Jengo la Mpanda Palaza ambalo ni kitegauchumi cha Shirika la Taifa la Nyumba (NHC) limezinduliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa mjini Mpanda, Julai 4, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu). |
*Awataka wasiwe madalali wa kuingiza wahamiaji haramu nchini
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amewataka watu wanaoishi kwenye makazi ya Mishamo na Katumba wawe waadilifu na wasitumike kama madalali wa kuingiza wahamiaji haramu nchini.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema mkoa wa Katavi umekithiri kwa kuwa na wahamiaji haramu wengi, hivyo amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Juma Homera ashughulikie tatizo hilo. Ametoa agizo hilo Julai 4, 2020 alipozindua jengo la ofisi na biashara la Mpanda Plaza lililojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) mjini Mpanda kwa gharama ya sh bilioni 2.8.
“Katavi imetulia lakini haijatengamaa kwa sababu ni kati ya mikoa yenye idadi kubwa ya wahamiaji haramu nchini ambao njia yao wanayotumia kuingilia Katavi ni makazi ya Katumba na Mishamo.”
Waziri Mkuu amesema Tanzania haijazuia watu wa Mataifa mengine kuingia nchini ila inawataka wafuate taratibu zilizowekwa na si kuingia kwa kutumia njia za panya.
Amesema anamajina ya watu zaidi 2,000 walioingia Tanzania kwa njia za panya na wamejiingiza katika maeneo mbalimbali, amewataka warudi kwao na wafuate taratibu kabla ya kuja tena nchini.
Akizungumzia kuhusu ujenzi wa Mpanda Plaza, Waziri Mkuu ameliponeza Shirila la Nyumba la Taifa kwa uwekezaji huo ambao utaliwezesha shirika hilo kujiongezea tija.
Kadhalika, Waziri Mkuu amelielekeza shirika hilo kwenda kujenga majengo ya makazi katika wilaya mpya ili kuwawezesha watumishi na wananchi kuishi kwenye makazi bora.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Dkt. Maulidi Banyani amesema uzinduzi wa jengo hilo la ghorofa tano ni muendelezo wa miradi iliyowekezwa na NHC kwa gharama ya sh bilioni 7.2 mkoani Katavi.
Dkt. Banyani amesema miradi mingine iliyowekezwa na NHC mkoani Katani ni pamoja na ujenzi wa nyumba 70 eneo la Ilembo, nyumba 24 katika mji wa Inyonga, Mlele.
“Tumejenga nyumba tano za Wakuu wa Idara halmashauri ya Wilaya ya Mlele, nyumba 24 za walimu katika shule ya msingi Kakuni, nyumba sita shule ya Kibaoni halmashauri ya Mpimbwe.”
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, alisema miongoni mwa changamoto zilizokuwa zinaukabili mkoa huo ni majangili ambapo waliendesha operesheni na kufanikiwa kikamata silaha 100.
Alisema kwa sasa wananchi wanaendelea kufanya kazi na kwamba ukusanyaji wa mapato umeongeza kutoka asilimia 76 mwaka 2019 hadi kufikia asilimia 97 mwaka huu.
Mkuu huyo wa mkoa ameongeza kuwa mbali na kuboresha ukusanyaji wa mapato, pia wameimarisha upatikanaji huduma za afya hususani kwa mama na mtoto.
No comments:
Post a Comment