Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Tanga, Jabir Singano, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani), ofisini kwake Septemba 22, 2026 kuhusu uzinduzi wa Kliniki ya Ardhi itakayo fanyika wilayani Muheza.
WANANCHI wa Mkoa wa Tanga wametakiwa kujitokeza kwa wingi katika uzinduzi wa Kliniki ya Ardhi utakaofanyika kuanzia kesho katika Wilaya ya Muheza, kwenye viwanja vya Stendi ya Bombani mkoani humo.
Wito huo umetolewa na Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Tanga, Jabir Singano, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Septemba 22, 2026, ofisini kwake kuhusu uzinduzi wa kliniki hiyo.
“Tunawaomba wananchi wajitokeze kwa wingi katika uzinduzi huo wa kliniki, ambayo ni muhimu hasa katika kuwapa wananchi uelewa kuhusu masuala mbalimbali ya ardhi,” alisema Jabir.
Alisema katika kliniki hiyo, huduma mbalimbali zitatolewa, ikiwa ni pamoja na kusikiliza migogoro ya ardhi na kuitafutia ufumbuzi.
“Pamoja na kutoa huduma hizo, pia tutatoa hati kwa wananchi ambao watakuwa wamekamilisha taratibu zote zinazotakiwa kufuatwa,” alisema.
Aliongeza kuwa kliniki hiyo imekuwa ikifanyika kila mwaka nchini kote kwa madhumuni ya kutoa elimu kwa jamii kuhusu masuala ya ardhi, sambamba na kusogeza huduma zinazotolewa na Wizara ya Ardhi karibu na wananchi.
Uzinduzi wa kliniki hiyo utadumu kwa siku 10, kuanzia Septemba 22, 2026 hadi Oktoba 1, 2026.
Jabir alisema kutokana na jitihada zinazofanyika hivi sasa katika Mkoa wa Tanga, migogoro ya ardhi imepungua kutokana na elimu inayotolewa kwa wananchi kuhusu masuala ya ardhi.
Amewataka wananchi kuacha kutumia madalali wanapohitaji kumiliki ardhi, akisema baadhi yao wamekuwa wakiwaingiza wananchi katika migogoro mbalimbali, badala yake watumie ofisi za ardhi pamoja na Halmashauri husika.
Aidha, amewataka wamiliki wa ardhi mkoani humo, wakiwemo wawekezaji, kuzingatia masharti ya mikataba waliyopewa baada ya kumilikishwa ardhi, ikiwa ni pamoja na kuendeleza maeneo yao na kuweka alama za mipaka ili kuepuka migogoro ya ardhi baina yao na wananchi.
Kwa upande wake, Msajili Msaidizi wa Hati Mkoa wa Tanga, Mwajuma Kihiyo, amewataka wananchi kutovamia maeneo ambayo siyo yao na yaliyoachwa wazi, akisema baadhi ya maeneo hayo yameachwa kwa ajili ya shughuli za kijamii.
Akizungumzia kliniki hiyo, Kihiyo alisema imelenga kusogeza huduma karibu na wananchi na kutatua changamoto mbalimbali zinazohusu masuala ya ardhi.
Msajili Msaidizi wa Hati Mkoa wa Tanga, Mwajuma Kihiyo, akisisitiza jambo kwenye mkutano na waandishi wa habari...............................
Habari hii imeandikwa na Dotto Mwaibale namba ya simu 0754362990

No comments:
Post a Comment