Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mkoa wa Tanga, Castro John, akizungumza na waandishi wa habari katika mahojiano maalumu yaliyofanyika ofisini kwake Septemba 16, 2026.
..........................
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), Mkoa wa Tanga imerekodi Ufanisi wa Asilimia 139 katika Makusanyo ya Kodi ambapo kwa miezi imekusanya Shilingi Bilioni 104.9 zaidi ya lengo la Bilioni 75.7 walizopangiwa.
Hayo
yameelezwa na Meneja wa TRA Mkoa wa Tanga, Castro John, wakati akizungumza na
waandishi wa habari katika mahojiano maalumu yaliyofanyika ofisini kwake
Septemba 16, 2026.“
"Miezi hii miwili ya Julai na Agosti tulipangiwa kukusanya Shilingi Bilioni 75.7 lakini tumekusanya Shilingi Bilioni 104.9," alisema John.
Ni kazi nzuri na ni utendaji wa asilimia 139, hivyo niendelee kuwashukuru walipa kodi kwa mwitikio wao wa ulipaji kodi kwa hiyari uliopelekea kuleta mafanikio haya,” alisema John.
Aidha, alitoa shime kwa wafanyabiashara kuendelea kushirikiana na kufanya kazi kama timu, na pale wanapoona kuna eneo linataka kuwavuta nyuma basi wakae pamoja kuzungumza kama wanavyofanya wakati wote.
John aliongeza kuwa mara zote ili kuboresha utendaji kazi wamekuwa wakikaa na viongozi wa wafanyabiashara na wafanyabiashara wenyewe.
Kwa mfano, kesho Septemba 17, 2026 watakutana na viongozi wa sekta ya mahoteli.
“Hayo tunayafanya katika kuhakikisha kwamba tunaboresha mazingira ya kufanya kazi, kuboresha ‘Team work’ kwa pamoja na sisi tuendelee kuwezesha biashara zao,” alisema John.
Meneja huyo alitumia nafasi hiyo kutoa wito kwa wafanyabiashara wote kuwa kama wanavyojua huu ni mwezi wa kulipa kodi awamu ya tatu, hivyo wafanyabiashara wenye wajibu wa kulipa kodi yao kwa awamu hiyo wafanye hivyo kabla ya Septemba 30, 2026.
Akisisitiza ulipaji kodi, alisema kutokulipa kuna madhara makubwa ikiwemo kulipa faini au kulipa riba—fedha ambayo ingemsaidia mfanyabiashara kuongeza mtaji wa biashara yake, hivyo alisisitiza wafanyabiashara wote kuzingatia jambo hilo.
Katika hatua nyingine, aliwashukuru wafanyabiashara wa Mkoa wa Tanga kwa namna ambavyo wanajitokeza na kushirikiana kwa pamoja, na jinsi wanavyolipa kodi kwa hiyari ambapo kumekuwa na mwitikio mkubwa.
" Pia niwashukuru viongozi wa vyama vya wafanyabiashara kama vile Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT), TWCC, TACC na vingine vyote; wamekuwa na mchango mkubwa kwa kuhakikisha TRA Tanga inaendelea vizuri na makusanyo ambayo Serikali inayapata,” alisema,"
Aidha, alimshukuru Mkuu wa Mkoa na vyombo vyake vyote, pamoja na wakuu wa wilaya kwa jinsi ambavyo wanafanya kazi kwa karibu kuhakikisha shughuli hiyo muhimu ya kukusanya mapato ya Serikali inafanyika.
John alieleza kuwa Mkoa wa Tanga una fursa ya mipaka ambayo inaunganisha na nchi jirani. Kwa mfano, mpaka wa Horohoro ambao unaunganisha na Kenya, na hata Bandari ya Tanga ambayo inapokea mizigo mbalimbali pamoja na Bandari ya Pangani ambapo kote kumekuwa na mwitikio mzuri wa ulipaji kodi.
“Niseme tu Tanga kulikuwa na shughuli za magendo kwa bidhaa nyingi kutoka nje kupitishwa katika mipaka isiyo rasmi, lakini sasa shughuli hizo zimepungua, jambo ambalo limesaidia mapato kuongezeka kwa upande wa forodha,” alisema.
John alisema kazi kubwa ya TRA ni kuwezesha biashara, hivyo ipo kwa ajili ya kazi hiyo ambapo alitoa rai kwa wafanyabiashara ambao bado wanafanya biashara za magendo kuacha kufanya hivyo na kwenda kujisalimisha.
Aliongeza
kuwa kuna operesheni nyingi ambazo wanazifanya kwa kushirikiana na vyombo
vingine vya Serikali, na wakibainika watakamatwa na vyombo vya moto
vitakavyokutwa vimebeba bidhaa hizo vitataifishwa na wahusika kufungwa.
Alisema kwa upande wa nchi, madhara ya magendo ni pamoja na kukosa takwimu sahihi kwa ajili ya shughuli za maendeleo.
John aliongeza kuwa madhara mengine ni kuwa katika mipaka ya nchi kuna taasisi zaidi ya 15 wakiwemo watu wa Afya ambao wanaangalia ubora wa bidhaa, hivyo bidhaa za magendo zinaweza kuhatarisha afya za watumiaji.“
Vita vya
kuzuia magendo ni vya Watanzania wote na ni wajibu wa kila mtu. Anapoona
magendo yakifanyika na kuacha bila kutoa taarifa, yanaweza kumuathiri pia,”
alisema John.
Mmoja wa Wafanyabiashara wa duka la vifaa vya ujenzi mkoani hapa, ambaye ni mmiliki wa Kampuni ya Taifa Store, Abbas Karimjee ameipongeza Serikali kupitia TRA kwa namna walivyo wawekea mazingira mazuri ya ulipaji kodi ambapo alitumia nafasi hiyo kuwahimiza wafanyabiashara wenzake kulipa kodi kwa wakati.
................................
Habari hii imeandikwa na Dotto Mwaibale simu namba 0754362990.

No comments:
Post a Comment