NMB YAKABIDHI HUNDI YA SH. MILIONI 438.4 KWA WAHANGA WA MOTO KARIAKOO - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday, 27 July 2021

NMB YAKABIDHI HUNDI YA SH. MILIONI 438.4 KWA WAHANGA WA MOTO KARIAKOO

Mkuu wa Kitengo cha Bima Benki ya NMB, Martine Massawe akizungumza wakati wa kukabidhi mfano wa hundi kwa wafanyabiashara waliokuwa na Bima waliounguliwa katika Soko Kuu la Kariakoo. Kushoto ni  Meneja Madai wa kampuni ya bima ya Reliance, Joel Mwakalebela na kulia ni Meneja wa Bima Benki ya NMB, Adam Nsenga.


Meneja wa Madai wa Kampuni ya Bima ya Reliance, Joel Mwakalebela akipongezana na mmoja wa wafanyabiashara waliounguliwa na Moto katika Soko Kuu la Kariakoo, Emmanuel Kabadi (kushoto) baada ya Benki ya NMB kukabidhi mfano wa hundi ya zaidi ya Shilingi Milioni  438 kwa wafanyabiashara 12  waliokuwa na Bima. Kushuto ni Sajida Kagasheki  mmoja wa wafanyabiashara na Kulia ni Meneja wa Bima wa Benki ya NMB, Adam Nsenga.

Mkuu wa Kitengo cha Bima wa Benki ya NMB, Martine Massawe(katikati) akikabidhi mfano wa hundi  ya Sh. Milioni 438 kwa wafanyabiashara 12 waliokuwa na Bima waliounguliwa katika Soko la Kuu la Kariakoo, Sajida Kagasheki na Emmanuel Kabadi (kushoto) wakati wa makabidhiano yaliyofanyika katika katika Tawi la NMB Kariakoo Business Center. Kutoka kulia ni Meneja wa Bima wa Benki ya NMB, Adam Nsenga na Meneja wa Kampuni ya Reliance, Joel Mwakalebela.

BENKI ya NMB kupitia Kampuni ya Reliance Insurance, imewalipa bima ya Sh. Milioni 438.4 wafanyabiashara 12, kati ya waliounguliwa moto maduka yao katika Soko la Kariakoo, Julai 10 mwaka huu. Wafanyabiashara hawa ni waliokuwa wamekatia bima mikopo na biashara zao kupitia NMB.

Hafla ya kuwakabidhi wafanyabiashara hao hundi hiyo, imefanyika katika Tawi la NMB Kariakoo Business Center, ambako wahanga hao walikiri kuwa hasara na maumivu yao ya kuunguliwa yamepozwa na malipo hayo ya haraka ya bima.

Akizungumza kabla ya kuwakabidhi hundi ya mfano, Mkuu wa Kitengo cha Bima Benki ya NMB, Martine Massawe, alitoa wito kwa Watanzania kujenga utamaduni chanya wa kuzilinda kwa bima mali na pesa wanazotafuta kwa jasho, ili kuepuka maumivu yasiyo na mfariji wakati wa majanga.


“Tuko hapa kwa ajili ya kuwafuta machozi wafanyabiashara waliokata bima nasi kupitia mikopo yao ama waliokuwa na bima za mali bila mikopo, ambao walikuwa sehemu ya wahanga wa moto sokoni Kariakoo.


“Wito kwa Watanzania, moto wa Soko la Kariakoo uwe fundisho kwao juu ya umuhimu wa bima. Moto ama majanga huja bila kuyatarajia, unapokata bima unakuwa umejiwekea kinga kuilinda pesa ama mali uliyotafuta kwa jasho lako.


“Uwepo wa bima hukurejeshea nguvu haraka kana kwamba hakuna janga lililokutokea. Wito huu sio tu kwa bima za mikopo, bali mali zote kwani gharama za bima hizi ni nafuu mno,” Akisisitiza umuhimu na unafuu wa bima hizo, Massawe alitolea mfano wa bima ya moto kuwa hukatwa asilimia 0.25 ya thamani ya mali, na kwamba kama mali ya Sh. Mil. 100, makato yake ya bima ni Sh. 150,000 tu bila V.A.T kiasi ambacho ni rahisi kuliko bima za magari.


 Kwa upande wake, Joel Mwakalebela, ambaye ni Meneja Madai wa Kampuni ya Reliance Insurance, aliwapongeza wahanga hao kwa uamuzi wao wa kukata bima, huku akisisitiza Watanzania kutosubiri mikopo ili kukata bima, badala yake watumie huduma hizo ili kujilinda na majanga.


“Tunawashukuru NMB kwa ushirikiano huu mwema uliowezesha malipo ya haraka kwa wahanga hawa. Wito wetu kwa Watanzania ni kutumia huduma zetu, ambazo zinapatikana katika kila tawi la NMB lilipo kote nchini,” alibainisha Mwakalebela.


Akizungumza katika hafla hiyo, Emmanuel Mbise, ambaye ni mmiliki wa maduka 2 yaliyoteketea kwa moto, alifichua kuwa maumivu waliyoyapata wahanga wa tukio hilo ni makubwa, lakini malipo ya bima kutoka NMB, yanawapa hafueni na faraja kubwa.


Naye Sajida Kagasheki, ambaye pia ni mmoja wa wahanga, alikiri kupata faraja kubwa kupitia malipo hayo ya bima, huku akiwataka Watanzania kukimbilia sana huduma za bima hasa kupitia NMB Bancassurance, ambazo ni mkombozi na mfariji wa kweli wakati wa matatizo kama ya moto, vifo, ulemavu, upotevu na kadhalika.


No comments:

Post a Comment