WAMILIKI WA ARDHI WAIKOSESHA SERIKALI TAKRIBANI BILIONI 125 - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Saturday, 4 July 2020

WAMILIKI WA ARDHI WAIKOSESHA SERIKALI TAKRIBANI BILIONI 125

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akimuonesha mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Taleck Ramani ya mkoa wake baada ya kumkabidhi wakati wa uzinduzi wa ofisi ya ardhi mkoa wa Shinyanga jana.Kulia ni Kamishna Msaidizi wa Ardhi Usimamizi na Uratibu Wizara ya Ardhi Wilson Luge.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akiangalia hati ya Bibi Zainab Kechuba kabla ya kumkabidhi  wakati wa uzinduzi wa ofisi ya ardhi mkoa wa Shinyanga jana. Kushoto ni Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Taleck.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akikata utepe kuashiria kuzinduliwa rasmi ofisi ya ardhi mkoa wa Shinyanga jana. Wa pili kulia ni Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Taleck na wa pili kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akimkabidhi Hati miliki ya ardhi Afisa Uhamiaji mkoa wa Shinyanga wakati  wa uzinduzi ofisi za ardhi mkoa wa Shinyanga ambapo alizitaka taasisi za serikali kuhakikisha zinapima maeneo yao na kumilikishwa. Kushoto ni mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Taleck.

Na Munir Shemweta, WANMM SHINYANGA

WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amesema zaidi ya wamiliki wa ardhi laki tisa nchini hawajamilikishwa ardhi na kupatiwa hati na hivyo kuisababishia serikali kushindwa kukusanya takriban  bilioni 125. 

Kufuatia hali hiyo Lukuvi ameagiza wamiliki wote nchini wakowemo zaidi ya 60,000 wa mkoa wa Shinyanga ambao viwanja vyao vimepimwa na michoro yake kuidhinishwa waende ofisi za ardhi katika halmashauri za wilaya kufuatilia hati ili waweze kumilikishwa ndani ya siku tisini

Waziri Lukuvi alisema hayo tarehe 3 Julai 2020 mkoani Shinyanga wakati wa uzinduzi ofisi za ardhi mkoa ikiwa ni mfululizo wa uzinduzi wa ofisi za ardhi katika mikoa mbalimbali nchini.

Alibainisha kuwa, mwananchi ambaye atashindwa kwenda kufuarilia hati yake katika kipindi cha siku tisini atapelekewa stakabadhi ya malipo ikimtaka alipe kuanzia pale ambapo kiwanja chake kilipimwa na michoro kuidhinisha.

"wale wamiliki ambao watashindwa kufuatilia hati katika kipindi cha siku tisini wataanza kudaiwa kodi ya pango la ardhi kuanzia pale michoro ilipoidhinishwa hata kama michoro hiyo iliidhishwa mwaka 1962  ataanza kudaiwa kuanzia hapo maana itakuwa ni uzembe wake," alisema Lukuvi.

Kwa mujibu wa Waziri wa Ardhi, serikali inataka kila mtanzania apate hati miliki ya ardhi kwa mujibu wa sheria kwa kuwa serikali inashindwa kukusanya kodi ya ardhi kwa mtu ambaye hana hati na kuwataka wamiliki wachukue hati zao ili serikali ipate mapato na kutoa huduma katika sekta mbalimbali kama vile barabara, maji na hospitali.

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack alishukuru kuanzishwa ofisi ya ardhi mkoa wa shinyanga na kueleza kuwa tayari amenza kuaona matunda ya ofisi hiyo kwa kupungua kwa migogoro ya ardhi katika mkoa wake na kuwahimiza wananchi wake kwenda katika ofisi za ardhi mkoa kuchukua hati.

"kama mkoa tutahakikisha tunaleta utulivu kutokana na kuanzishwa ofisi za ardhi katika mkoa wa shinyanga kwa kuwa migogoro itakuwa imepungua,"alisema Zainab.

Tayari zoezi la uzinduzi ofisi za ardhi katika mikoa mbalimbali limefanyika katika mikoa kumi na linaendelea katika mikoa ya Mara, Geita, Kagera, Lindi na Ruvuma.

Katika hatua nyingine Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi Lukuvi aliwakabidhi hati za ardhi wananchi pamoja na taasisi za serikali zilizopo mkoa wa Shinyanga akiwemo Bibi wa miaka 77 Zainab Kechuba aliyeonesha furaha kubwa baada ya kukabidhiwa hati yake.
Bibi Zainab alieleza kuwa, aliihangaikia hati yake kwa muda mrefu lakini sasa amefurahi kwa kupatiwa hati yake na kumuombea Rais John Pombe Magufuli umri mrefu na kuendelea kutawala Tanzania.
Waziri wa Ardhi alisema mwaka huu uwe mwisho wa migogoro ya ardhi kwa kuwa huduma za ardhi zimepelekwa karibu na wananchi kwa kuanzisha ofisi za ardhi za mikoa zenye wataalamu wa fani zote za ardhi sambamba na kusambaza vifaa mbalimbali vikiwemo vya upimaji katika mikoa.

No comments:

Post a Comment