SERIKALI YATUMIA SH. BILIONI 52.975 KUTEKELEZA MIRADI MBALIMBALI SINGIDA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 27 September 2021

SERIKALI YATUMIA SH. BILIONI 52.975 KUTEKELEZA MIRADI MBALIMBALI SINGIDA

Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa akionesha Jarida la Nchi Yetu wakati akitoa taarifa ya wiki ya Serikali kwa waandishi wa habari mkoani Singida leo.

Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa akizungumza na waandishi wa habari wakati akitoa taarifa hiyo.

Taarifa ikitolewa.

Waandishi wa habari wakisikiliza taarifa hiyo.

Waandishi wa habari wakisikiliza taarifa hiyo. Kushoto ni Afisa Habari Msaidizi Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Mwanahabari Elisante Mkumbo akiuliza swali kwenye mkutano huo.

Mwanahabari Damiano Mkumbo akiuliza swali kwenye mkutano huo.

Mwanahabari  Edina Alex akiangalia   Jarida la Nchi Yetu kwenye mkutano huo. 

Waandishi wa habari wakiwa kwenye mkutano huo.

Mkutano ukiendelea.

Kazi ikiendelea,

Katibu Mwenezi na Itikadi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida Ahmed Kaburu akiuliza swali kwenye mkutano huo.

Na Dotto Mwaibale, Singida


SERIKALI imetoa Sh.Bilioni 52.975  mkoani Singida kwa ajili  ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo barabara, elimu, afya, maji, huduma za utawala na uwezeshaji wa wananchi. 

Hayo yamesemwa na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa wakati akitoa taarifa ya wiki ya Serikali kwa waandishi wa habari mkoani Singida jana.

Alisema Serikali inaendelea kutoa huduma za kiutawala na maendeleo katika Mkoa wa Singida kama kawaida chini ya Mkuu wa Mkoa Dkt. Binilith Mahenge na kuwa hali ya mkoa ni shwari na wananchi wanaendelea na shughuli zao za uzalishaji mali bila bughudha. 

Alisema katika kuimarisha ustawi wa wananchi wa Singida, Serikali inatekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kama ambavyo inafanya katika mikoa mingine hapa nchini na katika kufanikisha utekelezaji huo Serikali inahakikisha inatoa fedha kama ilivyopangwa. 

Msigwa alisema kuanzia Mwezi huu wa tisa, Serikali imeleta Sh. Bilioni 2 na Milioni 275 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Vituo vya Afya 8 (Ntuntu-Ikungi, Mitundu-Itigi, Chibungwa/Sasajila-Manyoni, Ilunda-Mkalama, Iglansoni-Ikungi, Tyegelo-Iramba, Kasisiri-Iramba na Makuro-Wilayani Singida) na kukamilisha vyumba vya madarasa 22 katika shule za Sekondari. Hizi ni fedha ambazo zinakusanywa kutokana na tozo katika miamala ya simu. 

Alisema kuna miradi mbalimbali ya ujenzi wa Barabara na Madaraja inayoendelea kutekelezwa na kati ya Machi na Septemba mwaka huu 2021, Serikali imeleta Singida shilingi Bilioni 21 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi na ukarabati wa barabara na madaraja. 

"Mfano mmoja wapo ni ujenzi wa Daraja la Msingi (lenye urefu wa mita 100) katika barabara ya Ulemo-Gumanga-Sibiti. Ujenzi wa daraja hili utagharimu Sh. Bilioni 10.933, hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 69. Daraja hili pamoja na barabara zake unganishi zitakamilika Juni 2022,".  alisema Msigwa.

Msigwa aliongeza kuwa pamoja na miradi hiyo Serikali imeanza  kufanya upembuzi yakinifu na usanifu kwa ajili ya maandalizi ya ujenzi wa barabara ya Sabasaba, Sepuka na Ndago Kizaga yenye km 77.6.

Alitaja barabara nyingine kuwa ni ya mchepuo ya Singida (Singida bypass) ya kilometa 46, Barabara ya Mkalama-Gumanga-Nduguti-Iguguno ambayo ni sehemu ya barabara inayoanzia Bariadi mkoani Simiyu ambayo itaunganisha na Iguguno. 

Akizungumzia miradi ya maji alisema Serikali imeleta sh. Bilioni 5 na Milioni 278 kutekeleza miradi hiyo katika vijiji vya Mughamo, Ibaga, Kipumbuiko na Kintinku/Lusilile. Hii yote nijuhudi za Rais Samia Suluhu Hassan za kumtua ndoo ya Maji Mama na kukabiliana na tatizo la maji. 

