Maafisa Wakaguzi wa Ndani na Nje wakifuatilia mkutano huo.
Madiwani wakishiriki kikamilifu kwenye ajenda ya Mkutano huo Maalum.
Mweka Hazina wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Revocatus Mohabe, akizungumza kwenye mkutano huo.
Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Miraji Mtaturu kwa niaba ya Wabunge, Madiwani na Watendaji wote wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi akimkaribisha rasmi wilayani hapo Mkuu wa Mkoa Dk. Mahenge na Katibu Tawala Mkoa Doroth Mwaluko kwa kumkabidhi zawadi ya Mbuzi kama ishara ya upendo na mshikamano.
Na Godwin Myovela, Singida.
MKUU wa Mkoa wa Singida Dk.
Binilith Mahenge ameagiza Halmashauri zote mkoani hapa kuanza mchakato wa
kutenga maeneo ya mashamba makubwa kama ajenda mahususi ya kufanikisha
ongezeko la uzalishaji wa zao la alizeti kwa wawekezaji.
Dk. Mahenge aliagiza hayo
aliposhiriki na kuhutubia Mkutano Maalum wa Baraza la Madiwani la Halmashauri
ya Wilaya ya Ikungi mkoani hapa jana, ambalo lilikutana kujadili majibu ya
Hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha
ulioishia Juni 30, 2020.
Agizo hilo limelenga kupunguza
hali halisi iliyopo ya uhaba wa uzalishaji wa ndani wa mafuta ya kula,
ambapo kiwango cha mafuta hayo kinachozalishwa nchini kwa sasa ni Tani
150,000 pekee, ikilinganishwa na kiwango kikubwa cha takribani Tani
300,000 ambazo huagizwa kutoka nje ya nchi ili kutosheleza mahitaji.
"Tutakuwa na wawekezaji
wakubwa hapa Singida watakaohitaji kuanzia ekari 500 hadi 1000, hivyo
tunahitaji mashamba makubwa ili tuongeze wigo mpana wa uzalishaji na tija
ya zao hili," alisisitiza Dk. Mahenge.
Alisema kwa sasa viwanda vingi
vya ukamuaji mafuta ya alizeti vilivyopo mkoani Singida vinafanya kazi
chini ya uwezo, yaani vinazalisha kwa miezi 3 pekee kwa mwaka kisha
vinazimwa kwa miezi 9 iliyobaki kutokana na uhaba wa malighafi.
Hata hivyo, Dk. Mahenge alihamasisha kila mwana-Singida na yeyote anayehitaji kuwekeza kwenye alizeti ndani ya mkoa huo milango ipo wazi, na atapewa kila aina ya ushirikiano katika kufanikisha azma yake hiyo.
Alisema Mkoa huo una hali ya
hewa rafiki, na kutokana na jiografia yake ndio kiini hasa cha ustawi
sahihi wa zao hilo, huku akisisitiza upana wa soko lake kwamba mkulima
haitaji kwenda nje ya nchi kutafuta soko kutokana na uhitaji mkubwa wa bidhaa
hiyo uliopo nchini.
"Serikali ya Awamu ya Sita
imeamua kulivalia njuga suala la alizeti na tayari imeteua mikoa mitatu ya
Singida, Dodoma na Simiyu kwa ajili ya kuelekeza nguvu kuhakikisha zao
hili linaleta tija," alisema Dk. Mahenge .
Katika hatua nyingine, Mkuu
huyo wa mkoa alipongeza juhudi kubwa inayofanywa na watendaji wa
Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi kwa kuwa waaminifu kwenye eneo la ukusanyaji
wa mapato, sambamba na kutumia vizuri kwa mujibu wa sheria za matumizi ya
fedha za Serikali.
"Nilipofika Singida na
kupewa taarifa za maendeleo ya mkoa na kufungua baadhi ya vitabu
nikaona Ikungi mko vizuri kwenye eneo hili, kwa sasa mmevuka malengo kwa kukusanya
asilimia 82 mkizidisha ile 80 ya lengo. Na naambiwa hapa kwa miaka saba mfululizo
mmekuwa mkipewa hati safi...hongereni" alisema Dk. Mahenge.
Katika hilo aliwataka kuongeza
jitihada hizo mara mbili zaidi ili kuifanya halmashauri hiyo kuwa namba
moja kitaifa, na hatimaye kuleta chachu ya mageuzi ya kiuchumi kwa wana-Ikungi
na Singida kwa ujumla.
Aidha, alitoa wito kwa
Halmashauri zote za Mkoa kusimamia vyanzo vyote vya mapato ipasavyo ili
kuinua mapato, huku akisisitiza kwamba kila chanzo kilichopo kiainishwe na
kuhakikisha kinachangia asilimia 100 kwa usimamizi wake.
"Na katika hili nasisitiza
sana ili tufanikiwe ni lazima tukubali mabadiliko na mkubali kubadilika
tushirikiane kama timu moja ili wananchi wetu wapate maendeleo," alisema.
Dk. Mahenge.Kwa upande wake,
Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Ally
Mwanga alimhakikishia Mkuu wa mkoa kwamba watampa kila aina ya ushirikiano,
huku akisisitiza utayari wao wa kutoa mashamba makubwa kulingana na mahitaji
ya uwekezaji katika kuunga mkono juhudi zilizopo kwenye uzalishaji wa zao
la alizeti.
Kuhusu ajenda ya hoja za ukaguzi, Mkaguzi wa Ndani Mkoa wa Singida, Naomi Kalinga aliipongeza Ikungi kwa kufanikiwa kufanyia kazi vizuri hoja za ukaguzi kwa kuzipunguza kutoka 71 hadi 26, jambo linalothibitisha kuwa kuna kazi kubwa imefanyika.
Aidha, Kalinga aliwataka
kutobweteka na badala yake waendelee kuwa waaminifu na kuchapa kazi bila
ya kuruhusu hoja zilizofungwa kujirudia, ili kuifanya Ikungi kuwa mahali
salama pa kufanyia kazi.
Mkaguzi Mkuu Mkoa (CAG) Nkanyila Makawa, akikazia hilo aliwasihi watumishi na watendaji wote wa mkoa kuendelea kufuata sheria za matumizi ya fedha za Serikali ili kuepuka hoja zisizo za lazima zinazoweza kuibuliwa na jicho la pili ambalo liko nyuma ya kila mtumishi.
No comments:
Post a Comment