TAMBIKO LA WARUGURU LAANZA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Saturday 16 October 2021

TAMBIKO LA WARUGURU LAANZA


NA ADELADIUS MAKWEGA, KINOLE

SHEREHE za kimila za tambiko la kabila la Waruguru zimeanza rasmi katika kijiji cha Kinole mkoani Morogoro huku wakazi mbalimbali wa mkoa huu na jamii ya kabila hilo kutoka katika maeneo mengine ya Tanzania na nchi ya nje wakijongea katika viunga vya makazi ya Chifu Kingalu Mwanabanzi 15 kutimiza mila yao.

 

Watu kadhaa walionekana wakipanda mlima kuelekea katika viunga hivyo katika eneo lililozungukwa na uoto wa asili unaopendeza huku kwa kando wakisindikizwa na milio ya chini chini ya sauti ya ndege wa mwituni na sauti za wadudu ambazo zinawasindikiza waendao huko mithili ya zeze.

 

Akizunguza katika shughuli za awali za tukio hilo Chifu Kingalu Mwanabanzi amesema kuwa shughuli hizi zina maana kubwa kwa kabila lao na Watanzania kwa ujumla kwani ndani yake makubwa mengi hufanyika.

 

“Iwe kwa taifa, mkoa na hata mtu mmoja mmoja hutamkwa kila anachokitaka na hutokea.”

Akizungumza katika viungo hivyo vya makazi ya chifu Kingalu, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Utamaduni wa Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo Dkt. Emmanuel Temu amesema kuwa wizara inashiriki katika sherehe hizo kwa kuwa matambiko yote ni sehemu ya urithi wa utamaduni wa Mtanzania kutoka vizazi na vizazi.

 

“Tupo na tutaendelea kuwepo iwe usiku au mchana mpaka tambiko likamilike kuheshimu mila za Waruguru na utamaduni wa Mtanzania.”

 

Mpaka sasa viongozi kadhaa kutoka maeneo mengine jirani wameshawasili akiwamo  Chifu Mulenge Talevalo wa II wa Tambiko la Ulilo Ulanga, Chifu Soliambingu II Kiwanga wa Utengule Morogoro na Mheshimiwa Dunia Waziri ambaye ni diwani wa viti maalumu wa tarafa ya Mkuyuni .

No comments:

Post a Comment