa Ruvuma unaendelea kufunguka katika Nyanja mbalimbali za usafiri ukiwemo usafiri wa anga.
“Leo nimefika hapa katika uwanja wa ndege wa Songea kukagua kazi ambazo zimekuwa zinaendelea za kukarabati uwanja huu,ikiwemo kuurefusha uwanja na miumbombinu ambayo sasa imewezesha kuongeza ratiba ya safari za ndege kutoka mara mbili kwa wiki hadi mara tatu kuanzia mwezi ujao’’,alisema RC Ibuge.
Brigedia Jenerali Ibuge ametoa rai kwa wananchi mkoani Ruvuma ,mikoa jirani na Nyanda za Juu Kusini kuutumia uwanja wa ndege wa Songea ambao sasa upo tayari kutumika kusafiri kwa haraka ndani ya Tanzania na kuelekea maeneo mengine duniani.
Amesema kuanzia Novemba Mosi mwaka huu Shirika la Ndege Tanzania ATCL litaanza kutoa huduma za usafiri wa anga toka Dar es salaam hadi Songea mara tatu kwa wiki kwa siku za Jumatatu,Jumatano na Ijumaa na kwamba Mashirika mengine ya ndege tayari yamepanga kuanza kuutumia uwanja wa ndege wa Songea likiwemo Shirika la Auric Air.
Mkuu wa Mkoa anayakaribisha mashirika mengine ambayo yanaliona soko la usafiri wa anga la Kusini kupitia Songea wafike kwa sababu uwanja wa ndege upo salama na kwamba kiu ya wananchi wa Ruvuma ni kuhakikisha kuwa biashara zinafanyika kwa haraka zaidi ndani na nje ya nchi kupitia usafiri wa anga.
Hata hivyo Brigedia Jenerali Ibuge amesema kufunguliwa kwa uwanja wa ndege wa Songea,kuna fungua fursa za uwekezaji na utalii,kwa sababu Mkoa una vivutio vya kila aina likiwemo ziwa Nyasa,Hifadhi ya Taifa ya Nyerere,Mto Ruvuma,milima ya Livingstone na maeneo mengi yenye utalii wa kihistoria na kiutamaduni.
Kwa upande wake Meneja wa Ndege wa Songea Jordan Mchame amesema mara baada ya serikali kukarabati kiwanja cha ndege,idadi ya abiria inazidi kuongezeka ambapo ndege ya Bombadier yenye uwezo wa kubeba abiari 76 hivi sasa inabeba abiria kati ya 65 hadi 74.
“Hali hiyo inaonesha kwamba kuna abiria wengi wanaosafiri kwa ndege kwa kutumia uwanja wa ndege wa Songea,usafiri wa anga ni wa haraka na salama kuliko aina nyingine zote za usafiri,kadri idadi ya abiria inavyoongezeka tunatarajia hata gharama za nauli zitapungua’’,alisisitiza Mchami.
Hata hivyo amesema kabla ya ATCL kuanza kutoa huduma,nauli ya ndege binafsi kutoka Songea hadi Dar es salaam kwenda pekee ilikuwa kati ya shilingi 500,000 hadi 600,000 ambapo hivi sasa kupitia ATCL nauli kwenda ni shilingi 250,000 ,ambapo kwenda na kurudi ni shilingi 375,000 tu.
Naye Meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Lazack Alinanuswe akizungumzia mradi wa ujenzi wa uwanja huo,unaogharimu bilioni 37.09,amezitaja baadhi ya kazi ambazo zimekamilika kuwa ni barabara ya kurukia na kutua ndege na kwamba kilichobakia ni mnara na taa za kuongozea ndege ambavyo vinaendelea kukamilishwa.
Kiwanja cha ndege wa Songea ni miongoni mwa viwanja bora vya ndege Tanzania ambacho kilijengwa kati ya mwaka 1974 hadi 1980 na kiliwekewa lami hivyo kuwa na uwezo wa kutua ndege majira yote masika na kiangazi.
No comments:
Post a Comment