Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki. |
WAZIRI
wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki amewataka watanzania kuupuuza uzushi
uliojitokeza kutokana na kusambazwa kwa ujumbe wenye taarifa za
kupotosha kuhusu kuingizwa kwa mayai nchini kutokea nchi jirani na
kusababisha soko la mayai yanayozalishwa nchini kushuka bei.
Akizungumza Juni 17, 2021 ofisini kwake katika Mji wa Serikali Jijini Dodoma,
Waziri Ndaki alisema baada ya kuona ujumbe huo Juni 15 Mwaka huu,
Wizara ya Mifugo na Uvuvi ilifanya uchunguzi kwenye makao makuu ya mikoa
yote 26 nchini na baadhi ya wilaya ili kujiridhisha juu ya upatikanaji
wa mayai, bei ya trei ya mayai na soko lake kwa ujumla.
Hatua
hiyo inatokana na uwepo wa ujumbe unaozunguka kwenye mitandao ya
kijamii kuhusu kuingia kwa mayai mengi nchini kutoka nje ya nchi kiasi
cha kusababisha kushuka kwa bei ya mayai mpaka kufikia Shilingi 4,000/=
kwa trei.
Ujumbe huo ulikuwa na kichwa cha habari kinachosomeka “SOKO LA MAYAI DSM KITENDAWILI”. Alisema
njia zilizotumika kukusanya taarifa ni pamoja na kuongea na wafugaji
wakubwa wa kuku wa mayai, wafanyabishara wakubwa na wadogo wa mayai.
Alisema
pia walilazimika kufika sehemu za masoko wanakouza mayai na kujionea
hali halisi ikiwa ni pamoja na kujua bei ya trei la mayai, upatikanaji
wake na hali ya soko kwa ujumla.
Waziri
huyo alisema pia walitumia fursa ya kuongea na maafisa mifugo wa mikoa,
majiji, manispaa na halmashauri ili kupata taarifa juu ya bei ya trei
la mayai, upatikanaji wake na hali ya soko la mayai kwenye maeneo yao ya
kiutawala.
Akizungumzia
matokeo ya uchunguzi huo, Waziri Ndaki alisema mayai yanayozalishwa
nchini ni kidogo kiasi kwa sababu ya uhaba wa vifaranga wa kuku wa mayai
na tatizo la uhaba wa vifaranga limekuwepo tangu mwaka 2020 kutokana na
mlipuko wa ugonjwa wa COVID 19 duniani uliosababisha uingizaji nchini
wa vifaranga wa kuku wazazi kupungua sana.
Alisema
hali hiyo imesababisha idadi ya kuku wa mayai wanaotaga kwa sasa kuwa
wachache na kusababisha kuwepo na uhaba wa mayai nchini huku matokeo
zaidi ya uchunguzi yanaonesha kwamba bei ya trei la mayai katika ngazi
ya mfugaji ni kati ya Shilingi 6,500/= mpaka 9,000/=.
“Vilevile
bei ya trei la mayai sokoni ni Shilingi 6,800/= katika baadhi ya mikoa
mpaka Shilingi 12,000/= kwa mikoa ukiwemo wa Katavi lakini bei ya yai
moja sokoni au madukani ni kati ya Shilingi 250/= mpaka 500/=” Alisema
Alisema
mtu aliyezusha taarifa hizi za uongo ana nia ovu na tasnia ya ufugaji
kuku Tanzania na ameleta taharuki kubwa kwa wafugaji wa kuku na jamii
yote ya Tanzania, suala la uhaba wa vifaranga linafanyiwa kazi na
kufikia mwezi wa Septemba, 2021 hali itakuwa imesharudi kama kawaida.
“Wizara
inakanusha vikali taarifa zinazonguka kwenye mitandao ya kijamii kuwa
hakuna wingi wa mayai uliosababisha kushuka kwa bei ya mayai katika
ngazi ya mfugaji na sokoni kinachoonekana zaidi ni kuwa kuna upungufu
mkubwa wa mayai nchini uliosababisha bei kupanda mpaka kufikia Shilingi
12,000/= kwa teri” Alisema Waziri huyo.
Alisema
taarifa zilizosambazwa ni uzushi mtupu na hazina ukweli wowote kutokana
na kwamba serikali ilishazuia uingizwaji wa kuku na mazao yake kutokana
na uwepo wa tishio la ugonjwa wa mafua makali ya ndege Duniani.
