VIJANA WASHAURIWA KUTUMIA TEHAMA KWA MAENDELEO KIUCHUMI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Saturday, 16 October 2021

VIJANA WASHAURIWA KUTUMIA TEHAMA KWA MAENDELEO KIUCHUMI

 

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania, Bw. Waziri Kindamba (kushoto) alisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Bi. Sofia Mjema wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Vijana, Kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru na Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere yaliyofanyika katika Viwanja vya Magufuli Wilaya ya Chato mkoani Geita. Katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi.


Vijana wa halaiki wakitoa burudani katika hafla ya maadhimisho ya Wiki ya Vijana, Kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru na Kumbukumbu ya kifo cha Mwalimu J.K. Nyerere.


Vijana wa halaiki wakitoa burudani katika hafla ya maadhimisho ya Wiki ya Vijana, Kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru na Kumbukumbu ya kifo cha Mwalimu J.K. Nyerere.


Baadhi ya Viongozi wa Chama na Serikali wakifuatilia shughuli za Maadhimisho ya Wiki ya Vijana, Kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru na Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere yaliyofanyika katika Viwanja vya Magufuli Wilaya ya Chato mkoani Geita.


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwanyooshea mikono baadhi ya Washiriki wa Maadhimisho ya Wiki ya Vijana, Kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru na Kumbukumbu ya kifo cha Mwalimu Nyerere yaliyofanyika katika Viwanja vya Magufuli Wilaya ya Chato mkoani Geita.


Viongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru wakiwa katika maadhimisho hayo.

Na Mwandishi Wetu

VIJANA nchini Tanzania wameshauriwa kuitumia TEHAMA kwa malengo yaliyokusudiwa ili iweze kuwasaidia kupiga hatua katika kujijenga kiuchumi.

Ushauri huo umetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano, Bw. Waziri Kindamba wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Vijana, Kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru na kumbukumbu ya Baba wa Taifa iliyofanyika katika Viwanja vya Magufuli Wilaya ya Chato mkoani Geita.

Bw. Kindamba alisema watumiaji wa TEHAMA hususani vijana wanapaswa kuwa waangalifu na matumizi ya kimtandao ili kujiepusha na madhara yatokanayo na matumizi mabaya ya mitandao hiyo, na badala yake kuhakikisha inawasaidia kutatua changamoto zao kiuchumi.

Alisema matumizi mazuri ya TEHAMA yana mchango mkubwa kwa vijana katika kupata fursa za kibiashara na masoko, ikiwemo kujenga mahusiano mazuri sehemu mbalimbali nje na ndani ya nchi hivyo kuwawezesha kupata mbinu za kujitengenezea kipato.

Aidha alisema kukua kwa TEHAMA kumerahisisha shughuli nyingi za kiuchumi, kijamii na kisiasa jambo ambalo linachochea kiasi kikubwa cha maendeleo katika nyanja tofauti tofauti na hapo awali.

Alisema mbali na hilo TEHAMA pia imerahisisha utendaji kazi katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta za afya, elimu, kilimo na kuongeza uwajibikaji; ambapo kwa sasa kwa kutumia mtandao ni rahisi bidhaa au huduma kuwafikia watu wengi zaidi na kupata mrejesho wa bidhaa husika kwa wakati.

Katika hatua nyingine, Bw. Kindamba aliwaasa vijana na watumiaji wa mitandao ya kijamii kujiepusha na matumizi ya lugha zisizo na staha, kusambaziana picha za utupu zenye lengo la kukashifu wengine na hata kutangaza biashara haramu ambayo ni kinyume na taratibu za nchi, 

"Niwashari vijana waachea kuitumia teknolojia hii kutukana viongozi, kufanya utapeli, na wakati mwingine hata kulidhalilisha Taifa kwa matendo mengine yote ambayo si ya kiungwana ambayo baadhi wanafanya," alisema Kindamba.

Mkoa wa Geita uliteuliwa kwa ajili ya Maadhimisho ya Kilele cha Mbio Maalum za Mwenge wa Uhuru 2021, shughuli ambazo zimefanyika katika Uwanja wa Magufuli – Halmashauri ya Wilaya ya Chato, zikienda sambamba na maadhimisho ya kumuenzi aliyekuwa Rais wa Tanzania, hayati Dk. John Pombe Magufuli na kumbukizi la taifa la Tanzania la kifo cha baba wa taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. 

Aidha, pia vijana walipata fursa za kuhudhuria maadhimisho ya wiki ya vijana iliyoanza Oktoba 8, 2021 ambapo walikutana na kuonyesha kazi na shughuli za ujasiriamali wanazozifanya, ili kuleta chachu kwa wengine.

No comments:

Post a Comment