 Kuhusu umeme kupitia mradi wa usambazaji wa umeme vijijini (REA-III), Serikali imesambaza umeme katika vijiji 274 kati ya vijiji vyote 441 (sawa na asilimia 62.1). Kazi inayoendelea sasa ni kusambaza katika vijiji 167 vilivyobaki. Vijiji hivi vyote vitakuwa vimepata umeme ifikapo Desemba mwakani. 

Pia alisema Serikali inatekeleza mradi mkubwa wa umeme wa kitaifa unaitwa Backbone Transimission Investment Project (BTIP) na kuwa hapa Singida kuna kituo kikubwa cha kupooza umeme na kinapokea kutoka kituo cha Zuzu – Dodoma umeme wa msongo wa kilovoti 400. Uwezo wake wa juu ni kupokea, kupoooza na kusambaza jumla ya Megawati 600. Kwa sasa tayari kimeanza kuhudumia Mji wa Singida na kazi inayoendelea ni kuunganisha na mitambo ya msongo wa kilovoti 400 na ile ya kilovoti 220 ambayo inatumika kuwapelekea wananchi. 

Alisema mradi huo  ni sehemu ya mradi mkubwa wa kujenga njia kuu ya umeme kutoka Iringa, Dodoma, Singida hadi Shinyanga. Na pia ni sehemu ya mradi wa kuunganisha njia ya umeme kati ya Tanzania na Kenya. Njia hii inakwenda mpaka  Namanga – Arusha hadi kuunganisha na Isinya nchini Kenya. 

Alitaja Gharama za mradi huo kuwa ni  Dola za Marekani Milioni 56 (Bilioni 128.8), hadi sasa umefikia asilimia 99 na unatarajiwa kukamilika kabla ya Desemba mwaka huu 2021.

Akizungumzia mradi wa kimkakati wa kukabiliana na upungufu wa mafuta ya kula nchini alisema nchi yetu inahitaji kama tani 640,000 za mafuta ya kula, uzalishaji wetu ni tani 240,000 tu. Mafuta yanayobaki kiasi cha tani 400,000 tunalazimika kuagiza kutoka nje ya nchi na tunatumiza zaidi ya shilingi Bilioni 500 kuagiza mafuta hayo. 

Alisema Serikali imejipanga kuhakikisha inaleta mbegu za alizeti za kupanda tani 1,194 kwa ajili ya wakulima. Hizi ni mbegu bora ambazo zinatoa mafuta mengi. 

Alisema katika juhudi za kuongeza mbegu za alizeti kwa ajili ya kuzalisha mafuta, tunahitaji tani milioni 2 kwa mwaka lakini tunazalisha tani laki 6 tu. 

"Serikali inawapongeza viongozi na wakulima wa Mkoa wa Singida kwa kujiwekea mpango wa kulima ekari 597,000 na kuzalisha tani 581,986 ambazo zitazalisha tani 242,500 za mafuta. Hii itasaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya upungufu wa mafuta ya kula hapa nchini na kupanda kwa bei ya mafuta, alisema Msigwa.

 Msigwa alitumia nafasi hiyo kunatoa wito kwa wakulima wote nchini kuongeza uzalishaji wa alizeti na Serikali itaendelea kutoa huduma za ugani, kutafuta mbegu bora na kuhamasisha uwekezaji katika viwanda vya kusafisha mafuta. 

Adha Msigwa akizungumzia Mapambano dhidi ya Uviko-19 alisema  janga la ugonjwa  unaosababishwa na Virusi vya Korona (Uviko-19). Serikali kupitia Viongozi wake na Wataalamu imeendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya kujikinga na ugonjwa huo na kupokea chanjo. 

"Kwa kutambua changamoto ya kuhakikisha elimu dhidi ya ugonjwa huu inawafikia wananchi ipasavyo pamoja na kupata chanjo, Wiki hii Serikali imeanza kutekeleza Awamu ya Pili ya utoaji chanjo kwa kupanua uwigo wa vituo vya kutolea chanjo ya Uviko-19, tulianza na vituo 550 nchi nzima na sasa chanjo zinatolewa katika vituo vyote vinavyotoa chanjo zingine nchini. Kuna vituo zaidi ya 6,784 vinatoa chanjo na pia wataalamu wa kutoa chanjo sasa wanakwenda hadi vijijini na maeneo yote yenye mikusanyiko ya watu. Hata juzi kwenye mtanange wa Yanga na Simba, watu wamepata chanjo pale," alisema Msigwa. 

