MKUTANO WA MWAKA WA MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI DODOMA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday, 29 September 2021

MKUTANO WA MWAKA WA MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI DODOMA

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima akitoa tuzo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa CCBRT Brenda Msangi kwa mchango wa Shirika hilo kutoa ajira  nyingi katika Jamii.

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

SERIKALI imesisitiza nia yake kuendelea kujenga, kuboresha na  mazingira wezeshi kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini kufanya kazi kwa ufanisi na kuchochea  Maendeleo ya Taifa. 

Akifungua Mkutano wa Mwaka wa Mashirika hayo Jijini Dodoma ,Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima amesema Serikali inatambua  kazi kubwa inayofanywa na NGOs katika kuisaidia Serikali ili kuwaletea wananchi Maendeleo.

"Mashirika yanakwenda hatua kwa hatua na Serikali na hata Maendeleo haya tuliyonayo na hapa tulipofika ni kutokana na mchango mkubwa wa Mashirika haya" amesema Waziri Gwajima.

Mhe. Gwajima ameongeza kuwa Mkutano huo ni fursa muhimu ya kujadiliana masuala mbalimbali ya Maendeleo ikiwemo kuyajengea uwezo Mashirika hayo kuhusu sheria na kanuni zinazoongoza NGOs na Serikali pia kufahamu changamoto na shughuli zinazofanywa na NGOs ili kuwa na uelewa wa Pamoja.

Aidha, Mhe. Gwajima ametoa wito kwa NGOs kuimarika kwa kufanya kazi kwa weledi na uzalendo, kufuata sheria na kanuni zake kwa manufaa ya Taifa na kwamba Serikali ipo tayari kupokea maoni na changamoto kupitia Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yaani NaCONGO.

Amesisitiza kuwa, NGOs zifanye kazi kwa uwazi na uwajibikaji kwenye mipango yao ya kila mwaka hususani kuanzia kwenye maeneo wanayofanyia kazi. 

Amesema hatarajii kupokea malalamiko ya ukiukwaji wa misingi ya sheria kutoka pande zote za Serikali na Mashirika na kuwe na mifumo ya kujiratibu katika kuisaidia Jamii kutatua changamoto kwa kushirikiana na Jamii zinazowazunguka.

Mhe. Waziri ametumia fursa hiyo pia kuyahimiza Mashirika hayo kushirikiana na watendaji kwenye maeneo yao kuhakikisha elimu ya chanjo ya UVIKO 19 inatolewa kwa kina, ili wananchi wajitokeze kwa hiyari kuchanja.

"Nia ya Rais wetu Mhe. Samia Suluhu Hassan ni kuona Taifa lipo salama kwa kutekeleza afua za kinga ikiwemo chanjo kwa hiyari na dawa ni kuwa na elimu ya kutosha, hivyo Wadau niwakumbushe kushirikiana na wataalamu wa Afya kusimamia na kuwezesha elimu ya kutosheleza kwa wananchi ili suala la hiyari lifanyike" ameongeza Dkt. Gwajima.

Waziri Gwajima pia ametoa tuzo kwa baadhi ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yaliyofanya vizuri hasa kwa upande wa kuzalisha ajira nyingi kwa Watanzania yakiongozwa na CCBRT na Marie Stopes.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCONGO) Dkt. Lilian Badi amempongeza Waziri Gwajima Kwa kufanikisha uchaguzi wa NaCONGO na kusema kuwa ni wakati wa kufungua macho na kuboresha utendaji kazi kwa kushirikiana na Serikali ili kuongeza Kasi ya Maendeleo. 

Awali akiwasilisha maelezo kuhusu Ofisi yake na huduma za uratibu na usajili, Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Vickness Mayao amesema lengo la Mkutano huo ni kuimarisha ushirikiano na uhusiano wa NGOs na Serikali kwa kujadiliana changamoto zilizopo na namna ya kuzitatua kwa kuzingatia Sheria na Sera zilizopo.

Aidha, Mkutano umelenga kutambua na kujadili mchango wa NGOs katika Maendeleo ya Jamii na Taifa kwa ujumla.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu anayewakilisha Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Mhe. Neema Lugangira ameiomba Serikali kufanya mapitio ya kanuni ya fedha ya NGOs kuwezesha kupata vibali mapema ili kuharakisha utekelezaji wa miradi ya Maendeleo.

No comments:

Post a Comment