Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joseph Mkirikiti (kulia) akikabidhi Mwenge wa Uhuru kwa Mkuu wa Wiaya ya Sumbawanga Sebastian Waryuba (kushoto) jana katika kijiji cha Tunko wilaya ya Sumbawanga.
MWENGE wa Uhuru Kitaifa utatembelea miradi 18 ya maendeleo na vikundi saba vya wajasiriamali mkoani Rukwa kwa pamoja vikiwa na thamani ya Sh bilioni 10.55/-
Miradi hiyo itawekewa mawe ya msingi, itakaguliwa na kuzinduliwa katika wilaya tatu za Sumbawanga, Kalambo na Nkasi.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa,Joseph Mkirikiti alieleza hayo jana (20.09.2021) baada ya kukabidhiwa mwenge huo na Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Omary Mgumba katika sherehe ya makabidhiano katika kijiji cha Tunko kilichopo katika wilaya ya Sumbawanga mpakani na Mkoa wa Songwe.
Akizungumzia mchanganuo wa uchangiaji wa miradi hiyo alisema wananchi wamechangia Sh 101,496,100.00, Halmashauri zimechangia Sh 183,094,374/-, Serikali Kuu umechangia Sh 9,986,485,860/- huku wadau wa maendeleo na wahisani wamechangia Sh 286,174,244.07
" Mwenge wa Uhuru Kitaifa utakimbizwa kilomita 544.9 katika wilaya tatu za kiutawala" alieleza.
Alisema mkoa umejipanga kikamilifu katika kutekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya mbio za Mwenge wa Uhuru 2021 " TEHAMA ni msingi wa Taifa endelevu ; Itumike kwa usahihi na uwajibikaji".
Akizungumzia mapambano dhidi ya rushwa alisema katika kipindi cha Juni2020 hadi Julai 2021 Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoa uliokoa kiasi cha Sh 502,952,380/- ambazo Sh 334,464,330/- zilidhibitiwa na Sh 168,488,000/- zilikuwa fedha taslimu.
Kwa upande wake Kiongozi wa Taifa wa Mbio Maalumu za Mwenge wa Uhuru Kitaifa,Luteni Josephine Mwambashi alizitaka halmashauri kuhakikisha nyaraka zote muhimu zinakuwepo katika miradi itakayokaguliwa.
Pia alizitaka halmashauri katika miradi yote itakayokaguliwa na mwenge huo wawepo wataalamu ambapo watatoa taarifa za kina pia wawe na uwezo wa kujibu maswali watakayoulizwa na wakimbizi Mwenge Kitaifa.
Ukiwa katika halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga Mwenge wa Uhuru umezinduka jengo la ofisi ya Mthibiti Ubora wa Elimu katika mji mdogo wa Laela ambalo ujenzi wake umegharimu zaidi ya Sh milioni 169.2/- na
Pia utazindua vyumba viwili vya madarasa na ofisi ya walimu katika Shule ya Sekondari Sumbawanga ambao ujenzi wake umegharibu Sh milioni 44/- na utakagua barabara ya Mpanda 'Road' - Katandala Mission- Mashine za Mpunga- Majengo ambao ujenzi wake umegharimu Sh bilioni 7.9/-
Mwenge wa Uhuru ulioasisiwa na Baba wa Taifa,Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1961 mbio zake zilianza rasmi mwaka 1964 huu ukiwa ni mwaka 29 tangu mbio za Mwenge wa Uhuru zirejeshwe chini ya uratibu na usimamizi wa Serikali
No comments:
Post a Comment