Alisema kwa tulipofikia sasa, hatutaki Mtanzania aliyetayari kupata chanjo apate shida ya kwenda sehemu ya kuchanjwa. Tunaweka vituo vya chanjo kwenye vituo vya mabasi, kwenye masoko, vituo vya kupima uzito magari, Mwenge wa uhuru, tunakwenda mechi ya watani wa jadi na kila mahali ambapo tunaona pana weza kuwarahisishia watu kupata chanjo. Na hii ni kwa sababu, tumeona Watanzania wengi wapo tayari kupata chanjo lakini changamoto imekuwa kuvifikia vituo vinavyotoa chanjo. 

Alisema utoaji chanjo unakwenda vizuri, mpaka leo Watanzania takribani 400,000 wamechanjwa na wengine wanaendelea kupata chanjo dhidi ya uviko-19. Kasi hii imeongezeka sana baada ya Wizara ya Afya, TAMISEMI na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuzindua Awamu ya Pili ya Uhamasisha na utoaji elimu (Sepetemba 15, 2021) ambapo sasa chanjo zinapelekwa hadi vijijini na Wataalamu wetu sasa wameanza kupita nyumba kwa nyumba ili wale ambao wapo tayari kupata chanjo wapate. 

Aliongeza kuwa Serikali inawapongeza Wataalamu wa Afya wote kwa kazi kubwa wanayoifanya, kwanza kwa wao wenyewe kuonesha mfano kwa kupokea chanjo na pili kupeleka huduma za Mkoba kwa wananchi (yaani mwananchi anapata chanjo pale alipo. 

Msigwa alimpongeza kijana Michael Filbert Nondo ambaye ameamua kusafiri kwa baiskeli kutoka Kigoma hadi Dar es Salaam akipita kuhamasisha wananchi kupokea chanjo. Leo amefika Dodoma na kukutana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,  Jinsia, Wazee na Watoto lakini kwa bahati mbaya hatoweza kumaliza safari yake baada ya kupatwa na msiba wa kufiwa na mwanae huko Kigoma. Nawaomba vijana wote tuungane kuhamasisha jamii kupata chanjo kama anavyofanya kijana huyo. 

Alisema Serikali inahimiza watu kuchukua tahadhari dhidi ya Uviko-19 na kupata chanjo kwa sababu KINGA NI BORA KULIKO TIBA. Kitengo cha Kinga cha Wizara ya Afya kinachoongozwa na Dkt. Leonard Subi wanafanya kazi kubwa ya kuhakikisha wananchi wanapata elimu na chanjo, na leo hapa nimeongozana na Dkt. Ama Kasangala, yeye ni Kaimu Mkurugenzi wa kitengo cha elimu ya afya kwa Umma cha Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. 

Alisema  kwa kutambua kuwa Waandishi wa Habari wana umuhimu mkubwa katika jukumu la kuwaelimisha Watanzania kukabiliana na Uviko-19 Serikali imeona iongeze ushirikiano nao ambapo alimtambulisha Rais wa Umoja wa Vyama vya Waandishi wa Habari vya Mikoa (UTPC)  Deogratius Nsokolo alikuwa ameongozana naye. 

"Mimi lengo langu Waandishi wa Habari twende pamoja, tufanye kazi zetu kwa kuzingatia weledi, sheria za nchi, kanuni na taratibu lakini muhimu zaidi tuiweke nchi yetu kwanza (Tanzania Kwanza), tuwapiganie Watanzania pamoja. Kwenye hili janga la Korona Watanzania wanakufa kwa sababu ya kutozingatia afua hizi za kukabiliana na virusi vya ugonjwa huu, kutozingatia kuwa KINGA NI BORA KULIKO TIBA," alisema Msigwa. 

Msigwa alihitimisha hutuba yake kwa kuwaomba Waandishi wa Habari kushirikiana na Wataalamu waliopo katika mikoa yote hapa nchini  kuhakikisha elimu kwa wananchi inafika ipasavyo kwa kuwasiliana na Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Waganga wa Hospitali zetu, viongozi wa Mikoa na Wilaya ili Watanzania wapate chanjo na wajikinge na balaa hilo. 

Katika mkutano huo Msigwa alipata fursa ya kujibu maswali mbalimbali ya wananchi waliokuwa wakipiga simu moja kwa moja kwenye mkutano huo.

No comments:

Post a Comment