DKT. CHAULA AKABIDHI VITUO VYA TEHAMA ZANZIBAR - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Saturday, 4 July 2020

DKT. CHAULA AKABIDHI VITUO VYA TEHAMA ZANZIBAR

Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano) wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Zainabu Chaula (katikati) akikabidhi nyaraka zilizosainiwa za makabidhiano ya Vituo vya TEHAMA kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,Mawasiliano na Usafirishaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) Bwana Mustapha Aboud Jumbe (kushoto), (kulia) ni Mtendaji mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Bi. Justina Mashiba akushuhudia.

KATIBU Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano) wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Zainabu Chaula amekabidhi vituo 10 vya TEHAMA kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Bwana Mustapha Aboud Jumbe wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na kuagiza vituo hivyo vitumike kuwapatia wananchi wa Zanzibar huduma za TEHAMA hasa wale ambao hawana namna ya kupata huduma hiyo.

Vituo hivyo vilivyojengwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwa gharama ya shilingi 1,138,000,000 vimekabidhiwa rasmi katika hafla fupi ya makabidhiano iliyofanyika katikati ya wiki kisiwani Unguja katika Mkoa wa Mjini Magharibi eneo la Kiembe Samaki. 

“Vituo hivi vitumike kuongeza tija na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa Zanzibar,kwa kutambua hilo Wizara yenye dhamana ya mawasiliano inapaswa kuandaa mwongozo wa utendaji kazi ili vituo hivi viweze kujiendesha vyenyewe na hatimaye kuwezesha ujenzi wa vituo vingine kama hivi angalau kituo kimoja kwa mwaka”, alisisitiza Dkt. Chaula

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Bwana Mustapha Aboud Jumbe amesema kuwa ujenzi wa vituo vya TEHAMA Zanzibar ni jambo linaloimarisha Muungano kwa kuwekeza moja kwa moja kwa wananchi na kuzitaka taasisi nyingine za Muungano kutafuta mbinu za kuwasogezea huduma wananchi. 

“Maisha ya siku hizi yamekuwa ya kidijitali ambapo huduma nyingi zinafanyika kwa mtandao kama vile fomu za maombi ya ajira, passport na viza zinajazwa mtandaoni, hivyo kusogeza huduma hii kwa wilaya zote 10 ni jambo muhimu sana”, alisema Bwana Jumbe. 

Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote nchini (UCSAF) Bi. Justina Mashiba amesema kuwa matarajio baada ya ujenzi wa vituo hivyo ni kuamsha ari ya matumizi ya TEHAMA kwa wananchi wote wa maeneo husika wenye nia ya kutumia huduma ya hiyo pasipo kubaguliwa ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Vituo vya TEHAMA katika mikoa yote kumi Zanzibar ambapo kisiwani Unguja Vituo vimejengwa katika mikoa Sita ya kusini magharibi-Tunguu, Mjini Magharibi-Mwera,Kusini Unguja-kitogani, Kaskazini Unguja-Mkokotoni,Mjini Magharibi-Kiembe Samaki ,kaskazini unguja-Mahonda na Kisiwani Pemba Vimejengwa katika eneo la Wete, macho manne,Micheweni na Chonza, kwa lengo la kuwasogezea wananchi huduma za TEHAMA. 


No comments:

Post a Comment