Na Benny Mwaipaja, WFM, Mahe, Seychelles
TANZANIA imekabidhi uongozi wa mwaka mmoja wa Umoja wa Udhibiti wa Fedha Haramu wa Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika (ESAAMLG) kwa nchi ya Seychelles, huku ikijivunia mafanikio makubwa ya kuhakikisha kuwa nchi wanachama wa umoja huo zinakuwa na sera, sheria, taasisi na mifumo imara inayowezesha mapambano dhidi ya vitendo vya utakasishaji fedha haramu na ufadhili wa ugaidi.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, amekabidhi uongozi huo kwa niaba ya Serikali ya Tanzania kwa Waziri wa Fedha, Biashara, Uwekezaji na Mipango ya Kiuchumi wa Seychelles Balozi Maurice Lousteau – Lalanne, wakati wa Mkutano wa 18 wa Baraza la Mawaziri wa Umoja huo, uliofanyika Mjini Mahe, nchini Seychelles na kushuhudiwa na Rais wa Nchi hiyo, Mhe. Danny Faure.
Miongoni mwa mafanikio yaliyofikiwa katika kipindi hicho cha mwaka mmoja, ni kufanyika kwa tathimini ya mifumo ya kudhibiti utakasishaji wa fedha haramu na ufadhili wa ugaidi wa nchi tatu wanachama wa umoja huo za Mauritius, Madagascar na Seychelles, na kwamba zoezi la kuzitathmini nchi nyingine mbili za Zambia na Malawi, linaendelea.
"Rasilimali za nchi zetu zinahitaji kutumika vizuri, kwa sababu zinapotumika vibaya zinapunguza uwezo wa nchi zetu kuchochea maendeleo haraka, pale zinapo hatarisha sekta yetu ya fedha, matumizi adili ya rasilimali hizi na usalama wa nchi zetu" alisema Dkt. Mpango
Aidha, Dkt. Mpango amesema kuwa utakasishaji wa fedha haramu unazuiwa kwa sababu unamadhara makubwa kiuchumi, kijamii na kiusalama kwa nchi wanachama..
"Fedha ambazo zinakuja kuja tu hivi! Hujui kama zinakwenda kugharamia ugaidi, au ni fedha za wananchi wetu lakini wanazitorosha ambapo badala ya kuzitumia ipasavyo wanazitumia kufanya mambo haramu" aliongeza Dkt. Mpango
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Umoja wa nchi za Mashariki na Kusini Mwa Afrika ESAAMLG, Dkt. Elliawony Kisanga amesema kuwa tangu umoja huo uanzishwe miaka 19 iliyopita, yamekuwepo mafanikio makubwa na kazi iliyopo mbele ya uongozi mpya ni kuanza na kuendelea kufanyika kwa tathmini ya mifumo ya udhibiti ya nchi za Zambia, Malawi na Tanzania.
Mwenyekiti Mpya wa ESAAMLG, Waziri wa Fedha, Biashara, Uwekezaji na Mipango ya Kiuchumi wa Seychelles Balozi Maurice Lousteau – Lalanne, ameipongeza Tanzania chini ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, kwa uongozi wake mahili na kuuwezesha umoja huo kutekeleza majukumu yake ipasavyo na msukumo wake utakuwa kuwezesha nchi wanachama kuendelea kusimamia utekelezaji wa sheria.
Aidha Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa ESAAMLG ulitanguliwa na Mkutano wa 36 wa Kikosi Kazi cha Maafisa waandamizi wa ESAAMLG, ambapo Bw. Onesmo Makombe alikabidhi kwa niaba ya Tanzania Uenyekiti wa Kikosi Kazi hicho kwa Bw. Philip Moustache wa Jamhuri ya Seychelles.
Tanzania ilipokea uongozi wa Umoja huo Septemba 7 mwaka jana wakati wa Mkutano wa 17 wa Baraza la Mawaziri wa Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika uliofanyika Zanzibar, ikipokea majukumu ya uongozi huo kutoka nchi ya Zimbabwe ambapo Umoja huo unaundwa na nchi 18 ambazo ni Angola, Botswana, Eswatini, Ethiopia, Kenya, Lesotho, Madagascar, Malawi, Mauritius, Mozambique, Namibia, Rwanda, Seychelles, South Africa, Tanzania, Uganda, Zambia na Zimbabwe.
No comments:
Post a Comment