DKT MABULA AAGIZA KUMALIZWA MGOGORO WA ARDHI WANANCHI NA MAGEREZA KONDOA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday, 21 September 2021

DKT MABULA AAGIZA KUMALIZWA MGOGORO WA ARDHI WANANCHI NA MAGEREZA KONDOA

Kamishna wa Ardhi Msaidizi Thadei Kabonge akizungumza katika kikao kati ya Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula na viongozi pamoja na watendaji wa sekta ya ardhi katika wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma leo tarehe 21 Sept 2021 akiwa katika ziara ya siku tano mkoani Dodoma.

Na Munir Shemweta, KONDOA

NAIBU Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameiagiza halmashauri ya Mji wa Kondoa kushughulikia mgogoro wa ardhi kati ya Gereza la King'ang'a na wananchi katika halmashauri hiyo.

 

Dkt Mabula ametoa maelekezo hayo leo tarehe 21 Septemba alipokutana na viongozi pamoja na watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri za wilaya na mji wa Kondoa akiwa katika mwanzo wa ziara yake ya siku tano katika mkoa wa Dodoma.

 

Alisema, suala la migogoro ya mipaka linapaswa kushughulikiwa na halmashauri husika na juhudi za makusudi zisipochukuliwa basi migogoro ya ardhi haiwezi kuisha katika halmashauri.

 

Kwa mujibu wa Dkt Mabula, mgogoro unaoendelea sasa iwapo pande zinazopingana zingekaa pamoja na kushughulikia suala hilo ungekuwa umekwisha kwa kuwa wananchi walisharidhia kuachia sehemu ya eneo kwa shughuli za magereza.

 

Katika kuharakisha utatuzi wa mgogoro huo, Naibu Waziri wa Ardhi alimuelekeza Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Dodoma Thadei Kabonge kupeleka wataalamu wa upimaji eneo hilo ili kuainisha mipaka na utekelezaji huo ufanyike haraka.

 

"Naelekeza halmashauri husika kukutanisha pande zote na kuangalia nyaraka za umiliki na utekelezaji wake ufanyike mapema ili kuondoa mgogoro huo" alisema Dkt Mabula.

 

Aidha, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ameielekeza pia halmashauri ya Mji wa Kondoa kuhakikisha inawapatia viwanja takriban wananchi 200 katika eneo la Bicha ambapo halmashauri ilishachukua fedha kwa ahadi ya kuwapatia viwanja lakini ilishindwa kutekeleza.

 

"Halmashauri ya mji wa Kondoa mfikirie namna ya kusolve huu mgogoro wa wananchi ambao mmeshachukua fedha kwa ajili ya kuwapatia viwanja na hapa ofisi ya Kamishna mkoa wa Dodoma katika wiki ya kwanza ya mwezi Oktoba iende kupima viwanja kwa ajili ya kuwapatia wananchi" alisema Naibu Waziri wa Ardhi.

 

Awali Mbunge wa jimbo la Dodoma Mjini mkoani Dodoma Ally Makoa alimueleza Dkt Mabula kuwa changamoto kubwa katika jimbo lake ni mgogoro kati ya wananchi na jeshi la Magereza, mgogoro wa eneo la hifadhi pamoja na ule mgogoro wa wananchi walinaotaka kupatiwa viwanja.

 

Alisema, migogoro hiyo ikitatuliwa basi katika mji huo wa Kondoa hautakuwa na migogoro ya asili na itakayoibuka ni ile itakayosababishwa na watu.

No comments:

Post a Comment