Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na Viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA) pamoja na Wajumbe alipokuwa akifunga mkutano huo uliofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Edema, Mkoani Morogoro. |
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akisistiza jambo wakati wa mkutano huo uliofanyika jana Mkoani Morogoro. |
Na Mwandishi Wetu, Morogoro
USHIRIKIANO mzuri baina ya Serikali na Wafanyakazi umechangia katika kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi iliyofikia uchumi wa kati mwaka huu 2020. Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama alipokuwa akifunga Mkutano wa Baraza Kuu la Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) uliofanyika Mkoani Morogoro.
Waziri Mhagama alieleza kuwa bidii ambayo wafanyakazi nchini wameonesha katika utekelezaji wa majukumu yao kwenye sekta mbalimbali imekuwa ni chachu kwa taifa katika kufikia uchumi huo wa kati mapema sana wakati ilikuwa imelenga kufikia kiwango hicho 2025.
“Hali ya ukuaji wa uchumi hadi hapa ilipofikia ni kutokana na Serikali ilivyoweza kutekeleza kazi yake kwa kushirikiana na wafanyakazi ambao wamekuwa ni msingi mkubwa wa maendeleo ya uchumi wa nchi,” alieleza Mhagama.
“Hii ni ishara kuwa Wafanyakazi wamekuwa na ushirikiano wa karibu na serikali yao na pia wameonyesha dhamira dhati na utayari wa kujitolea kushiriki kwenye sekta mbalimbali za kimaendeleo ambazo zitaboresha Maisha ya watanzania kwa ujumla,” alisema Mhagama.
Alifafanua kuwa Rais wa Jamhuri ya Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amefanya mageuzi makubwa sana ya kiuchumi, akitolea mfano wa jitihada kumbwa alizozifanya ikiwemo utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati pamoja na jinsi anavyosimamia sera za uchumi nchini ambazo leo hii tunashuhudia maendeleo yaliyopo nchini.
“Mheshimiwa Rais aliwapongoza wananchi kwa mafanikio hayo ila kipekee pia tatambue na kupongeza juhudi zake katika kuiwezesha Tanzania kuingia uchumi wa kipato cha kati,” alisema Mhagama.
Alieleza kuwa Shirikisho hilo ni chombo muhimu kinachowaunganisha wafanyakazi wote nchini na ndio kinachofanya kazi na serikali katika kuhakikisha haki na majukumu ya wafanyakazi yanawasilishwa Serikalini na kwa waajiri nchini. Aliongeza kwa kuwapongeza wafanyakazi nchini kuwa sehemu ya mafanikio hayo ambayo yataweza kuboresha hali zao ikiwemo maslahi ya wafanyakazi.
“Serikali itaendelea kuthamini mchango wa Vyama vya Wafanyakazi katika kuimarisha mshikamano na umoja kwa kuheshimu dhhana ya utatu,” alisema.
Sambamba na hayo amelitaka Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) kutengeneza mpango kazi wa kutoa elimu ya Sheria mbalimbali zinazohusu masuala ya ajira na mahusiano kazini kwa viongozi wa vyama vya wafanyakazi.
“Nimatumaini yangu mkiwa na mpango huo utawasaidia kupata elimu itakayo wawezesha kuwa na majadiliano mazuri baina ya waajiri na wafanyakazi, na itakuwa ni suluhisho ya kutatua migogoro ambayo imekuwa ikijitokeza,” alisema Mhagama.
Alieleza, Ofisi ya Waziri imeandaa programu maalumu inayolenga kuvifikia vyama vyote vya wafanyakazi lengo ikiwa ni kuwapatia ujuzi wa masuala mbalimbali kuhusiana na sekta hiyo ya kazi ikiwemo namna ya kuandaa mikataba ya hali bora ambayo imekuwa ni chachu kwa wafanyakazi kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Aidha, Waziri Mhagama ametoa maagizo kwa Viongozi wa TUCTA pamoja na Vyama vya Wafanyakazi vyote kwa ujumla kuhakikisha wanakuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha na rasilimali za vyama vyao, kuheshimu maamuzi ya vikao na pia maamuzi yatakayotolewa na viongozi yawe shirikishi, kupunguza mogogoro isiyo ya lazima pamoja na kuwasisitiza wanapoelekea kwenye uchaguzi wa vyama vyao wafuate taratibu na kuzingatia sheria na kanuni.
Kwa Upande wake, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) Bw. Tumaini Nyamhokya aliahidi kufanyia kazi maagizo yote yaliyotolewa na alielezea Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli imekuwa ikishirikiana na Vyama vya Wafanyakazi kwa karibu pamoja na kushughulikia masuala mbalimbali ya wafanyakazi.
“Serikali hii ya awamu ya tano imetufanyia mambo mengi wafanyakazi, katika kipindi hiki suala la punguzo la kodi kwa wafanyakazi limekuwa ni faraja kubwa kwa wafanyakazi, tunaahidi kuendelea kushirikiana na serikali kutokana na namna inavyotujali,” alisema Nyamhokya.
Naye Kaimu Katibu Mkuu Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) Bw. Said Wamba alisema kuwa Shirikisho hilo la Vyama vya Wafanyakazi litaendelea kudumisha mshikamono na umoja kwa kutetea maslahi ya wafanyakazi ili waweze kufanyakazi kwa tija na kuleta ufanisi kwenye sekta ya kazi.
Mkutano huo wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) ulianza rasmi 29 Juni 2020 na kuhitimishwa Julai 3, 2020 ambapo katika mkutano huo yalitolewa mafunzo kwa viongozi na wajumbe kutoka kwenye vyama shiriki 13 ikiwemo CWT, TUICO, TALGWU, TUICO, TUGHE, CHODAWU, TEWUTA, TPAWU, TAMICO, COTWU (T), DOWUTA, RAAWU, TRAWU na TASU.
No comments:
Post a Comment