Aidha,
Wizara imekuwa ikitoa vibali maalum vya kuingiza vifaranga na mayai ya
kutotolesha ya kuku wazazi na kumekuwa na matukio machache ya uingizaji
wa mayai nchini kwa njia za panya lakini wizara imekuwa ikidhibiti hali
hiyo.
Hata hivyo alisema
mwezi Aprili mwaka huu chama cha wafugaji wa kuku kiliomba makampuni ya
kuku yaruhusiwe kuingiza vifaranga wa kuku wa nyama, vifaranga wa kuku
wa mayai na mayai ya kutotolesha kutokana na uhaba mkubwa wa vifaranga
nchini na serikali imeruhusu kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia Juni
mpaka Agosti 2021 na Tayari makampuni kadhaa yameshaanza kuingiza nchini
vifaranga na mayai ya kutotolesha na hivi karibuni tatizo hili
litafikia ukomo.
Katika
hatua nyingine waziri huyo, akizungumzia hali ya ugonjwa wa homa ya
nguruwe na jitihada zinazochukuliwa kukabiliana na tatizo hilo alisema
wizara ilitoa taarifa kwa umma kupitia vyombo vya habari juu ya kuwepo
kwa mlipuko wa ugonjwa wa homa ya nguruwe (African Swine Fever) katika
maeneo ya mikoa ya Mwanza, Kagera, Shinyanga na Dodoma.
Alisema
katika taarifa yake aliwaagiza wakuu wa Mikoa, wakuu wa Wilaya na
wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kusimamia kikamilifu
utekelezaji wa masharti ya karantini zilizokuwa zimewekwa na wataalamu
wa mifugo hasa kwa vile ugonjwa huo hauna chanjo wala tiba na
walisimamia vyema zoezi hilo.
Aidha
alisema wizara imekuwa ikifanya juhudi kubwa kudhibiti ugonjwa huu na
mpaka kufikia mwishoni mwa Mwezi Aprili, 2021 sehemu nyingi za nchi
hakukuwa na matukio ya ugonjwa huo.
“Mnamo
tarehe 01/06/2021 katika Manispaa ya Morogoro kulijitokeza matukio ya
nguruwe 14 kufa na uchunguzi wa kimaabara ulionesha ugonjwa wa homa ya
nguruwe “Alisema
Alieleza
kwamba tayari juhudi kubwa za kuudhibiti zinaendelea ambazo ni pamoja
na kuweka zuio (karantini) ya kuingiza na kutoa nguruwe na mazao yake
katika Manispaa ya Morogoro tangu tarehe 03/06/2021 na elimu kwa
wafugaji na wadau wengine wa nguruwe njia za kukinga ugonjwa usiingie
kwenye mabanda ya nguruwe.
Alieleza
kwamba mpaka kufikia tarehe 17/06/2021 hali ya ugonjwa katika Manispaa
ya Morogoro ulikuwa umedhibitiwa na hakuna kifo tena kilichotokea kwa
nguruwe.
Hata hivyo
alisema Juni 9 mwaka huu wizara ilipata taarifa juu ya uwepo wa ugonjwa
wa homa ya nguruwe katika Jiji la Dar es Salaam.
Alisema
baada ya kufanya uchunguzi katika mashamba ya nguruwe, ilibainika
kuwepo kwa taarifa za nguruwe 298 kufa katika mashamba mawili kwa kile
kilichodhaniwa ni ugonjwa wa homa ya nguruwe.
Alieleza
baada ya kuchunguza kwa kina kwa wanyama waliokuwa wamebaki kwenye
mashamba hayo pamoja na kuchukua sampuli na kuzipima katika maabara,
ilibainika kuwa ilikuwa sio ugonjwa wa homa ya nguruwe.
Aliongeza
kwamba ufuatiliaji zaidi ulifanyika kwenye sehemu zote za machinjio ya
nguruwe Dar es Salaam na kuchunguza nguruwe wanaochinjwa, hapakuwa na
viashiria vyovyote vya ugonjwa wa homa ya nguruwe. Wizara kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo inaendelea na juhudi za kudhibiti kabisa ugonjwa huu nchini.
No comments:
Post a Comment